Diwani Kata ya Mwabuzo Meatu Simiyu, Seni Challya akielezea hofu yake kuhusiana na utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF III. |
Mmoja wa waratibu kutoka Makao Makuu ya TASAF Oscar Maduhu akitoa mada kwa washiriki wa warsha ya siku moja wilayani Meatu, mkoa wa Simiyu |
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Meatu mkoani Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa kutoka TASAF makao makuu - Dar es Salaam. |
Mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa TASAF nchini, Jenga Nyamuko akifafanua baadhi ya hoja zilizotolewa na washiriki wa warsha ya siku moja juu ya kujengewa uelewa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini. |
MPANGO wa Kunusuru Kaya Maskini nchini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu huenda usiwe na matokeo mazuri baada ya baadhi ya wananchi kueneza uvumi wakidai fedha zinazotolewa na mfuko huo kwa kaya maskini zinatokana na mtandao wa Freemasons.
Hali hiyo imebainishwa na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wakati wa warsha ya siku moja ya kuwajengea uelewa kuhusiana na Mpango wa kunusuru kaya maskini iliyofanyika mjini Mwanhuzi ikiwashirikisha viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali ngazi ya wilaya, tarafa na kata.
Wakichangia mada iliyohusu uhawilishaji fedha na utaratibu wa kutuma fedha kwa kaya maskini na zinazoishi katika mazingira hatarishi madiwani hao walielezea changamoto kadhaa zinazoweza kuchangia kukwamisha lengo lililokusudiwa la kuzinusuru kaya hizo maskini wakitoa mfano wa dhana potofu inayoenezwa na baadhi ya watu wakidai fedha hizo ni za Freemasons.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mpango huu ni mpango mzuri maana umelenga kuwasaidia wananchi wetu ambao ni maskini, lakini hata hivyo kuna changamoto kadhaa ambazo zisipotatuliwa mapema zitachangia kutofanikiwa kwa mpango mzima, kwanza kuna suala la wakuu wa kaya ambao iwapo watakabidhiwa fedha hizo wataishia kwenye vilabu vya pombe,”
“Changamoto nyingine ni baadhi ya watu kusambaza uvumi wakidai fedha zinazotolewa na TASAF zinatokana na mtandao wa Freemasons, sasa kama unavyofahamu wananchi wetu wengi elimu yao ni ndogo, ni wazi watakataa kuzipokea, ni muhimu wakapewa elimu ya kutosha kabla ya kuanza utekelezwaji wa mpango huu,” alieleza diwani Seni Challya.
Diwani huyo wa kata ya Mwabuzo alishauri mbali ya kutolewa elimu ya kutosha kwa walengwa lakini pia ni vizuri baada ya kutambulika kwa kaya maskini na zinazoishi katika mazingira magumu fedha hizo wakabidhiwe wanawake katika kaya badala ya wanaume ili kuepuka ubadhirifu au kutumika kwa malengo mengine ikiwemo ulevi.
Akijibu hoja kuhusiana na uvumi wa fedha hizo kuhusishwa na mtandao wa Freemasons, mmoja wa waratibu wa kutoka TASAF Makao Makuu, Oscar Maduhu alikanusha uvumi huo ambapo alisema ni fedha hizo ni za watanzania ikiwemo msaada wa Benki ya Dunia (WB) na wadau wengine ikiwa lengo kuu ni kunusuru kaya maskini na zinazoishi katika mazingira magumu.
“Uvumi huu umelenga kutaka kuwapotosha na kuwatia hofu watu, serikali ya Tanzania haina uhusiano wowote na mtandao huu wa Freemasons, fedha hizi ni zetu wenyewe na nyingine tunasaidiwa na Benki ya dunia wakiwemo wadau wengine wa maendeleo, waheshimiwa madiwani na watendaji wote naomba tusaidiane kuwaelimisha wananchi,” alieleza Maduhu.
Aidha Maduhu alifafanua kuwa Mpango wa kunusuru kaya maskini na zinazoishi katika mazingira magumu ulibuniwa na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuzisaidia kaya hizo ziweze kuwa na maisha bora na kuboresha uchumi wao na kwamba kuna umuhimu wa viongozi kuhakikisha walengwa wote wananufaika.
Awali katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha, mkuu wa wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini iliyosomwa kwa niaba yake na katibu tawala wa wilaya hiyo, Chele Ndaki aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuzingatia yale yote watakayofundishwa ili kuwezesha kufanikiwa kwa lengo lililokusudiwa na serikali na kusisitiza suala la uwazi na ukweli katika utekelezaji wake.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji TASAF Makao Makuu, Jenga Nyamuko alisema Mpango wa kunusuru kaya maskini umelenga kufikia wastani wa kaya milioni moja nchini zinazoishi katika hali duni ya umaskini zitakazopewa ruzuku za aina tatu ikiwemo kutoa ajira za muda kwenye kaya zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi.
“Mpango utawezesha kaya maskini zinazoishi katika mazingira hatarishi, hususan watoto na wajawazito kupata lishe bora, huduma za afya na elimu ambapo walengwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaohudhuria kliniki na wanafunzi wanaosoma shule za awali, msingi na sekondari,” alieleza Nyamuko
Post a Comment