Ni wanyama wachache sana wanaotambulishwa zaidi na
bara la Afrika kama alivyo Twiga. Lakini sasa mnyama huyo anakabiliwa na
kitisho cha kutoweka kutokana na imani kwamba uboho wake unatibu ukimwi.
Twiga ni mnyama maarufu katika ukanda wa Savannah
kama walivyo Kangaruu kwa nchi ya Australia. Kwa urefu wa shingo yake wa hadi
mita mbili Twiga ndiyo mnyama mrefu zaidi duniani na amekuwa akivinjari katika
ukanda wa Savannah wa bara la Afrika tangu enzi. Nchini Tanzania Twiga ni
mnyama wa taifa, lakini pamoja na hadhi yake hiyo, mnyama huyo anakabiliwa na
kitisho kikubwa cha kutoweka.
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya
Twiga imepungua kwa kiwango cha kustusha, anasema Marlies Gabriel, raia wa
Namibia mwenye asili ya Ujerumani, ambaye pamoja na mume wake wanaendesha
biashara ya nyumba ya wageni katika mbuga ya wanyama ya Arusha, na
wanajishughulisha na utunzaji wa mazingira ya asili katika mkoa huo.
Hadi miaka
michache iliyopita, wanyama hao walikuwa wanakutikana kwa wingi katika maeneo
yanayozunzunguka mlima Meru, lakini leo hii wageni katika mbuga hiyo wanapaswa
kutafuta muda mrefu hadi kumuona Twiga.
Sababu kuu ni ujangili.
Sababu za kupungua kwa wanyama hao ni zile za
siku zote - ujangili. Twiga wanaweza kuuawa kwa wepesi mno kwa kutumia risasi
moja tu au waya, unasema mtandao wa taasisi ya uhifadhi wa Twiga GCF, ambayo
ndiyo taasisi pekee duniani inayojishughulisha na uhifadhi wa wanyama hao,
iliyoanzishwa mwaka 2009.
Watu zaidi na zaidi wanazidi kuamini kuwa uboho
wa mifupa ya Twiga unaponya magonjwa yanayohusiana na ukimwi, alisema Peter,
muongozaji wa wageni, ambaye ameshuhudia kupungua kwa idadi ya Twiga katika
maeneo ya Mlima Meru, Kilimanjaro na mfumo wa ekolojia wa Ambosile kwenye mpaka
kati ya Tanzania na Kenya.
Wataalamu kutoka taasisi ya GFC wanasema kilo
moja ya uboho wa Twiga inaweza kuingiza hadi dola za Marekani 120. Hii siyo
mara ya kwanza kwa wababaishaji kuuwa wanyama kwa visingizio vya kuwa viuongo
vyao ni tiba ya maradhi, kuongeza nguvu za kiume na haiba ya mtu. Uwindaji wa
tembo na faru kwa ajili ya pembe zao umewapelekea wanyama hao kwenye kingo za
kutoweka kabisaa.
Punguzo la asilimia 40.
Twiga, ambao wanapatikana katika mataifa 21
wamebainishwa kwenye orodha nyekundu ya shirika la uhifadhi wa mazingira asili
IUCN kama wanyama wasio hatarini. Lakini kupungua kwa wanyama hao kwa asilimia
40 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, kunabainisha kwamba hatua za ulinzi
zinahitajika hivi sasa kuliko huko nyuma.
Mwaka 1998 idadi ya Twiga ilikadiriwa kuwa
140,000, lakini kwa mujibu wa GFC, idadi hiyo ilikuwa imeshuka chini ya 80,000
kufikia mwaka 2012. Katika baadhi ya maeneo ambayo yanachukuliwa kama makaazi
ya asili ya Twiga, idadi ya wanayama hao imepungua kwa hadi asimilia 65. Ikiwa
Twiga watatoweka, dunia itapoteza moja ya spishi maarufu zaidi.
Shughuli za binaadamu.
Pamoja na ujangili, wanyama hao wanakabiliwa pia
na kitisho cha kutanuka kwa makaazi ya wanaadamu. Marlies Gabriel, anasema
mashuhuda waliripoti juu ya kuchinjwa kwa wanyama hao na raia, na pia katika
mbuga ya wanyama ya Serengeti, wageni waliripoti kukutana na mizoga ya Twiga.
Licha ya kupiga hatua kadhaa za kimaendeleo,
Tanzania bado inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa maskini zaidi duniani, na
hivyo raia wengi wanapendelea kujihusisha zaidi na kilimo na ufugaji kuliko
uhifadhi wa mazingira. Hilo limaanisha janga kwa wanyamapori wa eneo hilo.
Chini ya utawala wa rais wa kwanza Julius Nyerere
katika miaka ya 1960 na 1970, adhabu ya kuwinda Twiga ilikuwa kifo, anasema
Gabriel na kuongeza kuwa inatisha zaidi hivi sasa kuona kwamba wanyama hao
wanatoweka taratibu.
Source: DW News
Post a Comment