Bi. Nusrat Hanje akitoa mada katika kikao cha Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) mkoani Shinyanga |
WANAWAKE
nchini wamekumbushwa umuhimu wa kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua na
kuchaguliwa kuwa kiongozi na kushauriwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao nchini badala ya kuwaachia
wanaume peke yao.
Hali hiyo
imeelezwa na katibu wa Baraza la Vijana wa CHADEMA kutoka jimbo la
uchaguzi la Kigamboni jijini Dar es Salaam, Nusrat Hanje alipokuwa akitoa mada
kwenye mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA
(BAWACHA) mkoani Shinyanga.
Hanje
alisema wanawake wengi nchini mara nyingi hushindwa kujitokeza kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi katika maeneo yao kutokana na kuendekeza mfumo dume ambao
umekuwa ni moja ya changamoto kwao na hivyo wakati wa chaguzi mbalimbali wao
hubaki wakiwa ni wapiga debe wa wagombea wa kiume.
“Sisi
wanawake wengi nchini bado tunakabiliwa na mfumo dume, hii ni changamoto kubwa
kwetu, na ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa tushindwe kujitokeza katika
chaguzi mbalimbali kiserikali hata ndani ya vyama vyetu na hivyo kukosa fursa
za kuongoza katika maeneo yetu,”
“Sasa leo
tupo hapa moja ya mada yetu kuu ni uhamasishaji wanawake kujitokeza katika
kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu
unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwishoni, na tuweke mikakati ya jinsi ya
kupata ushindi katika uchaguzi huo,” alieleza Hanje.
Hata hivyo
aliwaasa wanawake hao kutokubali kutoa rushwa au kujirahisi na kukubali kutoa
miili yao kimapenzi kwa wasimamizi wa uchaguzi na viongozi wa chama chao pale
watakapokumbana na vikwazo kwa lengo la kutaka kupewa upendeleo wa kuteuliwa
katika mikutano ya kura za maoni.
Hanje
aliwakumbusha wanawake hao kwa wale ambao ni waumini wa kikristo kwamba ndani
ya kitabu kitakatifu cha biblia imeelezwa wazi kwamba, “…mwili wako ni hekalu
takatifu, usithubutu kulichafua kwa njia yoyote ile.”
“Ni vizuri
tukajiamini, tuache kuuogopa mfume dume, tujisimamie wenyewe lakini tuhakikishe
tunajiepusha na vishawishi vya aina yoyote pale tutakapokutana na vikwazo
mbalimbali katika kipindi hiki cha uchaguzi, tuepuke kujirahisi kiasi cha kutoa
rushwa, hasa ile ya ngono, ni mbaya sana, miili yetu ni sawa na hekalu
takatifu, hivyo tusiichafue,” alieleza.
Kwa upande
mwingine Hanje aliwatahadharisha wana CHADEMA kutahadhari na kuwaepuka kama
ukoma wagombea watakaokuwa wakipitapita huku wakigawa rushwa ya vitu mfano wa
chumvi, dagaa, khanga, vipande vya sabuni, kofia na T-shirt kwa lengo la
kutaka wachaguliwe kuwa madiwani au wabunge.
Kwa upande
wake mbunge wa viti maalum katika Jimbo la Shinyanga mjini kwa tiketi ya
CHADEMA, Rachel Mashishanga akisisitiza suala la wanawake kujitokeza kugombea
uongozi alisema ili uwiano ulio sawa kati ya wanaume na wanawake uweze
kupatikana katika vyombo vya kiuongozi nchini ni lazima wanawake pia wajitokeze
kugombea.
Mashishanga
alisema usawa katika nyanja za kiuongozi hauwezi kupatikana iwapo wanawake
daima watakuwa wakijirudisha nyuma na kwamba wao ndiyo wazalishaji wakubwa wa
mali ndani ya familia lakini bado wameendelea kukabiliwa na umaskini
uliokithiri kutokana na mfumo dume uliozoeleka miongoni mwao wa wakiamini
wanaume ndiyo vichwa vya familia.
Alisema njia
pekee ya kujinasua katika dimbwi la umaskini na kuondokana mfumo dume ni
wanawake kujitokeza na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi sambamba na
wanaume na kuweza kuleta mabadiliko ya kweli badala ya kuendelea kuwa wahanga
wa mabadiliko
Post a Comment