Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Wilson Nkhambaku akifungua moja ya vikao vya mabaraza ya madiwani wilayani mwake.
Sehemu ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakifuatilia kikao cha Baraza la madiwani.

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakiwa katika moja ya vikao kwa mujibu wa sheria na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 145 (1), (2) hadi ya ibara 146 (1) – (2).
SERIKALI kuu imeshauriwa kuzitambua mamlaka za serikali za mitaa nchini ambazo ndizo zilizoko karibu zaidi na wananchi na kuombwa iache tabia ya kutoa maagizo kutoka juu bila ya kuzishirikisha mamlaka hizo za chini.

Hali hiyo imetajwa kuleta mgongano mkubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kutokana na serikali kuu mara nyingi kutoa maelekezo yanayokinzana na mipango ambayo tayari imepangwa na halmashauri husika.

Akizungumza na Majira mjini Shinyanga mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya Taifa (NEC) kutoka wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Boniface Butondo alisema kwa kipindi kirefu serikali kuu kupitia ofisi ya waziri mkuu imekuwa ikitoa maagizo mbalimbali kwenda katika halmashauri za wilaya bila ya kuzishirikisha halmashauri husika.

Butondo aliyekuwa akizungumzia agizo lililotolewa na waziri mkuu Mizengo Pinda la kuzizuia halmashauri za wilaya kukusanya ushuru wa zao la pamba na badala yake ukusanywe na Bodi ya Pamba nchini alisema agizo hilo kwa kiasi kikubwa litavuruga mipango yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa na halmashauri yao ya Kishapu.

Alisema yeye binafsi ameshangazwa na agizo hilo na haoni sababu hasa iliyosababisha waziri mkuu atoe tamko hilo na kwamba amelitoa bila ya kuangalia jinsi gani halmashauri zinazotegemea ushuru huo zitakavyoathirika kutokana na kutolewa wakati tayari halmashauri zote husika zimeishapitisha bajeti zake za mwaka 2014/2015.

“Nimeshangazwa na uamuzi huu wa waziri mkuu kutoa agizo ambalo litaathiri mipango yetu ya maendeleo, miradi mingi tunaitekeleza kwa mapato ya ndani, asilimia 75 ya mapato hayo yanatokana na ushuru wa pamba, kwa mwaka huu tumepanga kukusanya shilingi bilioni 1.3, karibu nusu ya mapato yote ya ndani tuliyopanga kukusanya ambayo ni shilingi bilioni 2.9,”

“Lakini pia kwa upande mwingine hatukushirikishwa wala kushauriwa kabla ya kutolewa kwa agizo hili, serikali kuu inapaswa ielewe kuwa hizi serikali za mitaa ni serikali kamili na zimeundwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kutoa maagizo bila ya kuzishirikisha ni kutozitendea haki, na huenda viongozi wa serikali kuu hawathamini uwepo wake,” alieleza Butondo ambaye pia ni diwani wa kata ya Lagana Kishapu.

Mjumbe huyo wa NEC alisema kitendo cha Bodi kuagizwa ikusanye ushuru huo kitachangia kutokea kwa mgogoro mkubwa kati yake na halmashauri kutokana na bodi kuwa na matatizo makubwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali na kutoa mfano ilivyoshindwa kusimamia vizuri mfuko wa wakulima wa kununulia pembejeo maarufu kwa jina la “Pass book.”



Butondo alisema ni vizuri viongozi wakuu ndani ya serikali kuu wawe na utamaduni wa kuziheshimu mamlaka za serikali za mitaa ambazo zimeundwa kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 145 (1), (2) hadi ya ibara 146 (1) – (2) na kwamba si vizuri kwa serikali kuu kutoa maagizo mazito bila ya kuzishirikisha.

“Binafsi namshauri waziri mkuu akae chini na kuangalia upya uamuzi wa kuzizuia halmashauri kukusanya ushuru huu wa zao la pamba, huenda alishauriwa vibaya, vinginevyo miradi yetu mingi ya maendeleo itakwama kutekelezwa na hata bajeti tulizopitisha kwa mwaka huu wa fedha zitakuwa zimevurugika,” alieleza Butondo.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top