Umoja wa mataifa umewataka wanasiasa
na viongozi wa kidini Nchini Myanmar kulaani matamshi ya uchochezi na
chuki yaliyotolewa na kiongozi mmoja wa kibudha dhidi ya mjumbe maalum
wa umoja wa mataifa.
Kiongozi huyo wa kibudha Ashin Wirathu alimtusi mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa kumuita ''Kahaba'' na ''Mbwa''
Mkuu
wa kitengo cha haki za Binadamu katika Umoja huo, Zeid Ra'ad Al Hussein
alisema matamshi ya kiongozi huyo ni ya chuki na ya uchochezi.
Aliyetusiwa
ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kutoka nchini Korea Kusini,
Yanghee Lee, aliyekuwa nchini Myanmar wiki jana kuzungumzia hali
inayowakumba waisilamu ambao ni wachache nchini humo.
Wirathu alifungwa jela karibu miaka kumi kwa kuchochea ghasia dhidi ya waislamu.
Mtawa
huyo ni kiongozi wa vuguvugu la 969, ambalo linataka Myanmar kuwa nchi
ya Kibudha pekee yake na pia amekuwa akitoa wito wa waaisilamu kuwekewa
vikwazo pamoja na kudharauliwa.
Bwana Zeid aliyataja matamshi ya kiongozi huyo wa kibudha kama matusi makubwa na ya kibaguzi.
"Ningependa
kutoa wito kwa viongozi wa kidini na kisiasa nchini Myanmar kulaani
uchochezi wa aina yoyote na chuki,'' alisema bwana Zeid.
Tangu
utawala wa kijeshi kumalizika nchini Myanmar iliyokuwa inajulikana kama
Burma mnamo mwaka 2011 , watawa wamekuwa wakitaka dini ya kibudha kuwa
dini ya kitaifa na harakati hizo zimekuwa zikishika kasi kote nchini.
Mwaka
2012, mamia ya watu waliuawa na maelfu ya wengine kuachwa bila makao
baada ya ghasia kuzuka dhidi ya waumini wa kibudha na waisilamu katika
jimbo la Rakhine hasa kutoka kwa waisilamu wa Rohingya.
Post a Comment