Washiriki wa warsha ya siku moja iliyowashirikisha viongozi wa vyama vya siasa wilayani Shinyanga na viongozi wa wazee kujadili jinsi vyama vya siasa vitakavyoweza kushughulikia matatizo ya wazee bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa. Pichani wakinyoosha viungo vyao ili kuweza kufuatilia vyema mada.

Wazee wakifuatilia mada

Kiongozi kutoka chama cha NCCR-Mageuzi akiwasilisha maoni ya kundi lake mbele ya washiriki wa warsha hiyo ya wazee na viongozi wa vyama vya siasa.

Aliyekuwa mwenyekiti wa warsha, Dkt. Mhuli akifunga rasmi warsha hiyo ya wazee.

SERIKALI imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuwapatia mikopo midogo midogo wazee ambao bado wana uwezo wa kufanya shughuli za kilimo ili waweze kujiongezea kipato badala ya kuwa wategemezi kwa watu wengine.


Ushauri huo umetolewa  na mwezeshaji Ramadhani Msoka kutoka Taasisi ya Tanzania Social Protection Network (TSPN) katika warsha ya siku moja iliyowahusisha viongozi wa vyama vya siasa wa wilaya, viongozi wa wazee na iliyoandaliwa na Shirika la TAWLAE  mkoani Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la Help Age International (HAIT).

Msoka alisema pamoja na takwimu kuonesha kwamba asilimia 63 ya mashamba yote yanayolimwa hapa nchini hulimwa na wazee na kwamba pamoja na kuwepo kwa mpango wa Kilimo kwanza, lakini hakuna sehemu yoyote inayoelezea jinsi gani ya kuwasaidia wazee ili nao waweze kulima kilimo cha kisasa.

Alisema pamoja na wazee kuwa sehemu ya jamii hapa nchini lakini bado hawaaminiwi na taasisi mbalimbali za kifedha hivyo kushindwa kupata mikopo kutoka katika taasisi hizo hali na hivyo kushauri ni vyema sasa serikali ikaangalia uwezekano wa kuwasaidia kuwapatia mikopo ya kilimo wazee ambao bado wanajishughulisha na shughuli hizo.

Msoka alisema pamoja na kuwepo kwa sera ya wazee lakini bado serikali imekuwa ikisuasua katika kuitungia sheria sera hiyo ili iweze kufanya kazi vizuri na wazee waweze kupatiwa huduma muhimu walizoahidiwa hasa ikizingatiwa hivi sasa wengi wao wamegeuka kuwa walezi wa watoto wao walioathirika na UKIMWI.

Alisema pia takwimu zinaonesha asilimia 50 ya watoto yatima hapa nchini wanalelewa na wazee huku asilimia 80 ya wazee ambao ni asilimia 5.6 ya watanzania wote wanaishi maeneo ya vijijini ambako kuna maisha duni na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii na hivyo kuhitajika juhudi kubwa ya kuwasaidia.

“Hivi sasa asilimia 73 ya waathirika wa UKIMWI hurudi nyumbani kulelewa na wazee wao, lakini ni wazee hawahawa ambao hawana msaada wowote kutoka serikalini, hawakopesheki, na pia ndiyo walio katika hatari ya kuuawa kikatili kutokana na imani potofu za kishirikina hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa, maisha yao yapo shakani kila siku,” alieleza Msoka.

Kutokana na hali hiyo alitoa wito kwa vyama vya siasa kueleza wazi katika sera na ilani zao za uchaguzi ya jinsi gani watakavyoshughulikia matatizo ya wazee bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa kwa vile matatizo ya wazee yanafanana na hayafuatia itikadi ya kisiasa.

Kwa upande wao viongozi wa vyama vya siasa kutoka CCM, NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA waliahidi kufanyia kazi yale yote waliyokubaliana katika warsha hiyo ambapo kwa yale yanayostahili kuingizwa ndani ya sera na ilani zao za uchaguzi watayafikisha katika vikao husika ili yafanyiwe kazi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top