Deus Kibamba muwezeshaji katika mdahalo wa Mwenendo na Athari za mabadiliko ya tabia nchi.
 
Deus Kibamba kutoka Jukwaa la katiba akiwasilisha mada juu ya mikakati ya uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi nchini.
Sehemu ya washiriki wa mdahalo uliofanyika kata ya Mwandoya wilayani Meatu.
 
SHUGHULI mbalimbali za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo ya hifadhi za misitu mikubwa zimetajwa kuwa ndiyo chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mengi nchini hali ambayo inaweza kusababisha athari kubwa isipodhibitiwa mapema.
 
Hali hiyo imebainishwa katika mdahalo wa kijamii ulioandaliwa na Muungano wa Azaki za kiraia wilayani Meatu (MENGONET) uliofanyika katika kata ya Mwandoya wilayani Meatu mkoa wa Simiyu kwa ufadhili wa Shirika la The Foundation For Civil Society.
 
Mmoja wa wawezeshaji katika mdahalo huo, Deus Kibamba kutoka Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam alisema mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha mvua katika maeneo mengi kutokunyesha kwa mpangilio yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya mabadiliko ya tabia nchi kulikosababishwa na uharibifu wa mazingira.
 
Kibamba alisema kwa kadri shughuli za kibinadamu zinavyoongezeka kwenye maeneo ya hifadhi za misitu ipo hatari hata mazao yanayolimwa hivi sasa yakashindwa kusitawi vizuri na kusababisha kupatikana kwa mavuno machache na hivyo nchi kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.
 
Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na binadamu wenyewe wanaofanya shughuli za uharibifu wa mazingira pasipo kuzingatia athari zitakazotokana kitendo cha kuharibu misitu ovyo katika maeneo yao na kwamba hivi sasa hata baadhi ya mazao ya asili hayapatikani katika maeneo mengi mfano wa uyoga wa asili.
 
Kibamba alisema hata hivyo baadhi ya mataifa makubwa yaliyoendelea ikiwemo nchi ya Urusi ndiyo yaliyokithiri katika uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na maendeleo ya kiviwanda yaliyopo katika nchi zao na kwamba hivi sasa yanataka kulitumia bara la Afrika kusaidia kunyonya sumu za taka mbalimbali zinazozalishwa katika mataifa hayo.
 
“Baadhi ya mataifa makubwa duniani ndiyo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea katika maeneo mengi hasa katika bara letu la Afrika, wenzetu wana uwezo wa kutengeneza njia mbadala za kukabiliana na uharibifu huo tofauti na sisi ambao wengi wetu ni maskini,”
 
“Kwa hali hii ni lazima tuhamasishane wenyewe kwa wenyewe kuhakikisha tunatunza na kuilinda kwa nguvu zote misitu yetu mikubwa iliyosalia sambamba na upandaji wa miti mingi katika maeneo yetu ya makazi, tusipochukua tahadhari mapema ipo hatari ya kupata athari kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi,” alieleza.
 
Alisema mpaka hivi sasa kasi ya ukataji miti kwa ajili ya shughuli za kibinadamu katika maeneo mengi nchini imekuwa ikiongezeka na haiendani na kasi ya upandaji wa miti mipya na kwamba kila mtu anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake ili kuepusha uharibifu wa misitu na mazingira katika maeneo wanayoishi.
 
“Hivi sasa katika maeneo mengi watu wanalalamika kuwepo kwa ongezeko kubwa la joto, lakini hawajiulizi kwa nini hali hiyo inatokea, ni wazi kuwa kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira ndiyo sababu ya ongezeko la joto, sasa tuhimizane kupanda miti kwa wingi, mbali ya kutoa kivuli lakini pia miti hunyonya hewa chafu,” alieleza Kibamba.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top