Rais wa Marekani, Barrack Obama akipeana mkono na Rais wa Cuba, Raul Castro.
Rais Barack Obama wa Marekani na mwenzake wa Cuba, Raul Castro, wamekutana na kupeana mikono kwenye Mkutano wa Kilele wa Mataifa ya Amerika unaoendelea nchini Panama.


Afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani amethibitisha kuwa viongozi hao wawili walisalimiana na kuzungumza kwa muda mfupi, lakini akasema mazungumzo hayo hayakuwa rasmi.

Obama na Castro wanatazamiwa kukutana tena leo na kuzungumzia jitihada zao za kurejesha mahusiano, kuimarisha biashara na kutembeleana baina ya nchi zao.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kilele, Rais Obama alisema Marekani sasa ina sera mpya kuelekea majirani zake, akisisitiza kuwa zama za nchi yake kuchukuliwa ni mbabe mbele ya wenzake zimepita.

Ingawa siasa za Obama kuelekea mataifa ya Amerika Kusini inapongezwa, mwezi uliopita ziliingia doa baada ya utawala wake kutangaza vikwazo dhidi ya Venezuela, mshirika mkubwa wa Cuba.

Rais Nilocas Maduro wa Venezuela amepanga kumkabidhi Obama barua iliyosainiwa na mamilioni ya raia wake kutaka kuondoshwa kwa vikwazo hivyo, akisema anaamini ataungwa mkono na Rais Castro wa Cuba na viongozi wengine wa mrengo wa shoto.

Source: DW Swahili

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top