Mwenyekiti mwenza wa UKAWA, James Mbatia. |
VIONGOZI WA UKAWA KATIKA MOJA YA VIKAO VYAO. |
WAKATI TUKIELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 25, 2015,
UKAWA WADAI MAMBO MANNE, JE!! SERIKALI ITAYARIDHIA????
Mambo manne yanayodaiwa na Ukawa ambayo ni
ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50, mgombea binafsi katika
nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya uchaguzi na urais kupingwa
mahakamani ni yale yaliyoafikiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya
siasa Septemba 8, mwaka jana.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia
amesema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ni
ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa Katiba Mpya na
kuondoa uwezekano wa vurugu.
Katika kikao hicho, Mbatia alisema walitiliana
saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977,
Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba
na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari, jambo ambalo pia
halikufanyika.
Utekelezaji wa masuala hayo utawezekana iwapo
Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni ili yajadiliwe kwa dharura
katika mkutano ujao wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la Kumi, kwa kuwa uwezekano wa
kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.
Alipoulizwa iwapo jambo hilo linawezekana katika
Mkutano wa Bajeti, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Ndiyo
inawezekana. Serikali inaweza kuwasilisha jambo hili kwa dharura na
litajadiliwa na Kamati ya Uongozi, kama ikiona linafaa litapelekwa bungeni
kujadiliwa.”
Katika hilo Mbatia alisema: “Bado kuna nafasi ya
Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa kufanyika kama ambavyo tulikubaliana
na Rais kupitia TCD.”
Alisema ushauri wa TCD kwamba mchakato wa Kura ya
Maoni uahirishwe hadi mwakani umepuuzwa na matokeo yake yameonekana wazi na kwa
msingi huo, suala la kurekebisha maeneo hayo manne, si la kupuuza hata kidogo.
“Hili lisipofanyika utaibuka mgogoro mkubwa. Tatizo
la Serikali yetu ni kutotaka kutekeleza mambo yanayoonekana wazi kuwa na
mkanganyiko, ndiyo sababu ya kukithiri kwa migogoro ya wakulima, wafugaji,
wafanyakazi na mingine mingi,” alisema Mbatia.
DKT. WILLIBROD SLAA YEYE ALONGA!!!
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
endapo Serikali itashindwa kutekeleza makubaliano hayo, vyama vya upinzani
havina budi kuingia katika mapambano kwa katiba hiyohiyo.
“Kama hatumwelewi Rais Kikwete katika suala hili,
basi hatuwezi kumwelewa tena. Sioni juhudi zozote za Serikali kubadili maeneo haya.
Tulikubaliana naye mambo mengi lakini yote ameshindwa kuyatekeleza, hata hili
pia hawezi kulitekeleza,” alisema Dk Slaa.
Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema umefika
wakati wa vyama vya upinzani kupambana hivyohivyo licha ya kuwapo tume ya
uchaguzi isiyo huru.
“Nimeshinda ubunge Karatu vipindi vitatu na tume ikiwa
ni hiihii. Wapinzani tuna wabunge zaidi ya 100, nadhani tupambane tu,” alisema.
Alisema umefikia wakati wa kuing’oa CCM kwa
kutumia Katiba mbovu (iliyopo sasa) na kinachotakiwa kufanywa na vyama vya
upinzani ni kujipanga kuanzia vijijini hadi mijini ili kuzoa kura zote.
“Tumeshinda Kawe, Ubungo, Mbeya Mjini na hata
Nyamagana. Tuache kulialia sasa, twende katika mapambano. Kwanza Bunge lijalo
ni la Bajeti na kwa vyovyote vile mabadiliko tunayoyataka hayawezi kufanyika,”
alisema.
SOURCE: Mwananchi
News.
Post a Comment