Mbio
za kuusaka urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kupamba
moto baada ya kundi la wabunge wapatao 150 kujitokeza hadharani na
kueleza kumuunga mkono mmoja wa wanaotajwa kuwa wagombea, Edward
Lowassa, wakimtaka kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Hali hiyo inajitokeza wakati wa Mkutano wa Bunge wa 18
ukihitimishwa mwishoni mwa wiki na kubakia miwili tu Bunge la 10 kufikia
tamati, hivyo kwa kila hali uchaguzi mkuu kuzidi kunukia kazi kubwa
ikiwa ni kupatikana kwa rais wa tano wa Tanzania.
Kwa kitambo sasa kumekuwa na makundi yanayosigana kila moja likiwa
na mgombea wake, hata hivyo mpambano mkubwa wa kumpata mgombea
unaonekana kuwa zaidi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kurithi mikoba
ya Rais Jakaya Kikwete, anayehitimisha uongozi wake wa utawala Oktoba
mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mbio hizo, sasa ni rasmi kwamba kundi la wabunge wanaodaiwa
kufikia 150 walikutana katika chakula cha jioni mjini Dodoma eneo la
Kilimani mwishoni wiki iliyopita wote waliopata fursa ya kuzungumza
katika hafla hiyo, walisema wazi kuwa wanamuunga mkono Lowassa katika
mbio za urais.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani,
anadaiwa kutakiwa na wabunge hao kuwa muda ukifika achukue fomu za
kuwania urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika
Oktoba mwaka huu.
Ingawa kumekuwa na tetesi na minong’ono ya Lowassa kuungwa mkono
ndani ya CCM kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ambayo pia itampa fursa
ya kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, uamuzi wa wiki iliyopita wa wabunge
hao kusimama hadharani unaibua moto mkubwa wa kinyang’anyoro cha urais
huku jina la Lowassa likizidi kutajwa kama chaguo la wengi.
Habari ambazo NIPASHE imezipata zinasema kuwa wengi wa wabunge
waliozungumza walitaja sifa za kuwania urais, wakisisitiza kuwa Lowassa
anazo na kwamba ni mtu pekee kwa sasa wanaoona kuwa CCM inaweza kuingia
kwenye uchaguzi ikiwa na uhakika wa ushindi kama ataipeperusha bendera
ya chama hicho.
Katika hafla hiyo ambayo pia Lowassa anadaiwa kuhudhuria, mbunge
mmoja mkongwe mkoani Kagera (CCM), anadaiwa kusema kuwa wabunge marafiki
wa Lowassa wanamuomba agombee kutokana na kuwa na sifa zote za uongozi
hasa katika zama za sasa ambazo taifa linahitaji mtu wa kulikwamua.
"Mimi as a senior citizen (kama raia mkongwe), huu ni mwaka muhimu,
Oktoba tutakuwa na uchaguzi mkuu wa kumchagua kiongozi atakayeisukuma
mbele nchi yetu… sote tunafahamu chama chetu bado hakijatangaza
taratibu, lakini sisi wabunge marafiki zako tunakuomba, muda ukifika
chukua fomu kwa sababu unatosha," vyanzo vyetu vilimnuku mbunge huyo
akimshawishi Lowassa katika hafla hiyo.
Mbunge huyo anadaiwa kuainisha sifa muhimu za kiongozi kuwa ni
mwenye elimu madhubuti, uwezo wa kuona mbali (vision), muwajibikaji na
mchapakazi, uwezo wa kutenda na tabia nzuri, vitu ambavyo alisema kuwa
Lowassa anavyo hasa akirejea rekodi yake ya uwaziri mkuu kati ya 2005
hadi Februari 2008.
"Kule kwangu wananiuliza yule waziri mkuu aliyeleta hizi shule za
kata yuko wapi? Mimi nawajibu atarudi tu. Na kila mtu mitaani anataja
jina lako kwa hiyo sauti ya watu (wengi) ni sauti ya Mungu," alisema
mbunge huyo.
Wabunge wengine ambao walipata fursa ya kuzungumza ni pamoja na
Viti Maalum (Singida), Diana Chilolo, mbunge shabiki wa klabu ya Simba
atokaye mkoa wa Tanga(CCM), Mary Chatanda wa Viti Maalum (CCM) na mbunge
kutoka Ruvuma ambaye ni kada muhimu wa kuipigia debe CCM katika kila
kipindi cha uchaguzi.
Chilolo anadaiwa kuungana na mbunge mkongwe kutoka Kagera, akisema
kuwa Lowassa ni chaguo la wengi, huku mbunge kutoka Tanga akinukuliwa
akisema kuwa Lowassa ni binadamu mwenye imani na upendo wa hali ya juu.
"Huyu mzee mbali ya uwezo mkubwa wa kufanya kazi, lakini ana
huruma... mimi niko tayari kufukuzwa CCM kwa kumuunga mkono Lowassa,”
alisema mbunge kutoka Tanga.
Pia mbunge huyo (kutoka Tanga), anadaiwa kuahidi kuwa atatumia
nafasi yake kuhakikisha kwamba watu wote wanamuunga mkono Lowassa.
Mbunge huyo wa Tanga anadaiwa kusema kuwa kwa kumuona Chatanda katika hafla hiyo, kunadhihirisha kukubalika kwa Lowassa.
