Shirika la haki za binaadamu
Human Rights Watch limesema katika ripoti yake mpya kuhusu Burundi, kwamba
majeshi ya nchi hiyo na polisi walifanya mauaji kiasi ya 47 kati ya Desemba 30
2014 na Januari 3 mwaka huu 2015.
Mauaji
hayo yalifuatia mapigano yaliozuka dhidi ya kundi la watu waliokuwa na silaha
katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Cibitoke (CHIBITOKE). Ripoti ya Shirika
hilo imesema vijana wa chama tawala waliokuwa na silaha pia walishiriki katika
mauaji hayo.
Mkurugenzi
wa Shirika hilo anayehusika na Afrika Daniel Bekele amesema majeshi ya Burundi
yana wajibu wa kuwalinda raia dhidi ya machafuko na matumizi ya nguvu, lakini
haina maana kuwauwa wale iliowakamata. Akaongeza kwamba inaelekea wanajeshi na
Polisi hawakufanya jitihada yoyote kuwakamata watu waliosalimu amri, lakini
badala yake wakawapiga risasi.
Mauaji
ya Cibitoke ni sehemu ya mpango mpana wa mauaji wa majeshi ya Burundi na
wanachama wa Umoja wa vijana wa chama tawala CNDD-FDD wnaojulikana kama
Imbonerakure, matukio yanayoanzia miaka mingi nyuma.
Wahanga wa mauaji hayo ni
pamoja na raia na wanachama wa makundi yenye silaha pamoja na wale wanaotuhumiwa
kuwa wapinzani. Mauaji ya Cibitoke ni mojawapo ya matukio makubwa kabisa ya
aina yake katika miaka ya karibuni.
Taarifa
chache zilizopatikana kuhusu kundi moja lililokuwa na silaha, zinaeleza kwamba
lilivuka mpaka kuingia Burundi kutokea nchi jirani Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo mwezi Desemba mwaka jana.
Mashahidi
na duru za kijeshi zinasema waliohusika walikuwa wamejizatiti kwa silaha.
baadhi ya waliokamatwa waliliambia Shirika la Human Rights watch kwamba lengo
lao lilikuwa kuunda kambi msituni mashariki mwa Cibitoke, ambako zingetokea
harakati zao dhidi ya serikali ya Burundi.
Mashahidi
wamesimulia mauaji mwanzoni mwa mwezi Januari, katika msitu wa Kindindi karibu
na wilaya za Mpinga na Murwi na pia baina ya milima ya Ngoma na Rugano,
wakishiriki pia vijana wa Imbonerakure neno lenye maana ya " Muuwe huyo
mbwa."
Mkurugenzi
wa Afrika wa Shirika la haki za binadamu human Rights watch Bekele, amesema
maafisa wa Burundi wanapaswa kufanya uchunguzi ulio wazi na kuhakikisha
wahusika wamefikishwa mbele ya sheria.
Mara
nyingi tume zilizopita kuhusiana na uchunguzi wa matukio ya aina hiyo
zilichukua msimamo wa kisiasa. Ripoti hiyo ya Human Rights watch inaelezea
matukio mengi.
Wizara
wa mambo ya nchi za nje ya Marekani ilisema katika taarifa tarehe tano mwezi
huu, kwamba inasumbuliwa na ripoti ya kuhusika majeshi ya usalama ya Burundi
katika mauaji ya wanachama 24 wa kundi moja la waasi baada ya kujisalimisha
mapema mwezi uliopita mkoani Cibitoke.
Human
Rights watch limesema nchi kama Uholanzi zinaisaidia Polisi ya Burundi na
Marekani inalipa msaada jeshi la Burundi. Limezitaka nchi hizo zishinikize
pafanyike uchunguzi huru na wa uwazi na kuifahamisha wazi serikali ya Burundi
kwamba hawatoweza kuendelea kuzisaidia taasisi au vikosi vinavohusika katika
ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, na kwamba maafisa wanajukumu la
kuwawajibisha wahusika kwa kuwafikisha mahakamani.
Post a Comment