Mkurugenzi msaidizi kitengo cha pembejeo za kilimo, Canuth Komba akifungua rasmi mkutano wa mawakala wa pembejeo za kilimo kanda ya ziwa uliofanyika mjini Shinyanga., |
Mwenyekiti wa TANADA wa Taifa, Marco Mahecha akizungumza na wajumbe wa mkutano wa mawakala wa pembejeo za kilimo kanda ya ziwa katika mkutano uliofanyika mjini Shinyanga. |
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo akichangia hoja. |
Wajumbe wakifuatilia mkutano kwa umakini mkubwa. |
Mmoja wa watendaji kutoka wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika nchini, Sofia Masawe (Ofisa kitengo cha mbegu) akifuatilia mkutano. |
WIZARA ya kilimo, chakula na ushirika nchini
imefanikiwa kutoa mafunzo kwa mawakala 3,855 wa pembejeo za kilimo nchini juu
ya uendeshaji wa biashara, matumizi bora ya kilimo na hifadhi salama ya
pembejeo za kilimo kwa lengo la kuboresha sekta ya kilimo nchini.
Hali hiyo imebainishwa mjini Shinyanga na
mkurugenzi msaidizi kutoka wizara ya kilimo nchini Canuth Komba alipokuwa
akifungua mkutano mkuu wa mawakala wa pembejeo Tanzania kutoka kanda ya Ziwa
ambapo alisema serikali imetoa mafunzo hayo kutokana na kutambua mchango wa
mawakala hao.
Komba alisema juhudi zinazofanywa na mawakala
hao zimewezesha suala la upatikanaji wa pembejeo kwenye maeneo ambayo
yanapatiwa ruzuku kuweza kupatikana katika kila kijiji ikilinganishwa na hapo
awali ambapo wakulima walilazimika kwenda kuzinunua makao makuu ya wilaya au
katika miji midogo.
Alisema hivi sasa serikali imepania kuleta
mapinduzi ya kijani ambayo yanategemea mambo muhimu ya msingi yakiwemo
upatikanaji wa matumizi bora ya pembejeo za kilimo, huduma bora za ugani na
matumizi ya kilimo cha umwagiliaji.
“Sote tunafahamu umuhimu wa matumizi bora ya
pembejeo za kilimo, mbegu bora, mbolea na viuatilifu katika kuongeza uzalishaji
na tija. Hata hivyo pembejeo hizi muhimu
katika kilimo haziwezi kuwafikia wakulima kwa wingi na kwa wakati iwapo
mawakala hawatashiriki kwa ukamilifu na uaminifu,”
“Nashukuru kwa juhudi zenu na serikali inaamini
zitasaidia katika kuwanufaisha wakulima wetu katika kuongeza uzalishaji wa
chakula, tija na kuleta mapinduzi ya kijani ili dhana ya kilimo kwanza ipate
kufikiwa, na serikali inasisitiza suala la kufanya kazi zenu kwa mujibu wa
sheria na kanuni za mbegu, mbolea na madawa,” alieleza.
Alisema sekta ya kilimo ni moja ya sekta muhimu
katika uchumi wa maendeleo ya nchi ambapo inatoa ajira kwa asilimia 74 ya
watanzania huku ikichangia kwa asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini
kwa miaka yenye mvua za kutosha.
“Tathmini ya uvunaji wa mazao na upatikanaji wa
chakula kwa mwaka 2013/2014 inaonesha uzalishaji wa mazao ya chakula, hususan
nafaka uliongezeka kutoka tani milioni 6.7 mwaka 2012 hadi tani milioni 7.6 kwa
mwaka 2013 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 13.4 na hali imekuwa
ikiongezeka mwaka hadi mwaka,”
“Mkutano huu ni muhimu kwani utawapa fursa ya
kutoa taarifa juu ya maendeleo, matatizo na changamoto zinazojitokeza katika
kuwaendeleza mawakala ambao ni kiungo muhimu katika kuwafikishia wakulima
pembejeo za kilimo,”
“Pia ni fursa nzuri kwa wadau kubadilishana
mawazo, uzoefu na hatimaye kutayarisha mkakati utakaosaidia kuongeza kasi ya
usambazaji na ubora wa pembejeo za kilimo, ili ziweze kuwafikia wakulima kwa
wakati, bei nafuu na hatimaye kuleta mapinduzi ya kijani (Green Revolution) na
kuleta kilimo chenye tija kwa wananchi wa Tanzania,” alieleza Komba.
Post a Comment