Uegeshaji na uingizaji wa magari makubwa katikati ya mji ni moja ya kero inayowakera wakazi wa manispaa ya Shinyanga.

Baadhi ya wakazi wakishangaa jinsi magari yalivyobanana kutokana na uegeshaji wa pande zote mbili za barabara huku sheria za manispaa zikizuia uegeshaji huo.

BAADHI ya wakazi wa manispaa ya Shinyanga wamelalamikia kitendo cha uongozi wa manispaa hiyo kushindwa kusimamia kikamilifu sheria zake ndogo hali ambayo inachangia watu kufanya shughuli zao bila kujali na kuchangia ongezeko la uchafu na msongamano katika baadhi ya mitaa.




Wakazi hao wanasema pamoja na manispaa ya Shinyanga kuwa na sheria zake ndogo zilizotungwa kwa ajili ya kuuweka mji katika hali ya usafi lakini sheria hizo hazifanyi kazi na kusababisha baadhi ya watu kujiendeshea shughuli zao kienyeji katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Walisema watendaji wa manispaa wanaopaswa kusimamia masuala ya usafi wamekuwa hawatimizi wajibu wao hali ambayo inatia hofu na kuashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa kwa vile baadhi ya shughuli zinazofanyika katika maeneo yasiyoruhusiwa hufanyika mbele ya macho yao na hakuna hatua zozote wanazochukua.

Wakitoa mfano wa shughuli hizo ni pamoja na uendeshaji wa gereji bubu za pikipiki na magari katika maeneo ya makazi, wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi kupanga bidhaa zao nje katika maeneo yasiyoruhusiwa ikiwemo yale ya watembea kwa miguu na magari makubwa kuingia katika ya mji ambayo yamekuwa yakisababisha msongamano mkubwa.

“Kwa kweli tunashangazwa na viongozi wetu wa manispaa kufumbia macho tabia hii ya ukiukwaji wa sheria zilizotungwa na manispaa, inaonesha zipo tu katika maandishi maana hatuoni hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaozivunja, kiuhalisia manispaa yetu hivi sasa haina hadhi ya kuitwa manispaa,”

“Hivi sasa wafanyabiashara wote wa vifaa vya ujenzi wanapanga ovyo bidhaa zao nje ya maduka yao mpaka katika maeneo ya wapitanjia, sheria za manispaa zinakataza upangaji huo, lakini hatuoni wenzetu wakichukua hatua zozote, sheria inazuia magari makubwa kuingia katikati ya mji, lakini bado yanaingia, tunashangaa!!” alieleza mmoja wa wakazi hao.

Hata hivyo mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga, Festo Kang’ombe mara kwa mara amekuwa akidai ofisi yake inashindwa kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaovunja sheria za manispaa hiyo kutokana na baadhi ya wanasiasa kuingilia kati.

Mbali ya kukiri ukiukwaji wa baadhi ya sheria za manispaa, Kang’ombe alidai mara nyingi wanasiasa hasa madiwani wamekuwa wakiingilia kati pale ofisi yake inapotaka kuchukua hatua za kisheria wakidai kitendo hicho ni kuwabughudhi wananchi.

Kwa upande wake Naibu Meya wa manispaa hiyo, David Nkulila alikiri kuwepo kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria ndogo zinazotungwa na manispaa ambapo alidai zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya watendaji kushindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu.

“Ni kweli yapo mambo mengi hivi sasa hayaendi sawa, kama suala hili la msongamano wa magari makubwa katikati ya mji hata mimi halinifurahishi, nafikiri tutawahimiza watendaji wetu waliwekee mkazo, itakuwa haina maana yoyote kutunga sheria ndogo halafu hazifanyi kazi, lazima tuchukue hatua sasa,” alieleza Nkulila.



Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top