TIMU ya
kombaini ya mpira wa miguu kutoka kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga
imeibuka kidedea katika mashindano ya kugombea kombe la Mashishanga baada ya
kuwachapa wapinzani wao timu ya Veterani ya mjini Shinyanga kwa mabao 4 – 1.
Kufuatia
ushindi huo timu hiyo ilikabidhiwa rasmi kombe la ubingwa huo lenye thamani ya
shilingi laki nne, fedha taslimu shilingi 500,000 na mipira mitatu ambapo
mshindi wa pili, Veterani walikabidhiwa fedha taslimu shilingi 300,000, seti ya
jezi na mipira miwili huku mshindi wa tatu timu ya kata ya Ngokolo walipata
shilingi laki mbili na mipira miwili.
Kwa upande wa
mchezo wa mpira wa pete wanawake, timu ya Polisi Shinyanga iliyojinyakulia
kombe na fedha taslimu shilingi laki tatu ambapo mshindi wa pili timu ya walimu
manispaa alipata shilingi laki mbili na mipira miwili huku timu ya ShyCom
ikiibuka na ushindi wa tatu iliyojinyakulia shilingi laki moja na mipira
miwili.
Akikabidhi zawadi
kwa washindi wa mashindano hayo yaliyozishirikisha timu 17 za mpira wa miguu
kutoka kata zote za manispaa ya Shinyanga na sita za mpira wa pete mgeni
rasmi, Askofu Edson Mwombeki alimpongeza mwandaaji wake mbunge wa viti maalum
kwa tiketi ya CHADEMA, Rachel Mashishanga kwa uamuzi wa kukuza michezo jimboni.
Mwombeki
alisema kupitia michezo hiyo mbali ya kuibua vipaji vya vijana lakini pia
imeweza kuongeza mshikamano miongoni mwao bila kujali itikadi ya vyama vyao vya
siasa na kwamba michezo hiyo itawasaidia vijana hao kujitangaza na kuweza
kujiunga na timu kubwa ambapo hivi sasa michezo ni sehemu ya ajira.
Naye mbunge
Mashishanga alisema lengo la kuandaa mashindano hayo maarufu kwa jina la
Mashishanga Cup ni kutaka kuwaweka pamoja vijana wa jimbo la Shinyanga na
kujijenga kiafya na pia kukuza vipaji vyao katika michezo hiyo pamoja na kuwapa
sehemu ya kupata burudani wakazi wa Shinyanga.
“Ndugu zangu
mbali ya kutoa shukrani zangu za dhati kwa ushiriki wenu katika mashindano haya
lakini niwaeleze lengo lake kubwa ni kujenga mahusiano mazuri miongoni mwetu
bila kujali itikadi za vyama vyetu vya siasa, na huu ni mwanzo tu, lakini hivi
karibuni natarajia kuendesha mashindano mengi kwa upande wa mbio za baiskeli,”
alieleza Mashishanga.
Hata hivyo
mbunge huyo aliishauri serikali iangalie uwezekano wa kuwatengea fungu maalumu
wabunge wa viti maalumu ili liweze kuwasaidia katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya kimaendeleo katika majimbo wanayoyaongoza ikiwemo michezo kama
inavyofanyika kwa wabunge wa majimbo.
Post a Comment