Bayern Munich yabugizwa 4-1
Mabingwa wa Ujerumani
Bayern Munich wameanza vibaya sehemu ya pili ya msimu baada ya mapumziko ya
kipindi cha baridi, kwa kubugizwa magoli 4-1 na Wolfsburg iliyo katika nafasi
ya 2, kwenye mechi pekee ya jana usiku.
Haikuwa siku njema kwa mabingwa hao
wanaofundishwa na Kocha Pep Guardiola, ambao hadi wanakwenda mapumziko walikuwa
hawajashindwa mechi yoyote msimu huu. Kwa muda wa dakika tisini tu, Wolfsburg
ilikuwa imewabugiza magoli 4, idadi sawa na magoli iliyofungwa Bayern Munich
katika mechi 17 za sehemu ya kwanza ya msimu huu.
Mnamo dakika ya tatu tu ya mchezo mholanzi Bas
Dost aliunganisha pasi iliyochongwa na Daniel Caliguiri, na kuachia mkwaju
ambao kipa Manuel Neuer wa Bayern Munich aliusindikiza kwa macho hadi kwenye
kona ya wavu. Juhudi za Bayern kutaka kuzawazisha ziliishia pachungu, baada ya
Wolfsburg kuwageuzia kibao, katika shambulizi lililohitimishwa kwa goli la pili
lililotiwa kimiani na yule yule Bas Dost.
Mkuki kwa nguruwe, kwa
binadamu mchungu
Magoli mawili kwa nunge yaliwafanya wachezaji
wa Bayern ambao hawakuzoea kujikuta katika hali hiyo wakipoteza subira, na
kucheza rafu iliyopelekea kadi ya njano kwa kiungo wao Xabi Alonso, ambaye
alionekana kupandwa na jazba. Hadi mapumziko ubao wa magoli ulionyesha
Wolfsburg 2, Bayern Munich 0.
Kama mabingwa hao walidhani watarekebisha mambo
katika kipindi cha pili ilikuwa ni ndoto tu, kwani ilikuwa Wolfsburg iliyoliona
lango tena mnamo dakika ya 53 ya mchezo, kupitia mbelgiji Kevin de Bruyne,
aliyekimbia nusu ya uwanja, na kumtumia salamu kipa Neuer kwa nduki kutoka
umbali wa mita kumi.
Magoli matatu kwa sufuri ugenini yaliufanya
mlima wa Bayern Munich kuwa mrefu, lakini kwenye dakika ya 55 Juan Bernat
aliweza kurudisha bao moja ambalo liliishia kuwa pekee la kufutia machozi.
Haikuishia hapo kwani kauli ya mwisho ilitoka kwa Wolfsburg mnamo dakika ya 73,
pale yule yule Kevin de Bruyne aliposhindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza
la Bayern Munich kwenye mechi hiyo kwa kupachika bao la nne.
Guardiola akubali kipigo
Akizungumza na waandishi wa habari baaya ya
mechi, kocha wa Bayern Munich Pep Guardiola hakuwa na ukaidi. ''Ni kweli
walikuwa timu bora na walistahili ushindi'' alisema Guardiola, na kuongeza kuwa
magoli yao yaliingia katika muda mbaya kwa Bayern, yaani dakika za mwanzoni na
za mwishoni.
Kwa upande mwingine, kocha wa Wolfsburg Dieter
Hecking amewapongeza vijana wake, akisema ushindi huu unawapa ari ya kuendelea
kufanya vyema.
Kongo dhidi ya Kongo katika
kombe la Afrika la Mataifa
Na katika michuano ya kombe la Afrika la
Mataifa ambayo hii leo inaingia katika raundi ya robo fainali zitachezwa mechi
mbili jioni ya leo, ya kwanza ikiwa kati ya watani wa jadi, Kongo Kinshasa na
Kongo Brazzaville, ya pili itakuwa kati ya Tunisia, na wenyeji Guinea ya
Ikweta.
Akizungumzia mechi dhidi ya watani wao wa Congo
Brazzaville, kocha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Florent Ibenge, amesema
ni mchezo kati ya ndugu wanaotenganishwa tu na mto Kongo. Kocha wa Kongo
Brazzaville Claude Le Roy ambaye siku za nyuma aliifunza Kongo Kinshasa ameunga
mkono kauli ya mpinzani wake, akisema utakuwa mchuano baina ya ndugu wanaojuana
vyema, na kwamba hilo litaongeza msisimko.
Chanzo cha habari: DW Swahili.
Post a Comment