Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari wakati wa kujadili changamoto wanazokutana nazo wanapofuatilia matukio ya ukatili wa kijinsia katika mikoa yao. |
Mmoja wa kikongwe aliyelazimika kukimbia makazi yake baada ya kutuhumiwa kuwa ni mchawi akihojiwa na mwandishi wa habari ambapo hata hivyo hakuwa na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha juu ya maswahibu yaliyomsibu.
UMOJA wa vilabu vya waandishi wa
habari nchini (UTPC) unakusudia kuanzisha ushirikiano wa karibu na Chama cha
wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA) kwa lengo la kuongeza nguvu katika
mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hapa nchini.
Hali hiyo imebainishwa jijini Mwanza na mkurugenzi mtendaji wa UTPC,
Abubakar Karsan alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu kwa waandishi wa
habari kutoka mikoa mitano ya kanda ya ziwa iliyoandaliwa na TAMWA kwa ufadhili
ya Shirika la Idadi ya watu la Umoja wa mataifa (UNFPA).
Karsan alisema uongozi wa UTPC
kwa kipindi kirefu ulikuwa ukitafuta utaratibu wa jinsi ya kuwa na ushirikiano
na TAMWA kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na hatimaye ndoto yao hivi sasa
imefanikiwa baada ya kuwepo kwa mipango ya kuanzishwa kwa mahusiano kati ya
taasisi hizo mbili.
Alisema kitendo cha kuanzishwa
kwa ushirikiano huo kitasaidia kwa kiasi kikubwa kwa waandishi wa habari
kupitia kalamu zao kuweza kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia
vinavyotendeka hapa nchini ambapo pia mipango imo mbioni kuundwa kwa mtandao wa
waandishi wa habari watakaojikita zaidi katika kuandika habari za ukatili wa
kijinsia.
“Ndugu mkurugenzi kuja kwako UTPC
kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya asasi zetu mbili ambazo zina
mchango muhimu sana
kwa maendeleo ya taaluma ya uandishi wa habari hapa nchini kwa upande mmoja na
maendeleo ya nchi kwa upande wa pili,”
“UTPC tunaahidi kutoa ushirikiano
madhubuti kwa TAMWA ili malengo yetu yaweze kufanikiwa, hasa katika suala zima
la kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia vinavyoendelea
kutokea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” alieleza Karsan.
Akifafanua mkurugenzi huyo
alisema vyombo vya habari vina dhima kubwa katika kupiga vita vitendo vya
ukatili wa kijinsia ambavyo kama vitaachwa
viendelee kutendeka vinaweza kuvunja mshikamano wa kijamii na hatima yake ni
mparaganyiko wa taifa.
“Athari za ukatili wa kijinsia
zinaweza kuwa za kimwili, kisaikolojia au za kiuchumi jamii, pamoja na ukweli
kwamba athari hizi huwapata wanawake, wanaume na watoto lakini jinsi
inayoathirika kwa kiasi kikubwa ni wanawake, na hii inatokana na fikra kengeufu
inayojengwa kwamba mwanamke ni kiumbe dhaifu anayestahili kusaidiwa,” alieleza
Karsan.
Kwa upande wake mkurugenzi
mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka aliwapongeza waandishi wa habari nchini kwa
juhudi zao wanazozionesha katika kuandika habari zinazohusiana na vitendo vya
ukatili wakielezea madhara wanayopata watu wanaotendewa vitendo hivyo kiasi cha
jamii kuanza kuanza kubadilika.
“TAMWA mara kwa mara tumekuwa
tukitoa mafunzo kwa waandishi wa habari hapa nchini kwa ajili ya kuwajengea
uwezo wa jinsi ya kuandika kwa ufasaha habari zinazohusiana na vitendo vya
ukatili wa kijinsia vinavyofanyika miongoni mwa jamii,”
“Tunaamini tutakapowajengea uwezo
wana habari na wao kupitia kalamu zao wataweza kuifikisha elimu hii kwa sehemu
kubwa ya jamii, watu wengi wataelewa ubaya wa kumfanyia mtu mwingine ukatili wa
aina yoyote ile na hivyo kuachana na vitendo hivyo, mpaka sasa kuna mafanikio
ambayo yameanza kuonekana kutokana na kazi za waandishi,” alieleza Msoka.
Alisema mafanikio ya TAMWA pia
yamechangiwa na mchango mkubwa wanaoupata kutoka kwa makundi mbalimbali ya
wanaharakati yanayojishughulisha kupiga vita ukatili wa kijinsia ikiwemo asasi
za kiraia kama vile Mtandao wa Jinsia (TGNP),
Kituo cha Sheria na haki za binadamu (LHRC), na Chama cha wanasheria wanawake
(TAWLA).
