Mmoja wa askari polisi mkoani Shinyanga akitoa elimu juu ya ulinzi shirikishi.  Wadau wamelipongeza jeshi hilo kwa jinsi linavyoimarisha ulinzi mkoani Shinyanga.


WADAU wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga wamelipongeza jeshi hilo kwa kazi nzuri wanayoionesha katika kupambana na vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo pamoja na kwamba wanafanya kazi yao katika mazingira magumu.


Pongezi hizo zilitolewa  na Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila wakati wa ufungaji wa warsha ya siku moja kwa wadau wa Jeshi la Polisi iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya siku maalumu ya Polisi katika mkoa wa Shinyanga.

Nkulila alisema pamoja na polisi kufanya kazi zao katika mazingira magumu lakini bado wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali hali ambayo imewezesha wakazi wa mkoa wa Shinyanga kuishi kwa amani na usalama.

“Kwa niaba ya wadau wa polisi hapa mkoani petu nichukue fursa hii kukupongezeni kwa kazi nzuri mnazozifanya kila siku, mkoa wetu kwa hivi sasa hauna matukio ya kutisha, hali hii inatokana na jinsi mlivyoimarisha ulinzi, endeleeni na juhudi hizo,”

“Kwa upande wetu sisi viongozi wenye dhamana ya kuongoza watu tunapaswa kuihamasisha jamii ione umuhimu wa kushirikiana na polisi wetu katika kuimarisha ulinzi katika maeneo yao kupitia mpango wa ulinzi shirikishi, na wananchi wetu wasisite kutoa taarifa wawaonapo polisi wachache wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi yao,” alieleza Nkulila.

Aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuwalalamikia polisi kwamba hawatimizi wajibu wao kwa vile alisema hata ndani ya jeshi hilo wapo polisi wachache wasio waadilifu ambao isiwe sababu ya kuharibu sifa za wengine ambapo alitoa mfano hata upande wa viongozi wa umma wapo wachache wasio waadilifu.

Akiwasilisha mada katika warsha hiyo, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu, Mpinga Gyumi alisema kwa hivi sasa hali ya ulinzi na usalama hapa nchini inakwenda vizuri japokuwa kuna matukio ya hapa na pale ya uhalifu ambayo hata hivyo kwa ushirikiano wa wanajamii mengi hudhibitiwa mapema.

Hata hivyo katika kuhakikisha suala la ulinzi na usalama linaimarika katika mkoa wa Shinyanga, Gyumi alisema ni muhimu kwa viongozi wa vitongoji na mitaa kuhakikisha wanazingatia suala la matumizi ya daftari la wakazi katika maeneo yao ili kuwezesha kila mgeni anayeingia anafahamika na kuorodheshwa ndani ya daftari hilo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku alisisitiza suala la polisi kata kuishi katika kata wanazopangiwa badala ya kukaa mijini hali ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa wananchi kushindwa kupata msaada wa haraka panapotokea tukio lolote la kiuhalifu katika maeneo yao.

“Pamoja na hali ya usalama na utulivu tulionao katika  mkoa wetu lakini bado tunakabiliwa na tatizo la mauaji ya wanawake vikongwe, hili linahitaji juhudi na ushirikiano wa kila mdau kulikomesha kabisa, na kikubwa kinachohitaji ni kutoa elimu kwa wananchi wetu waone ubaya wa kumuua mtu bila ya sababu,” alieleza Nkhambaku.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top