Meneja wa Shirika la Save the Children, Augustino Mwashiga akiwasilisha mada kwa washiriki wa uzinduzi wa mradi wa kupunguza udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano mkoani Shinyanga. |
Washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika uzinduzi huo. |
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na Ofisa Lishe mkoani Shinyanga, Mariam Mwita. |
Hali hiyo imebainishwa mjini Shinyanga wakati wa uzinduzi wa mradi wa kupunguza udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano (Accelerating Nutrition Initiatives (ANI) mkoani humo ambapo ilielezwa kuwa asilimia 43 ya watoto wanakabiliwa na tatizo la udumavu.
Akifungua rasmi kikao cha uzinduzi wa mradi huo, katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Anselm Tarimo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na msaidizi wake, Rubanzibwa Projectus alisema kunahitajika juhudi za makusudi ili kukabiliana na tatizo hilo.
Dkt. Tarimo alisema moja ya sababu inayochangia udumavu kwa watoto ni tabia ya wanawake wengi kutozingatia taratibu za unyonyeshaji watoto wao ambapo takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 13 tu ya wanawake wanaojifungua ndiyo hunyonyesha watoto wao kwa miezi sita bila ya kuwapa vyakula vingine.
Hata hivyo alisema zipo changamoto nyingi zinazochangia hali hiyo ikiwemo suala la elimu duni juu ya masuala ya chakula na lishe, ukame unaosababisha upungufu wa mboga za majani, usindikaji na uhifadhi duni wa chakula na mila na desturi zilizopitiwa na wakati zinazompa kipaumbele baba kupata chakula bora.
“Suala la utapiamlo siyo kwa watoto tu, bali hata wanawake walio katika umri wa kuzaa, kisayansi tutakubaliana kuwa mbegu bora hutoa matunda bora, mama akikosa lishe ni dhahiri hata kiumbe atakachojifungua kitakuwa ni dhaifu na si hilo tu yawezekana pia akapata matatizo wakati wa kujifungua,” ilieleza sehemu ya hotuba ya Dkt. Tarimo.
Kwa upande wake Ofisa mafunzo, elimu ya lishe na mtafiti kutoka wizara ya Afya kitengo cha Taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC), Gelagister Gwarasa alisema ili mradi huo ufanikiwe ni jukumu la wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuielimisha jamii juu ya matumizi ya vyakula mchanganyiko.
Gwarasa alisema takwimu zinaonesha hali ya udumavu unaochangiwa na utapiamlo ni mbaya katika mkoa wa Shinyanga ikilinganishwa na takwimu za kitaifa ambapo wakati kitaifa tatizo la utapiamlo ni asilimia 42.5 lakini kwa mkoa huo ni asilimia 43.3 huku kati watoto watano chini ya miaka miwili wawili wana udumavu.
Naye meneja wa Shirika la Save the Children mkoani Shinyanga linaloendesha mradi huo kwa ushirikiano wa wizara ya afya na Taasisi ya chakula na lishe, Augustino Mwashiga alisema mradi huo katika mkoa huo utatekelezwa katika wilaya za Kishapu na Kahama ambako ndiko kwenye tatizo kubwa ikilinganishwa na wilaya nyingine za mkoa huo.
Kwa mujibu wa Mwashiga mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la kimataifa la nchini Canada, Canadian Department of Foreign Affairs Trade, and Development (DFATD) chini ya Shirika la afya duniani (WHO) utatekelezwa katika wilaya 11 zilizopo kwenye mikoa ya Lindi na Shinyanga utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.
Post a Comment