Pia TAMWA hushirikiana na mashirika
mbalimbali ya kimataifa yanayopigania haki za binadamu na kupinga vitendo vya
ukatili wa kijinsia ambapo Shirika la Idadi ya watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA)
kwa hivi sasa ndilo linalofadhili mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya
harakati dhidi ya Ukatili wa kijinsia nchini.
Msoka anasema, “….Waandishi wa
habari wana wajibu mkubwa wa kuleta mabadiliko ya kijamii kutokana na kazi
kubwa waliyonayo katika kujenga na kubadilisha mwelekeo wa watu ambapo
wakielimishwa kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia wataihamasisha jamii juu ya
aina zote za ukatili huo na hivyo kuondoa mfumo wa ubaguzi wa kijinsia na
kuwepo mahusiano mazuri yasiyo ya kikatili.”
Kwa upande wao waandishi hao wa
habari waliweza kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika mikoa yao ambapo kwa sehemu
kubwa changamoto hizo zilikuwa zikifanana ikiwemo tatizo la jamii kwa sehemu kubwa
kuogopa kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika familia
zao kwa kuchelea aibu au kuchekwa na jamii.
Baadhi ya changamoto nyingine
zilizobainishwa ni uwezo mdogo wa kifedha kwa ajili ya kusafiria kwenda maeneo
ya vijijini ambako vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiendelea
kutokea na jamii kwa sehemu kubwa ikiwa bado inaendelea kuheshimu mila na
desturi zilizopitwa na wakati ambazo kwa sehemu kubwa zinawakandamiza wanawake
na watoto.
Kundi la waandishi kutoka mkoani
Shinyanga lilitaja pia tatizo la baadhi ya watendaji katika madawati ya jinsi
yaliyopo katika vituo vya polisi kukataa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa
habari kwa visingizio kwamba bado wanafuatilia chanzo cha tukio husika.
Changamoto nyingine iliyobainishwa na waandishi kutoka mkoa wa Shinyanga na Kagera na tatizo la kushindwa kujieleza kwa ufasaha kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo suala la mawasiliano ya lugha za asili ambazo waandishi hushindwa kuzielewa. Hata hivyo walishauriwa kutafuta wakalimali pale linapojitokeza tatizo la lugha.
Kwa upande wao wawakilishi wa
mkoa wa Kagera pamoja na changamoto nyingi walizoziainisha walisema tatizo la
umbali wa maeneo ambako hutokea vitendo vya ukatili linachangia waandishi
kushindwa kufika maeneo hayo kutokana na kutokuwa na usafiri ambapo walitoa
mfano wa maeneo ya visiwa vilivyomo ndani ya ziwa Victoria .
Hata hivyo waandishi hao
walijadili na kupendekeza njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto
zilizojitokeza ikiwemo suala la kutolewa elimu ya kutosha kwa jamii ili iweze
kuachana na tabia ya kuficha au kuwaficha watu wanaotendewa vitendo vya
kikatili na badala yake washirikiane na wadau wa kupiga vita vitendo hivyo kwa
kuwafichua watuhumiwa wote ili sheria ichukue mkondo wake.
Waandishi hao walikubaliana
pamoja na changamoto zinazowakabili kutumia fursa walizonazo kwa kuandika
habari na makala mbalimbali zitakazoielimisha jamii iweze kushiriki kikamilifu
katika kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo
yao na hivyo kuweza kupunguza kama
siyo kukomesha kabisa vitendo hivyo.
Akichangia katika mbinu zilizobainishwa na waandishi ya jinsi ya kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo katika kufuatilia na kuandika habari juu ya ukatili wa kijinsia, mkurugenzi wa TAMWA aliwashauri wajenge utamaduni wa kushirikiana kati ya waandishi wa mkoa mmoja na mkoa mwingine kwa kupeana taarifa juu ya vitendo vilivyotokea ili waweze kushirikiana kufuatilia.
Lakini pia alisema pale waandishi wanapopata fursa ya kuhudhuria katika mikutano mbalimbali ya kijamii basi wajenge tabia ya kuomba nafasi ili waweze kutoa ujumbe mfupi juu ya ubaya wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na jinsi ya kuvipiga vita ili jamii iliyohudhuria katika mikutano iweze kupata elimu na hivyo kuondoa woga na waweze kuwafichua watuhumiwa wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Post a Comment