MS, ndani ya ACT hakujengwi chama; kunajengwa mtu. Ndani ya ACT hakuna demokrasia, kama kungekuwa na demokrasia kusingekuwa na mgogoro kati “wavamizi” wanaoongozwa na Zitto na genge lake; na wenye chama chao, wanaoongozwa na Lucas Kadawi Limbu, mwenyekiti mwanzilishi wa ACT Tanzania.

Limbu na wenzake leo hii, wako mahakamani kupinga kinachofanywa na Zitto, Prof. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.

Kama Zitto angekuwa mkweli, asingefanya mapinduzi ya chama kwa kubadilisha katiba kinyemela; falsafa ya chama, kadi za chama, nembo ya chama na jina la chama.

Ndani ya ACT kuna jitihada mahususi za kufukuza waasisi ili kumuandalia mtu mmoja makazi ya kisiasa; na mwenye maslahi binafi.

Nakubaliana na wewe kuwa mwenyekiti wa chama - Anna Elias Mughira, kwa jina jingine, Anna Shadrack Maghiya, siyo lolote siyo chochote. Amefanywa kama boya linaloelea baharini baada ya kukata nanga.

Anayeitwa kiongozi mkuu wa chama, ndiye mkuu wa chama kwenye mikutano mikuu ya chama taifa, Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC). Kiongozi mkuu wa chama, ndiye anayekuwa mkuu wa siasa, mshauri na mwelekezaji kwa viongozi wote na maafisa wa ACT-Tanzania.

Hata nafasi yake – Kiongozi Mkuu wa Chama – hakuna utaratibu wa kuigombea. Je, iko wapi demokrasia ambayo yeye na genge lake wamekuwa wakidai kuipigania?

Mbona mwenyekiti hana mamlaka ya kuagiza, kuteuwa; na au kuelekeza katibu mkuu wa chama ama mfanyakazi mtumishi mwingine wa chama? Madaraka yote yametupwa kwa kiongozi mkuu wa chama.
Iko wapi tofauti ya mfumo wa utawala wa kiongozi mkuu na utawala wa kifalme?

Katiba ambayo Zitto na wenzake wanatumia inasema, pamoja na mengine, kiongozi mkuu ndiye atateua wajumbe watano wa kamati kuu; ndiye mtoa tamko rasmi kuhusu masuala ya sera na mtazamo wa chama; mtoa habari mahususi kwenye mkutano mkuu, NEC na CC na masuala mengine ya kitaifa na kimataifa.

Kitila na wenzake wanaimba kuwa Zitto sasa ndiye atakuwa “nuru na taswira ya ACT-Tanzania ambayo wamegeuza jina na kuita ACT-Wazalendo."

Katika mifumo ya kidemokrasia, “nuru na taswira” ya chama inakuwa mtu mmoja? Ni kitu gani hasa? Ni “zidumu fikra za Zitto?” Fikra zipi” Ni wanachama kumwacha Zitto awapeleka anakotaka? Ni ufalme wa Zitto?

Inawezekana kuwa hilo ndilo alikuwa anatafuta katika Chadema – na alikiri kuandaa – kupindua uongozi na watendaji ili achukue chama na kubaki dikiteta mkuu katika mfumo anaouita wa kidemorasia?

Yako wapi majigambo ya kupigania demokrasia? Kwa hili, hata wale ambao Zitto anatuhumu udikiteta, hawajawahi kujiundia uungu wa aina hii.

Source: Mwanahalisi online.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top