Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Makao Makuu, Tunu Munthali akisoma taarifa ya utaratibu wa Uwezeshaji Kaya duni wilayani Kishapu, mkoa wa Shinyanga kwa washiriki wa warsha ya siku moja ya kuwajengea uelewa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya ya Kishapu.
Washiriki wa warsha hiyo katika picha ya pamoja kushoto na mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Makao Makuu, Tunu Munthali.

Mmoja wa wawezeshaji kutoka Timu ya Taifa ya uwezeshaji, Barnabas Mkumbo akiwasilisha mada mbele ya washiriki.

Mmoja wa washiriki akifuatilia mafunzo kwa umakini zaidi.

MPANGO wa miaka kumi wa kunusuru kaya maskini nchini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu umetajwa kuwa ni moja ya mipango mizuri iliyoandaliwa vizuri na serikali kwa lengo la kuwakomboa wananchi wake kutoka katika dimbwi la umaskini.

Hata hivyo baadhi ya madiwani wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wamewatahadharisha wanasiasa wenzao kutotumia vibaya mpango huo kwa lengo ya kujiimarisha kisiasa ili waweze kushinda katika chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wakichangia hoja katika warsha  ya kuwajengea uelewa kuhusu utekelezwaji wa mpango huo iliyofanyika mjini Mhunze wilayani Kishapu, baadhi ya madiwani walielezea wasiwasi wao kwamba pamoja na mpango mzima kuwa mzuri lakini ipo hatari ya baadhi ya wanasiasa kuutumia vibaya kwa lengo la kujinufaisha wenyewe.

“Mheshimiwa mwenyekiti binafsi naomba nitoe angalizo kwa wanasiasa wenzangu, hivi sasa tunaelekea kwenye chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, sasa tusiutumie mpango huu kutaka kujijenga zaidi kisiasa, maana iwapo tutaufanya kuwa ni wa kisiasa ipo hatari ya kuwaacha walengwa halisi kwa vile tu hawatuungi mkono,”

“Sasa tukifanya hivi tuelewe wazi mpango mzima hautakuwa na maslahi yoyote kwa walengwa na badala yake utageuka kuwa sehemu ya kampeni kwa lengo la mtu kutaka kuchaguliwa hivyo atahakikisha wanaonufaika ni wale tu wanaomuunga mkono au wanaotokana na chama chake cha siasa, hapana tuwe makini kwa hili,” alieleza Mbuke Mvanga diwani viti maalum.

Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa timu ya uhamasishaji Taifa kutoka TASAF makao makuu, Barnabas Mkumbo alisema pamoja na taratibu kuzuia wanasiasa kuingilia shughuli za kiutendaji, lakini wao kama wawakilishi wa wananchi katika maeneo yao wanapaswa kuhakikisha haki inatendeka.

“Mheshimiwa madiwani ni lazima wahakikishe kila mlengwa katika maeneo yao anafikiwa, tunachozuia ni kuingilia utendaji, kazi ya kuibua walengwa kazi hii inafanywa na mikutano mikuu ya vijiji, na tunashauri watu wa kwanza kufikiriwa wawe ni wale wanaoishi maeneo ya mbali ya kijiji, maana wengi hawa ni maskini,”

“Halmashauri ya kijiji, diwani au kiongozi ye yote kijijini hana mamlaka ya kuteua mtu, tunasema hivi kutokana na uzoefu mara nyingi kuonesha kwamba baadhi ya viongozi inapotokea fursa yoyote basi hukimbilia kuwapendelea watu wao wa karibuni, hatutaki hili litokee, mpango huu umelenga kunufaisha kaya duni na si vinginevyo,” alieleza Mkumbo.

Awali katika hotuba ya ufunguzi mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku iliyosomwa kwa niaba yake na katibu tawala wa wilaya, Octavian Mangosongo alisema, pamoja na nia nzuri ya serikali ya awamu ya nne kuanzisha mpango huo lakini unaweza usiwe na mafanikio iwapo viongozi na watendaji wote hawatausimamia kikamilifu.

“Ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa kwa ukamilifu, ushiriki wa wadau wote katika ngazi mbalimbali unahitajika sana, hivyo basi ni matarajio yangu mtakwenda katika maeneo yenu kueleza na kuitekeleza kikamilifu miongozo na taratibu mlizoelekezwa kwa kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu,” alieleza Nkhambaku.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa TASAF makao makuu, Tunu Munthali alisema mpango huo utatoa kwa walengwa ruzuku ya aina mbili ambazo ni ruzuku ya msingi na ruzuku inayotegemea kutimiza masharti ya elimu na afya.

Akifafanua Munthali alisema ruzuku ya msingi inatolewa kwa kaya iliyomo kwenye mpango kiasi cha shilingi 10,000 kwa mwezi na kama kuna mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 itaongezwa kiasi cha shilingi 4,000 bila kujali mtoto anasoma au hasomi.

“Kwa ruzuku inayotegemea kutimiza masharti ya elimu na afya mtoto chini ya miaka mitano atapewa shilingi 4,000 iwapo atahudhuria kliniki kila mwezi, wanaosoma shule ya msingi shilingi 2,000 (watoto wanne), kidato cha kwanza hadi cha nne, shilingi 4,000 (watoto watatu)  na kidato cha tano na sita shilingi 6,000 kwa watoto wawili kila mwezi,” alieleza Munthali.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top