Mzee Titus Ihema mkazi wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga akizungumza na mwandishi wa habari kupongeza uamuzi wa waziri |Mkuu Mizengo Pinda kusisitiza suala la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kujengwa katika kata ya Busangi.

BAADHI ya wazee waasisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamempongez waziri mkuu Mizengo Pinda kwa hatua yake ya kusisitiza ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kujengwa katika kata ya Busangi.

Mbali ya kumpongeza waziri mkuu, pia wazee hao wameiomba kamati ya Siasa ya CCM mkoani Shinyanga kutengua mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya siasa ya wilaya ya Kahama wakipendekeza kuahirishwa kwa suala la ujenzi wa makao makuu mpaka baada ya uchaguzi mkuu mwakani kwa vile hatua hiyo itakuwa na madhara makubwa kwa chama.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kahama wazee hao walielezea hatua yao kuunga mkono kauli ya waziri mkuu na kwamba uamuzi wa makao makuu ya halmashauri ya Msalala kujengwa Busangi umezingatia jiografia ya halmashauri na kata hiyo ipo katikati.

Mmoja wa wazee hao, Titus Ihema alisema ni ajabu kuona baadhi ya watendaji na viongozi wa chama wakiwemo madiwani kupinga agizo la waziri mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa serikali ambapo alisisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa agizo lake kwa lengo la kusukuma haraka maendeleo ya wananchi wa Msalala.

“Binafsi sisi wazee hatufurahishwi kabisa na kitendo hiki cha watu kuendelea kupingana na maamuzi halali yaliyotolewa mapema na madiwani  wetu katika vikao vyao halali   ambapo baada ya kupatikana kwa halmashauri ya Msalala walikubaliana makao makuu ya halmashauri yajengwe Busangi, leo iweje watake kubadili maamuzi haya?”

“Busangi kijiografia ipo katikati na tayari ina huduma zote muhimu za kijamii kama vile kituo cha afya, mahakama, polisi na barabara inayopitika kipindi chote cha mwaka, hivyo ni rahisi kwa watu kupata huduma zote muhimu wanazozihitaji bila ya kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Segese ambako ni pembezoni mwa halmashauri,” alielezea Ihema.

Alisema kitendo cha kutaka kutengua maazimio halali ya awali juu ya ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kinaweza kusababisha kwa kiasi kikubwa kuchelewa kwa maendeleo ya wakazi wa Msalala na hivyo hata lengo la serikali la utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya mpango wa Matokeo makubwa sasa (BRN) litaweza kukwama.

“Sisi waasisi wa Chama cha Mapinduzi tuna kila sababu za kupongeza tamko la waziri mkuu wetu alilolitoa hivi karibuni kuhusiana na suala zima la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri ya Msalala kujengwa Busangi, huu ni uamuzi wa busara, maana hapo ni katikati itakuwa ni rahisi kwa wananchi kwenda kufuata huduma mbalimbali,”

“Tunachowaomba wenzetu watendaji ndani ya serikali wahakikishe wanaheshimu agizo la waziri mkuu ambalo limezingatia maamuzi ya awali ya madiwani wetu, na hivyo waanze utekelezaji wa ujenzi wa makao makuu pale Busangi, mbali ya kuwa katikati, lakini pia pana huduma zote muhimu za kijamii, ikiwemo kituo cha polisi, hospitali na mahakama,” alieleza Ihema.

Naye Sallu Maganga mkazi wa Busangi alilaani vikali shinikizo la baadhi watendaji wa serikali na madiwani wanaotaka kutengua maamuzi ya awali na kueleza huenda nyuma yao kuna mikono ya rushwa kwa lengo la kutaka kuwasaidia wafanyabiashara wa Segese wakiamini iwapo makao makuu yatajengwa katika kata yao basi biashara zao zitashamiri zaidi.

“Ujenzi wa makao makuu katika kata ya Busangi umezingatia zaidi sera ya serikali ya CCM ya kusogeza huduma za kijamii karibu zaidi na wananchi, sasa hawa watendaji wa serikali na baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM wilayani Kahama wanaopinga makao makuu kuwa Busangi kwa kweli hatuwaelewi,”

“Waziri mkuu ndiye mtendaji mkuu wa serikali, itakuwa ni ajabu mtu wa chini apingane naye, binafsi nahisi uwepo wa mianya ya rushwa kwa baadhi ya wenzetu hawa, sisi wazee tunasisitiza wamuheshimu kiongozi huyu, na tuiombe serikali iwashughulikie wale wote watakaoonekana dhahiri wanataka kupinga maamuzi yake,” alieleza Sallu Maganga mkazi wa kata ya Chela.

Hivi karibuni madiwani wa halmashauri ya Msalala wakiwemo baadhi ya watendaji wa serikali wamejikuta katika mvutano kuhusiana na suala la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo ambapo pamoja na baraza la madiwani awali kuridhia ujenzi huo ufanyike kata ya Busangi diwani mmoja aliwasilisha hoja binafsi katika baraza akiomba kutengua uamuzi huo wa awali.

Hoja hiyo binafsi iliyokubaliwa na baadhi ya madiwani wakiwemo wataalamu w halmashauri hiyo ilipingwa vikali ikidaiwa iliwasilishwa kinyume cha utaratibu za uwasilishaji wake hali iliyomlazimu waziri mkuu Pinda kutoa agizo la kuheshimiwa kwa maamuzi ya awali ya ujenzi huo kufanyika katika kata ya Busang
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top