Mmoja wa kikongwe wilayani Kahama ambaye alilazimika kukimbia makazi yake kutokana na hofu ya kuuawa akihojiwa na mwandishi wa habari mjini Kahama.

Mauaji ya Kikatili yameendelea kuitikisa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga baada ya mkazi mwingine katika kitongoji cha  Muhida kata ya Busangi aliyetajwa kwa jina la Milembe Masanja (50) kuuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na ugomvi wa kugombea mipaka ya mashamba.


Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga lilitoa takwimu za mauaji yanayotokea katika mkoa mzima ambapo wilaya ya Kahama iliongoza ambapo hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana kuliripotiwa  matukio 45 kati yake 25 yakitokana na imani za kishirikina na 20 yalisababishwa na wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema mauaji hayo yalitokea Julai 14, mwaka huu saa 2.00 usiku baada ya watu wawili waliotambuliwa kwa majina ya Chuchu Lugodisha na Ngeja Lugodisha wote wakazi wa kijiji cha Lunguya mkoani Tabora kuvamia nyumbani kwa Milembe na kumshambulia kwa kumkatakata mapanga hadi kufa.

Kamanda Kamugisha alisema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa kugombea mipaka ya shamba kati ya familia ya Madaha Luhemeja na familia ya marehemu Milembe ambapo inadaiwa familia ya Madaha iliamua kukodisha watu wa kufanya mauaji hayo.

“Mauaji haya yanatokana na ugomvi wa mashamba, watu waliofanya mauaji haya inasemekana walikodiwa na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Madaha Luhemeja mkazi wa kitongoji cha Muhida ambao walivamia nyumbani kwa Milembe na kumkatakata mapanga sehemu za kichwani na mikono yote miwili na kusababisha kifo chake papo hapo,”

“Mara baada ya kuhakikisha Milembe amekufa walitoroka pamoja na Madaha na hivi sasa tunaendesha msako wa kuwasaka popote walipo ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji, na tunatoa wito kwa raia wema watoe taarifa katika kituo chochote cha polisi pale watakapowaona watuhumiwa hao,” alieleza Kamugisha.

Hata hivyo alisema mpaka hivi sasa watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na mauaji hayo waliotajwa kuwa ni Pili Paulo (37), Juma Paulo (19) na Daudi Ngassa (57) wote wakazi wa kata ya Busangi wilayani Kahama.

Kamanda Kamugisha ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga kuimarisha ulinzi katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanafuatilia nyendo za kila mgeni anayefika katika maeneo yao na ye yote watakayemtilia shaka wasisite wa kuogopa kutoa taarifa mara moja katika kituo chochote cha polisi au ofisi za serikali.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top