Nyaitabano akipongezwa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama CHADEMA Taifa, Wilfred Lwakatare baada ya kujiunga rasmi na CHADEMA. |
Aliyekuwa kada wa CCM, Damary Nyaitabano akitangaza rasmi kuhama CCM na kujiunga na CHADEMA, kushoto ni mwenyekiti wa CHADEMA Shinyanga mjini, Hassan Baruti. |
Akitangaza rasmi kujitoa CCM katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA alisema uamuzi wake huo wa kujitoa CCM na kujiuzulu wadhifa aliokuwa nao wa uenyekiti wa mtaa, unatokana na kutokubaliana na msimamo wa CCM wa kukataa kuheshimu maoni ya watanzania waliyoyatoa mbele ya Tume ya Jaji Joseph Warioba kuhusu katiba mpya.
Mbali ya madai ya viongozi wa CCM kugoma kuheshimu maoni ya wananchi na kutojadili rasimu iliyoandaliwa kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba lakini pia chama hicho hakijatekeleza ahadi mbalimbali ilizozitoa wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 na hivyo watanzania kukipa ridhaa ya kuunda serikali.
“Nimeamua kwa hiari yangu mwenyewe, sijanunuliwa na mtu maana baada ya kukaa na kutafakari nimebaini wazi CCM haina dhamira ya kweli ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wake na ndiyo maana hivi sasa kinapinga rasimu ya Jaji Warioba isijadiliwe bungeni ambayo ndiyo yenye maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,”
“Kwa hali hiyo natangaza rasmi kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na ninajiunga na CHADEMA, naomba nikabidhi kadi yangu ya zamani ya CCM kwa uongozi wa CHADEMA, nimeamua kuachana kabisa na chama hiki pamoja na kwamba nilikuwa ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa kwa tiketi ya CCM,” alieleza Nyaitabano.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA Shinyanga mjini, Hassan Baruti alimpongeza Nyaitabano kwa ujasiri aliounesha bila kujali maslahi aliyokuwa akiyapata ndani ya CCM na kwamba kitendo hicho kinastahili kuigwa na watu wengine waliomo ndani ya CCM wenye kujali maslahi ya watanzania.
Akimkabidhi rasmi kadi ya CHADEMA, Baruti alisema kila mtanzania mwenye uchungu wa taifa lake anastahili kulipigania taifa lake kwa kuhakikisha nchi inapata watawala wapya watakaojali maslahi ya watanzania wote tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo CCM daima kimekuwa kikipigania maslahi yake binafsi.
Katika hatua nyingine mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA Taifa, Wilfred Lwakatare akiwahutubia wakazi wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya mahakama ya mwanzo juzi, alikipongeza kitendo cha serikali ya CCM kumtupa gerezani na kudai kimemuongezea umaarufu.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Lwakatare alisema kitendo cha serikali ya CCM kumtungia tuhuma za uongo za ugaidi kimesababisha kuongezeka kwa umaarufu wake na kwamba alipokuwa ndani ya gereza la Segerea alijifunza mambo mengi juu ya uonevu unaofanywa na serikali hiyo ya CCM.
“Naishukuru sana serikali ya CCM kwa kunitungia tuhuma feki za ugaidi, zimeongeza sifa yangu (CV) na hivi sasa naitwa Gaidi Feki, nilikaa Segerea nikakutana na majembe mengine humo ndani, nimejifunza mengi, lakini kitendo hicho hakitanizuia wala kupunguza kasi katika mapambano kuelekea kwenye ukombozi wa kweli,” alieleza Lwakatare.
Post a Comment