Mji wa Katoro jana ulizizima kwa mabomu ya
machozi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wanafunzi na wananchi waliofunga
barabara kuu ya Geita Bukoba waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuwawekea
matuta ili kuepukana na ajali.
Tafrani hiyo ilikuja baada ya mwanafunzi Mussa Joseph
(9), wa darasa la nne, Shule ya Msingi Ludete, kugongwa na kufa wakati akivuka
barabara katika eneo la stendi mpya Katoro.
Sinema nzima ilianza saa mbili asubuhi baada ya
ajali hiyo ambapo wakazi wa eneo hilo wakishirikiana na wanafunzi wa Shule za
Msingi Ludete na Mkapa kufunga barabara kwa mawe huku wakiwa wameshika
silaha mbalimbali.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Katoro, Gervas Daudi,
akizungumza eneo la tukio alidai kuwa mwanafunzi huyo aligongwa na pikipiki
hiyo majira ya saa tano asubuhi wakati akivuka barabara akitoka shuleni hapo.
Alisema mwanafunzi huyo ambaye amezikwa jana nyumbani
kwao Katoro alifariki dunia papohapo kutokana na pikipiki hiyo kuwa kwenye
mwendo kasi na dereva wake hakuweza kusimama kuhofia kupigwa na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, alifika
eneo la tukio na kuamuru uongozi wa halmashauri ya wilaya, walimu
waliohamasisha vurugu hizo wachukuliwe hatua za kinidhamu na kwamba walimu
wakuu wa shule hizo washushwe vyeo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Joseph Konyo
alithibitisha tukio hilo ingawa hakutaka kuzungumzia kwa undani kwa kuwa mkuu
wa wilaya alikwishalizungumzia.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kalifonia, Elias Muembeni
alisema wanafunzi hao wamechukua hatua ya kufunga barabara baada ya
kuwapo kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo.
“Hadi sasa zaidi ya watu watano wamekwishapoteza
maisha kwa kugongwa na magari pamoja na pikipiki katika eneo hili,” alisema
Muembeni.
Aliongeza: “Badala ya kutumia
busara, waliamua kulala barabarani wakiwa tayari kwa lolote na kudai
wasingetoka hadi matuta yawekwe ndiyo maana foleni ya magari imekuwa
kubwa kama unavyoiona.’
Chanzo cha Habari: Gazeti la Mwananchi.
Post a Comment