Chatanda ambaye pia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, inaaminika
kuwa alikuwa hasimu mkubwa wa Lowassa wakati akiwa katibu wa chama
tawala mkoa wa Arusha.
Habari zinasema kuwa Chatanda na Lowassa walikuwa na uhasama mkubwa
na wote waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa mkoani Arusha walionja
makali ya Chatanda.
Vyanzo vya habari vilivyojipenyeza kwenye hafla hiyo iliyofanyika
baada ya iliyokuwa imeandaliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, vinasema
kuwa Chatanda mwenyewe aliposimama kuzungumza alikiri kuwa alikuwa
hamuungi mkono Lowassa pamoja na kwamba wanafahamiana kwa muda mrefu,
lakini sasa anaungana na wale wanaomuomba agombee.
"Mimi na Edward hatuna ugomvi, wapambe wake ndiyo walikuwa
wanatuchonganisha, na kwa kweli sikuwa kabisa namuunga mkono, lakini
wagombanao ndiyo wapatanao…mimi sasa hivi nimeingia mwili mzima kumuunga
mkono Edward na hakuna wa kunitoa," chanzo chetu kinamnukuu Chatanda,
akitangaza msimamo mpya wa kisiasa katika makundi ya kusaka urais
kupitia CCM.
Kutokana na msimamo huo mpya, habari zinasema kuwa Chatanda alipigiwa makofi na wabunge wenzake.
Hata hivyo, alipotafutwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana kuelezea
tukio hilo, Chatanda alikanusha vikali, akieleza kuwa hakuwapo kwenye
chakula hicho na wala hafahamu chochote kuhusiana na hafla hiyo.
"Mimi sikuwapo, na wala sijui kama hicho kitu kilikuwepo, sijui chochote na wewe ndiyo kwanza unaniambia," alisema.
Naye Chilolo alipotafutwa, alikanusha kushiriki hafla hiyo, akisema
kwamba hata Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliandaa chakula cha jioni
siku hiyo lakini hakuweza kuhudhuria kwa sababu hakuwa anajisikia
vizuri.
"Spika aliandaa chakula cha jioni, nasikia watu walikula,
walikunywa na kuserebuka... sasa ningewezaje kuacha kwenda kwa Spika
niende kwa Lowassa?" alisema Chilolo.
Naye mbunge kutoka Ruvuma ambaye alishatangaza siku nyingi kuwa
anamuunga mkono Lowassa katika safari yake kuelekea Ikulu, anadaiwa
kusema kuwa ushahidi wa kukubalika kwa Lowassa ulidhihirika wakati wa
kilele cha sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea Februari Mosi mwaka
huu, kutokana na kushangiliwa na uwanja mzima mara alipowasili.
"Sikilizeni niwaambie... miye nilikuwapo uwanjani, wale wengine
wote hawakushangiliwa pamoja na kutembea mbali na jukwaa ili watu
wawaone. Lakini huyu Lowassa alivyoteremka mbele tu ya jukwaa kuu,
uwanja mzima ulilipuka," vyanzo vyetu vilimnukuu mbunge huyo akisema
kwenye hafla hiyo.
Naye mbunge wa jimbo mojawapo linaloaminika kuwa ni ngome ya CCM
jijini Dar es Salaam ananukuliwa akimuelezea Lowassa kama kiongozi
shupavu na makini.
"Uwezo wake naujua... kwa kweli tunajifundisha mengi kutoka kwake," alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo kutoka Dar es Salaam alipotafutwa kwa njia ya simu
jana, alisema yuko msibani Kipunguni A kulikotokea maafa ya moto na
kuteketeza ndugu sita wa familia moja, hivyo asingeweza kueleza
chochote.
Naye mbunge kutoka Zanzibar (CCM), anayesifika kwa kuwa mkali kila
mara linapofikia suala la kutetea maslahi ya visiwa hivyo, ananukuliwa
akimuomba Lowassa kukubali ombi lao kwani anatosha kwenye kiti cha
urais.
Habari za ndani zinasema kuwa Lowassa ambaye hata hivyo hajatangaza
rasmi nia ya kuwania urais, aliposimama kujibu kauli za wabunge hao,
anadaiwa kusema suala la urais ni jambo zito hivyo kwa sasa anamwachia
kwanza Mungu.
"Ndugu zangu nafarijika sana kwa kauli zenu, lakini hili suala la
urais ni kubwa, tumuachie huyu aliye juu (Mungu), yeye akiamua liwe
linakuwa," vyanzo vyetu vilimnukuu Lowassa akisema wakati wa hafla hiyo.
Ombi la wabunge hao limekuja miezi michache baada ya matokeo ya
utafiti wa Taasisi ya Twaweza, kuonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa
kukubalika miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.
Matokeo ya utafiti huo ambayo yalitolewa mwishoni mwa mwaka jana
yalionyesha kuwa iwapo uchaguzi mkuu ungefanyika wakati huo, Lowassa
angeibuka mshindi kwa asilimia 13, wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
angefuatia kwa karibu akiwa na asilimia 12 huku Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk. Willibrod Slaa akiwa wa tatu kwa asilimia 11.
Hata hivyo, asilimia 33 ya wananchi waliohojiwa walisema bado hawajaamua wampigie kura mgombea gani.
Utafiti huo wa Twaweza ulifanywa Septemba 2014 kwa kuwahoji wananchi 1,445 kutoka Tanzania Bara.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment