Mbunge wa viti maalumu mkoani Shinyanga, Azza Hillal akimkabidhi baiskeli ya walemavu mtoto mwenye ulemavu mkazi wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga, wa kwanza kushoto ni mama mzazi wa mlemavu huyo, Mwajabu Abdalah.

Mbunge wa viti maalumu Azza Hillal (kulia) akikabidhi msaada wa viti 150 kwa ajili ya mradi wa ukodishaji wa viti utakaoendeshwa na ofisi ya UWT Shinyanga mjini, anayepokea msaada huo ni mwenyekiti wa UWT wilaya ya Shinyanga mjini, Shella Mshandete, wa kwanza kushoto ni katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Sangija.
WANAWAKE wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini wameshauriwa kujitokeza kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya kukaa kusubiri nafasi za viti maalumu au kuteuliwa na Rais.

Ushauri huo umetolewa na mbunge wa viti maalumu mkoani Shinyanga na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Azza Hillal alipokuwa akizungumza na wajumbe wa mabaraza ya Jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT) katika wilaya za Kishapu na Shinyanga mjini.

Azza alisema hakuna sababu ya wanawake kuogopa kugombea nafasi za majimbo kwa vile mara nyingi hudai wanaweza bila ya kuwezeshwa hivyo wakati chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu vikikaribia wanapaswa kujiandaa kwa ajili ya kugombea nafasi hizo badala ya kusubiri kupitia viti maalumu.

“Ndugu zangu sisi wanawake tunao uwezo mkubwa wa kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi iwapo tu tutaondoa woga tulionao, mara nyingi tumekuwa tukiwaachia wanaume kugombea nafasi muhimu kwa hofu tu ya mfumo dume kwamba watatushinda, hata pale tunapokuwa na uwezo kuliko wao wanaume bado hatujitokezi,”

“Wito wangu leo kwenu ninawaomba tuondoe woga, uchaguzi ujao tuwashangaze wanaume, tugombee pale ambapo tunaona tuna uwezo, iwe udiwani, ubunge na hata urais, sisi ni wengi, tukishikamana na kuacha kuoneana wivu ni wazi wanaume tutawagaragaza vibaya, mradi tuwe na uwezo tusifanye majaribio,” alieleza Azza.

Katika hatua nyingine mbunge huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kuacha tabia ya kuwaficha na badala yake wawapatie fursa za kupata elimu kama wanavyopatiwa watoto wengine na kwamba mtu anapomficha mlemavu anamuongezea matatizo zaidi.

Azza alisema walemavu wana haki sawa na watoto wengine na kwamba pale wazazi ama walezi watakapokuwa hawana uwezo wa kuwatunza watoto wenye ulemavu zipo asasi mbalimbali na jamii yenyewe wanaweza kutoa msaada wa kuwasaidia ikiwemo kuwawezesha kwenda shule na kuwapatia vifaa vya usafiri kwa wasio na uwezo wa kutembea.

Alisema yeye binafsi pamoja na kutokuwa na fungu la mfuko wa jimbo kama ilivyo kwa wabunge wa majimbo, ameamua kutoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia baadhi ya walemavu mkoani Shinyanga ikiwemo viti na baiskeli za walemavu ambazo kwa kiasi fulani zitawapunguzia matatizo wao wenyewe, wazazi na walezi wanaowalea.

“Niombe tu watu wengine wenye uwezo wajitokeze kuwasaidia ndugu zetu hawa wenye ulemavu, hawa ni watanzania wenzetu, wana haki kama watu wengine, hivyo tusiwanyanyapae tuwaone ni sehemu ya jamii, tukumbuke tu sote hapa ni walemavu watarajiwa, hakuna anayeelewa huku mbele atakumbwa na mkasa gani,” alieleza Azza.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top