IMEELEZWA kuwa kuna
uwezekano mkubwa kwa Tanzania kujikuta haina wataalam wa kutosha katika
nyanja mbalimbali kutokana na kitendo cha serikali kupuuza suala la elimu na
badala yake kuelekeza zaidi nguvu zake katika masuala yanayohusiana na mambo ya
kisiasa.
Hali hiyo imebainishwa na baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaoendelea na mafunzo yao ya vitendo katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga ambapo walisema kitendo cha serikali kushindwa kuwalipa fedha zao wanazopaswa kulipwa wakiwa mafunzoni kinaonesha wazi jinsi gani isivyothamini suala la elimu.
Wanafunzi hao walidai kwamba kitendo cha serikali kuwapuuza wasomi walioko masomoni hivi sasa kinachangia kwa kiasi kikubwa wengi wao washindwe kufuatilia vizuri masomo yao kiasi cha kukata tamaa ya maisha hali ambayo ni hatari kwa mstakabali wa taifa.
Mmoja wa wanafunzi hao, Gabriel Dogani, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) jijini Dar es Salaam alielezea kushangazwa kwake na jinsi serikali inavyotoa kipaumbele katika suala zima la kuwalipa malipo mbalimbali wanasiasa huku wanafunzi wa vyuo wakihangaika kwa kutokuwa na fedha.
“Hivi sasa kuna malalamiko ya wanafunzi wa vyuo vikuu walioko katika mafunzo ya vitendo kutokulipwa fedha zao kama utaratibu unavyoelekeza, wengi wanaishi kwa shida, baadhi wamegeuka ombaomba, serikali imeziba masikio haitaki kuwalipa fedha walizoahidiwa kulipwa wanapokuwa mafunzoni,”
“Kwa hali hii baadhi yetu wameacha kuendelea na mafunzo haya ya vitendo, sasa unafikiri huo uzoefu wataupataje? ni jambo la kusikitisha kuona serikali inatoa kipaumbele kwa wanasiasa, bunge maalumu la katiba linaloendelea hivi sasa linatafuna mamilioni ya shilingi, lakini serikali imeshindwa kutulipa sisi kiasi cha shilingi bilioni 6.6 tu,” alieleza Dogani.
Kwa upande wao wanafunzi Kasanzu Luganga na Josephin Mboya wanaondelea na mafunzo ya vitendo katika ofisi za Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) mkoani Shinyanga walisema kitendo cha serikali kuwazuia kuandamana ili kufikisha kilio chao kinaonesha jinsi gani elimu isivyothaminiwa katika nchi hii.
“Binafsi sielewi kama kweli watanzania tutakuwa na fursa za kushiriki katika ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni wazi tutashindwa kukidhi vigezo tutakapowania fursa za ajira tutakaposhindana na wenzetu wa mataifa mengine kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha elimu, ni vizuri serikali sasa ikaliona hili,” alieleza Luganga.
Wanafunzi hao walisema ipo hatari ya mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) katika sekta ya elimu kutofanikiwa iwapo serikali haitabadili msimamo wake katika kuwahudumia wanafunzi mbalimbali wa vyuo ikiwemo kuondoa urasimu katika utoaji wa mikopo na uboreshaji wa sekta hiyo kwa kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana kuanzia ngazi ya msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
Post a Comment