MTANZANIA USIKURUPUKE KUPIGIA KURA KATIBA USIYOJUA KILICHOMO NDANI YAKE |
MAMBO 20 MUHIMU YA WANANCHI YALIYOTUPWA NA KATIBA INAYOPENDEKEZWA.
UNATAKA KUUJUA UKWELI BASI SOMA HAPA NA MJULISHE MWENZIO.
Katiba Inayopendekezwa ina mapungufu makubwa na imeyatupilia mbali
maoni muhimu ya wananchi kama yalivyotolewa na wananchi wenyewe kama
ifuatavyo;-
1. Kupunguzwa kwa madaraka ya Rais Wananchi walipendekeza
madaraka makubwa ya Rais hasa ya uteuzi yapunguzwe na ziundwe Taasisi za
kikatiba za kumshauri Rais kabla hajafanya teuzi. Wananchi
walipendekeza pia baada ya Rais kumteua kiongozi basi itabidi mteuliwa
huyo Bunge limthibitishe. Katiba Inayopendekezwa imeyafuta haya yote na
imemuongezea Rais Madaraka.
2. Kutenganisha Mamlaka ya Mihimili
ya Dola Wananchi walipendekeza uhuru zaidi kwa Bunge na Mamlaka zaidi
kwa Bunge kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali. Pendekezo hili
linaenda sambamba na kutenganisha serikali na Bunge, hali ambayo iko
sasa. Rasimu ya Warioba ililipa Bunge Mamlaka zaidi kuisimamia Serikali
na hata pale ambapo Bunge lingekataa bajeti au muswada mbaya wa serikali
mara kadhaa, Rais asingeliweza kulivunja Bunge. Wananchi walisema sana
Mawaziri wasitokane na wabunge, ili wabunge wafanye kazi ya uwakilishi
pekee na mawaziri watumie weledi wao kumsaidia Rais kazi za Serikali.
3. Kumwajibisha Mbunge Rasimu ya Warioba iliwapa wapiga kura uwezo wa
kuwawajibisha Wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati
wowote (Recall Powers) kama wakienda kinyume na maslahi ya wananchi
katika jimbo husika. Wananchi walijiuliza kama mbunge ni mtumishi wao,
iweje hayuko katika kituo cha kazi kwa miezi kadhaa na wasiweze
kumwajibisha mpaka miaka mitano?
4. Vyanzo vya Mapato vya
kuaminika Kuwepo kwa vyanzo vya mapato vya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano vitakavyogharimia mambo ya Muungano ambayo yamepunguzwa kutoka
22 hadi 7 lilikuwa pendekezo ambalo hata taasisi za serikali
zilipendekeza. Pendekezo la Katiba Inayopendekezwa imerudisha mapato ya
Muungano kama Katiba ya Mwaka 1977, na kwa kufanya hivyo tumerudi kwenye
mgogoro wa msingi, kuchukua kodi tatu, ushuru wa forodha, ushuru wa
bidhaa na mapato kutoka Zanzibar ni kuiua Zanzibar na kuifanya ishindwe
kumudu matumizi yake ya ndani kwa mambo yasiyo ya Muungano na vivyo
hivyo kwa Tanganyika.
5. Muundo wa Shirikisho lenye Mamlaka
Kamili Kwa miaka nenda rudi tumekuwa na kitendawili cha ni muundo gani
wa Muungano Jamhuri yetu inao. Kitendawili hiki kimeelezwa na wengi
akiwemo Baba wa Taifa Mw. J.K Nyerere. Rasimu ya Warioba iliweka kwa
mara ya kwanza Muundo Jamhuri ya Muungano kuwa ni wa Shirikisho lenye
Mamlaka Kamili na lenye Serikali 3.
6. Kupunguza ukubwa wa
Serikali Wananchi walionesha kutofurahishwa na ukubwa wa serikali
unaopelekea matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi. Walipendekeza
uwepo wa serikali ya muungano iliyo imara, yenye ufanisi na ndogo.
Rasimu ya Warioba ilisema idadi ya mawaziri isizidi 15, Katiba
Inayopendekezwa inasema Mawaziri wasizidi 40.
7. Tume ya Uhusiano
na Uratibu Rasimu ya Warioba ililenga kuhakikisha kunakuwepo uhusiano
mzuri, mawasiliano na uratibu wa serikali zote tatu chini ya Mamlaka ya
Serikali ya Muungano na kupitia Tume ya Uhusiano na Uratibu. Bunge
Maalum lilishindwa kuelewa mantiki ya pendekezo hili na Katiba
Inayopendekezwa imelivuruga kabisa, kutoka pendekezo la Warioba la “Tume
ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali” hadi “Tume ya Uratibu wa Mambo ya
Muungano” katika Katiba Inayopendekezwa.
8. Kupunguza ukubwa wa
Bunge Wananchi walizungumzia pia ukubwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
na gharama zinazoambatana nalo, na wakapendeza bunge dogo na lenye
ufanisi mkubwa. Warioba alisema idadi ya wabunge isizidi 75, Bunge
Maalum likasema Wabunge 390.
9. Ukomo wa vipindi vya ubunge
Wananchi walizungumzia nafasi za ubunge kuhodhiwa na watu fulani kwa
miaka nenda rudi na wakapendekeza ifike mahali kuwe na ukomo ili kuleta
uwakilishi mpana na mabadiliko. Rasimu ya Warioba iliweka ukomo wa
vipindi vya ubunge kuwa vitatu na kuwa na ukomo wa miaka 15 kwa Bunge la
Jamhuri ya Muungano. Bunge Maalum na Katiba Inayopendekezwa wamefuta
pendekezo hili.
