MAUAJI yanayotokana na imani potofu za kishirikina
yameendelea kuukumba mkoa wa Shinyanga baada ya kikongwe mwenye umri wa miaka
80 na binti yake kuuawa kikatili kwa kukatwa katwa mapanga hadi na kisha
kuchinjwa na kusababisha vifo vyao wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya
kishirikina.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha
aliwataja waliouawa kuwa ni Dilu Tungu (80) na mwanae Bunya Mihangwa (45) wakazi
wa kijiji cha Ihugi wilayani Shinyanga na kwamba mauaji hayo yalitokea tarehe 15.10.2014 saa
2.00 usiku.
Akifafanua Kamanda Kamugisha alisema siku hiyo ya tukio
watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa Tungu walipokuwa wakiandaa chakula
cha jioni na wanafamilia wengine ambapo walishambuliwa kwa kukatwa katwa
mapanga sehemu mbalimbali za miili yao na kisha walichinjwa mithili ya kuku hadi
kufa.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauaji
hayo ni imani za kishirikina baada ya Bwanya Mlyashimba (40) mkazi wa kijiji
hicho kuwatuhumu marehemu hao kwamba walimroga na kusababisha akose nguvu za
kiume na pia walimroga mama yake (Bwanya) aitwaye Hollo Mahangwa aliyefariki
mnamo mwaka 2013.
“Tunamshikilia huyu mtuhumiwa Bwanya kwa mahojiano zaidi kuhusiana
tukio hili na pia tunaendelea kuwasaka watu wengine waliohusika na mauaji haya,
tunawaomba wananchi watusaidie kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa
watuhumiwa wote,” alisema Kamugisha.
Tukio la pili limetokea pia tarehe 15.10.2014 saa 11 jioni huko kata ya
Kilago Kahama mkazi mmoja wa kijiji cha Chibiso wilayani Kahama mkoa wa
Shinyanga anayekisiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35 alikufa baada ya
kushambuliwa na wananchi wenye hasira na kisha mwili wake kuuchoma moto baada
ya kumtuhumu kwa wizi wa ng’ombe wawili ambao hata hata hivyo mmiliki wake hakufahamika mara moja.
Hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na mauaji hayo ambapo
Kamanda Kamugisha amerejea wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia
sheria mkononi pale wanapowakamata watuhumiwa na kwamba badala ya kuwaua ni
vizuri wanapowakamata wakawakabidhi mikononi mwa vyombo vya dola.
Katika tukio lingine mfanyakazi wa Manispaa ya Shinyanga
aliyetajwa kwa jina la Frola Kakiziba (47) amekufa wakati akipatiwa matibabu
katika hospitali ya serikali mkoani Shinyanga baada ya kugongwa na pikipiki iliyokuwa
ikiendeshwa na Ofisa ardhi alipokuwa amebebwa katika pikipiki nyingine maarufu
kama ‘bodaboda’ akielekea kazini.
Kamanda Kamugisha alisema ajali hiyo ilitokea jumatatu asubuhi ya tarehe 15.10.2014 saa
1.15 asubuhi eneo la Ushirika katika barabara ya Shinyanga kuelekea Mwanza
ambapo pikipiki yenye namba za usajili T.317 BWV aina ya SUNLG mali ya Khamis
Nkelege mkazi wa manispaa ya Shinyanga ilipoigonga pikipiki nyingine iliyokuwa
imembeba Kakiziba.
Jeshi la Polisi linamsaka dreva wa bodaboda aliyekuwa amembeba
Kakiziba ambaye alitoroka baada ya kutokea kwa ajali hiyo na kwamba chanzo cha
ajali hiyo ni uzembe wa madereva wa pikipiki zote mbili ambapo wito umetolewa
kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani wanapoendesha vyombo vya
moto.
Post a Comment