Mpina (aliyeweka mikono mfukoni) akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa viongozi waandamizi wa kiwanda cha kutengeneza nyuzi kilichopo eneo la Nhelegani manispaa ya Shinyanga. |
Msemaji wa kampuni Jim Lin akitoa maelezo kwa Mheshimiwa Mpina. |
Sehemu ya kiwanda hicho. |
Mpina akiwa na viongozi wa kiwanda cha Dahong Group Ltd. |
Mpina akiangalia ngozi ambazo zimekamilika kutengenezwa zikisubiri hatua ya kufungwa ndani ya mafurushi kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi. |
Hapa anaangalia mandhari ya ndani ya kiwanda. |
Ngozi ambazo zimeishafungwa ndani ya mafurushi zikisubiri kupelekwa nje ya nchi kuuzwa. |
Ushauri huo umetolewa mjini Shinyanga na mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina baada ya kuvitembelea viwanda viwili vya kutengeneza nyuzi na kusindika ngozi vilivyojengwa na wawekezaji kutoka nchini China na kubaini mapungufu kadhaa ikiwemo ukiukwaji wa mikataba ya uwekezaji wake.
Mpina alisema serikali inapaswa kuwa makini na baadhi ya wawekezaji wanaoingia nchini kwa lengo la kuwekeza huku wakiwa hawana uwezo wa kuzalisha kile walichoahidi kukizalisha na badala yake hugeuka kuwa kikwazo kwa wawekezaji wazawa pale wanapoamua kuuza bidhaa zao katika soko la ndani.
Alisema wapo wawekezaji ambao wamepata misamaha ya kodi ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya hali ya juu ambazo mbali ya kuipatia serikali mapato lakini pia ingesaidia kupandisha thamani ya shilingi ya Tanzania lakini wameshindwa kutekeleza kikamilifu mikataba yao.
“Ni muhimu hivi sasa serikali ikapitia upya mikataba ya wawekezaji wote wa kigeni ambao wameonesha dhahiri kushindwa kutekeleza kikamilifu mikataba yao, lazima ihakikishe wawekezaji hao wanasitishiwa mikataba yao, kwani baadhi hivi sasa wanazalisha bidhaa ambazo pia zinazalishwa na wazawa na kuziuza hapa hapa nchini,"
“Bidhaa zinazouzwa na mwekezaji wa kigeni hapa nchini bei yake ni ya chini kutokana na kuwa na msamaha wa kodi tofauti na bidhaa zinazozalishwa na wazawa ambao wanalipia kodi zote za serikali, sasa hii ni hatari kwa watanzania, serikali ihakikishe hawa watu wanaheshimu mikataba yao,” alieleza Mpina.
Akifafanua mwenyekiti huyo ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu mkoa wa Simiyu alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha mwekezaji kampuni ya Xing Hua Investment Co. Ltd. kinachosindika ngozi eneo la viwanda manispaa ya Shinyanga kusimamisha uzalishaji wake hivi sasa kwa madai ya kuanguka bei katika soko la dunia.
Msemaji wa kampuni hiyo Chen Teng alimweleza Mpina kwamba kiwanda chao kimesimamisha uzalishaji hivi miezi miwili sasa kutokana na kuanguka kwa bei ya ngozi katika soko la dunia na pia wafugaji hivi sasa wamepandisha bei ya ngozi na hivyo wanahofia kupata kupata hasara.
Hata hivyo akiwa katika kiwanda cha kutengeneza nyuzi cha kampuni ya Dahong Group Ltd. Mpina alipigwa na mshangao baada ya kuelezwa kuwa mwekezaji huyo hivi sasa hatoweza kujenga tena kiwanda cha kutengeneza nguo kama mkataba wake unavyoelekeza akihofia kupata hasara na badala yake atatengeneza nyuzi pekee.
“Kwa kweli ni hali ya kusikitisha sana, hawa watu walipokuja nchini walisema wana uwezo wa kuwekeza katika sekta ya viwanda vya nguo, nyama, kutengeneza nyuzi, na mikataba yao inaonesha hivyo, leo hii wamejenga kiwanda cha nyuzi pekee cha nguo wanakataa kukijenga wakihofia hasara, lakini hizi nyuzi watapeleka kwenye viwanda vyao China,”
“Huu ni ujanja, maana wamebaini iwapo watajenga kiwanda cha nguo hapa nchini ni wazi wataua viwanda vilivyoko nchini kwao, hivyo wameona bora watengeneze hiki cha nyuzi na nyuzi hizo zipelekwe China ambako watatengeneza nguo na kuzileta hapa nchini kuwauzia watanzania kwa bei kubwa, hii haikubaliki,” alieleza Mpina.
“Ni kweli mbali ya kiwanda hiki cha nyuzi tulitakiwa kujenga pia cha kutengeneza nguo na shule kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima wa zao la pamba, lakini tumeona kwa sasa tuachane na kiwanda cha nguo badala yake nyuzi zetu tutapeleka China, lakini hivi sasa tumeanza ujenzi wa shule ya wakulima,” alieleza msemaji wa kampuni ya Dahong Group Ltd. Jim Lin.
Aidha Mpina alisema mwekezaji wa kiwanda cha kusindika ngozi ameonesha wazi hana uwezo wa kifedha baada ya kushindwa kununua ngozi kutoka kwa wafugaji kwa madai wana bei kubwa na kuanguka kwa bei katika soko la dunia na hivyo kusimamisha uzalishaji ikiwa ni miezi michache tangu kilipoanza uzalishaji wake.
Post a Comment