Mkurugenzi mtendaji wa UTPC, Abubakar Karsan akifungua warsha ya siku tatu kuhusu harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia. |
Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka akitoa mada kwa waandishi wa habari. |
Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara, Kagera na Mwanza wakifuatilia mafunzo kutoka kwa mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka |
VITENDO vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia nchini vinaweza kukomeshwa iwapo serikali kwa upande wake itaamua kushirikiana kikamilifu na jamii katika kupiga vita vitendo hivyo.
Hali hiyo imebainishwa na Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu mjini Mwanza kuhusu harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na TAMWA kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Kagera, Mara na Shinyanga.
Karsan alisema pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na vikundi vya wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo Chaama cha wanahabari wanawake (TAMWA) lakini bado serikali kwa upande wake haijachukua hatua madhubuti za kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.
Alisema kibaya zaidi hata serikali yenyewe kupitia sera, matamko yake ya kimkakati na hata baadhi ya sheria zilizopo hapa nchini zinaendeleza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake ambapo alitoa mfano wa kutengwa kwa viti maalumu vya udiwani, ubunge na nafasi za uteuzi.
“Kwa bahati mbaya hata serikali yetu kupitia sera, matamko ya kimkakati au baadhi ya sheria zake hutenda ukatili wa kijinsia. Mfano mzuri ni huu utaratibu wa kuwatengea wanawake viti maalumu, nafasi hizi ukiangalia kiundani zinajenga dhana kwamba wanawake ni dhaifu,”
“Huu nao ni ukatili wa kijinsia, maana inaonesha wanawake hawana uwezo wa kugombea majimbo sambamba na wanaume, hivyo inaonekana ni vizuri wakapewa upendeleo maalumu, serikali inapaswa kuliangalia upya suala hili la viti maalumu ili kuweza kutoa haki sawa kwa wote,” alieleza Karsan.
Akifafanua alisema mara nyingi pamekuwa pakipatikana taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari nyakati za uchaguzi ambapo habari kadhaa huandikwa zikielezea jinsi wanawake wanavyonyanyaswa huku wengine wakilazimishwa kutoa rushwa ya ngono ili tu waweze kupata viti hivyo maalumu.
Karsan alisema UTPC hivi sasa kwa ushirikiano wa Chama cha wanahabari wanawake (TAMWA) imo mbioni kutengeneza mtandao wa waandishi wa habari watakaokuwa wakiandika habari za ukatili wa kijinsia kwa nchi nzima lengo likiwa ni kuweza kuihabarisha jamii juu ya madhara ya vitendo hivyo na kuonesha hatua za kuchukuliwa pale vinapotokea.
Naye mkurugenzi mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika katika maeneo yao ambapo alisema jamii nchini inaweza kubadilika kwa kiasi kikubwa iwapo vyombo vya habari vitawaelimisha kwa kina juu ya ubaya wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Post a Comment