10. Kuwepo kwa Tunu za Taifa (Core Values)
Wananchi walipendekeza uwepo wa tunu za Taifa (core values) katika
katiba, tunu hizi ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya Taifa. Raia wa Tanzania walikuwa na wajibu wa
kuheshimu tunu hizi lakini Katiba Inayopendekezwa imezifuta tunu hizi.
11. Maadili na Miiko ya Viongozi Wananchi walizungumza kuporomoka kwa
kiasi kikubwa kwa maadili ya jamii, watumishi na viongozi wa umma, wengi
wakisema Katiba iainishe Maadili na miiko ya viongozi wa umma ambayo
kwayo tutawawajibisha. Katiba Inayopendekezwa imesema Maadili na Miiko
kwa viongozi (mathalani kutenganisha biashara na uongozi ili kuepusha
mgongano wa maslahi), isiwemo kwenye Katiba bali ikawekwe kwenye Sheria.
12. Masharti yasiyoweza kubadilishwa na Bunge Rasimu ya Warioba iliweka
masharti ya kuzuia Bunge kubadili baadhi ya masharti mahususi ya Katiba
(entrenched provision) ibara ya 119 isipokuwa kwa ridhaa ya wananchi
kupitia kura ya maoni (mathalan Malengo Makuu ya Taifa, Haki za Binadamu
n.k. Na bahati mbaya tulisahau kuweka na Sura ya 3 juu ya Maadili).
Masharti yote ya Ibara hii yamefutwa isipokuwa Muundo wa Muungano na
Uwepo wa Jamhuri ya Muungano.
13. Kuwepo kwa Tume Huru ya
Uchaguzi Wananchi walizungumza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi
ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano.
Ilisisitizwa juu ya umuhimu wa Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kwamba
Mwenyekiti wa Tume na Makamu wake wathibitishwe na Bunge ili kuwapa
uhalali wa kitaifa, pendekezo hili limefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
14. Usawa wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume Kuwepo uwiano wa
uwalikishi wa 50:50 kati ya wanawake na wanaume ni lazima kwa mazingira
ya sasa. Uwiano kati ya wanawake na wanaume katika vyombo mbalimbali vya
dola hasa vile vya kutung sheria limeendelea kuwa tatizo nchini na
lililokaa kwa muda mrefu. Wananchi na hasa wanawake na baadhi ya wanaume
walipendekeza uwiano ulio sawa katika kufikia fursa hasa ukizingatia
wanawake ndio wazalishaji wakubwa. Katiba Inayopendekezwa imefutilia
mbali pendekezo hili muhimu.
15. Kuanzishwa kwa Mgombea Huru Haki
ya wananchi kushiriki shughuli za umma imekuwa ikizuiwa siku nyingi na
kwamba ushiriki katika shughuli za umma kama kiongozi wa kuchaguliwa
inapaswa kuwa haki ya msingi ya mwananchi yeyote yule. Rasimu ilitoa
haki ya mgombea huru bila vikwazo, Katiba Inayopendekezwa imeweka
masharti magumu ambayo hakuna mtu anayeweza kuyatimiza kirahisi, kitendo
hiki sio sawa.
16. Msaada wa Kisheria kwa Wananchi Wananchi
walieleza kutokuridhishwa kwao na huduma za msaada wa kisheria kwa
wananchi wenye uhitaji huo na wakapenda huduma ya msaada wa kisheria
liwe suala la kikatiba kwa mwananchi yeyote yule na serikali iwajibike
kutoa huduma hiyo. Katiba Inayopendekezwa imesema wananchi hawatakuwa na
haki ya kudai huduma hii kokote nchini, hata mahakama hazitaweza
kusikiliza mashauri ama Serikali imetoa haki hii au haikutoa haki hii
rejea Ibara ya 21.
17. Uhuru wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Rasimu ya
Warioba ilipendekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi atekeleze kazi zake kwa
uhuru, bila woga, upendeleo wala chuki na kwa mujibu wa masharti ya
Katiba hii na sheria za nchi. Masharti haya yamefutwa na Katiba
Inayopendekezwa.
18. Tume ya Utumishi wa Jeshi la Wananchi Tume ya
Warioba ilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania itakayokuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya
utumishi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katiba
Inayopendekezwa imefuta masharti haya licha ya wapiganaji kupendekeza
utaratibu wa kusimamia maslahi yao Kikatiba.
19. Tume ya Utumishi
wa Jeshi la Polisi Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi
itakayokuwa na jukumu la kusimamia utumishi wa Jeshi la Polisi. Katika
uajiri wa askari wa Jeshi la Polisi, Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi
itazingatia kanuni na misingi ya utumishi iliyoainishwa katika Katiba
hii.
20. Misingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi Rasimu ya Warioba
ilipendekeza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi
la Jamhuri ya Muungano litazingatia:-
(a) viwango vya juu vya kitaaluma
na nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wake;
(b) ulinzi na ukuzaji wa haki
za binadamu;
(c) kanuni za uwazi na uwajibikaji; na
(d) kukuza mahusiano
na jamii. Warioba akaendelea kusema, Jeshi la Polisi, katika kutekeleza
majukumu yake, litashirikiana na vyombo vinavyohusika na kupambana na
uhalifu vya Nchi Washirika katika kufanya uchunguzi na kushughulikia
makosa ya rushwa na ufisadi.
Misingi hii yote imefutwa na Katiba
Inayopendekezwa.
Post a Comment