Rais wa zamani wa Yemen Jumamosi (21.02.2015) ametoroka kutoka kifungo
cha nyumbani cha wiki kadhaa mjini Sanaa nyumba yake ikiwa imezingirwa
na waasi wa Kishia
Washauri
walio karibu naye wamesema kwamba Rais huyo wa zamani Abd Raboo Mansour Hadi
ameondoka Sanaa na tayari amewasili katika mji mkuu wa iliokuwa Yemen ya kusini
Aden ambapo wafuasi wake wamegoma kuyatambuwa mamlaka ya baraza la rais
lililowekwa na wanamgambo wa Kihouthi kuchukuwa nafasi yake.
Ameondoka
mjini Sanaa akiwa kwenye msafara wa magari kadhaa kwa kupitia mji wa tatu kwa
ukubwa nchini humo wa Taiz ambao kama vile Aden hauko chini ya udhibiti wa
waasi wa Kishia wa kundi la Wahouthi.
Afisa
mwandamazi wa uslama mjini Aden ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Hadi
mwenye umri wa miaka 69 anakaa kwenye kasri la rais katika kitongoji cha
kidiplomasia cha mji huo wa bandari wa Yemen kusini ambako ndiko alikozaliwa.
Aliwababaisha walinzi
Washauri
wake wanasema kwamba Hadi ambaye amekuwa kwenye kifungo cha nyumbani kwa wiki
kadhaa kufuatia mapinduzi ya waasi hao wa Kishia anapanga kuondoka nchini
kwenda nje kwa ajili ya matibabu.
Washauri
hao wameongeza kusema kwamba waasi wamemuachia Hadi kutokana na shinikizo
kutoka Umoja wa Mataifa,Marekani,Urusi na vyama kisiasa ndani ya nchi hiyo.
Hata
hivyo mjumbe wa kamati kuu ya kundi la Wahouthi Ali al-Quhum ameliambia shirika
la habari la Ujerumani dpa kwamba Hadi alitoroka kifungo hicho cha nyumbani kwa
kuwakwepa walinzi kwa kuwababaisha.
Afisa
huyo mwandamizi pia amekaririwa akisema hayo na tovuti ya habari ya ndani ya
nchi ya al-Akhbar na kuongeza kwamba hakuna tena maana iwapo rais huyo wa
zamani ameendelea kubakia hapo au kuondoka.
Wahouthi walivyodhibiti serikali
Wanamgambo
wa kundi la Wahouthi ambao ngome yao kuu iko nyanda za juu kaskazini wanakoishi
Washia wengi waliuteka mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa hapo mwezi wa Septemba bila
ya upinzani.
Mwezi uliopita waasi hao waliiteka Ikulu na kuyazingira makaazi ya
Hadi jambo lililopelekea rais huyo kujiuzulu.
Kwa
mujibu wa mashahidi baada ya Hadi kuondoka kwenye makaazi yake Wahouthi walifanya
uporaji kwenye nyumba yake na kwamba watu watatu walionekana wakitoka na
bunduki za aina ya Kalashnikov kutoka kwenye nyumba hiyo.
Jamal
Benomar mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen amesema hapo Ijumaa kwamba makundi
yanayohasimiana nchini humo yamekubaliana kuunda baraza jipya la kutunga sheria
litakalojumuisha Wahouthi, wabunge wa zamani na wapya kuiongoza nchi hiyo
katika kipindi cha mpito.
Lakini
muungano wa vyama vya kisiasa nchini humo umeukataa mpango huo kwa hoja kwamba
haukidhi haja ya kuleta ufumbuzi kamili.
Ahmed
Lakaz msemaji wa chama cha Mkusanyiko wa Vyama vya Wafanyakazi ambacho kilikuwa
kinashiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Yemen amesema
kwamba vyama hivyo vimewaeleza Wahouthi kwamba hawatashiriki katika mchakato
huo iwapo Hadi hatoachiliwa.
Kutumbukia kwenye mzozo wa kisiasa
Yemen
imetumbukia kwenye mzozo wa kisiasa tokea waasi wa kundi la Wahouthi kuuteka
mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa na baadae kulazimisha kujiuzulu kwa rais
aliyechaguliwa anayeungwa mkono na mataifa ya magharibi na kulivunja bunge
wakati wakimweka Hadi kwenye kifungo cha nyumbani.
Wakati
huo huo waasi hao wa kundi la Wahouthi Jumamosi walijaribu kuvamia kambi ya
kikosi maalum ilioko nje ya mji mkuu na kushambuliana kwa risasi na wanajeshi
wa kikosi hicho ambao wengi wao ni tiifu kwa Ali Abdallah Saleh mtangulizi wa
Hadi. Kwa mujibu wa maafisa wa usalama mapigano hayo yameuwa watu watatu.
Washauri
wa Saleh wanasema kiongozi huyo wa zamani anaiona kambi hiyo kuwa muhimu kwa
uhai wake na kamwe hatoruhusu iangukie mikononi mwa Wahouthi kama vile
ilivyokuwa kwa vituo vyengine vya kijeshi ambavyo tayari viko mikononi mwa
Wahouthi.
Washauri wake hao wamezungumza hayo kwa masharti ya kutotajwa jina
kutokana na kwamba Saleh hakuwaruhusu wazungumze na waandishi wa habari.
Maandamano dhidi ya Wahouthi yaendelea
Maelfu
ya watu pia wameandamana Jumamosi kumuunga mkono Hadi katika mji wa kusini
wajimbo la Ibb ambapo wamewataka Wahouthi kuondoka katika eneo hilo na kuacha
kuingilia kati masuala ya ndani ya jimbo hilo.
Duru za usalama zinasema Wahouthi
waliwafyetulia risasi na kuuwa mwandamanaji mmoja na kujeruhi wengine wawili.
Waasi
hao wa kundi la Wahouthi walijipenyeza hadi kwenye maeneo yanayokaliwa na
Wasunni wengi kusini na magharibi mwa mji mkuu wa Sanaa ambapo walikabiliana na
upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa kikabila na wanamgambo wa kundi la Al
Qaeda.
Mji
wa Taiz na baadhi ya sehemu nyengine za kaskazini halikadhalika eneo zima la
kusini mwa Yemen hayako chini ya udhibiti wa waasi hao.
Mzozo
huo wa kisiasa nchini Yemen pia unauweka mashakani uwezo wa Marekani kuendeleza
operesheni zake za kupambana na ugaidi hususan kutokana na kuondolewa kwa Hadi
mshirika madhubuti wa Marekani.
DW News!!!
Post a Comment