BAADHI ya wakazi wa manispaa ya Shinyanga wameulalamikia uongozi wa serikali mkoani humo kukukubali kupandishwa hadhi kwa hospitali ya mkoa kuwa ya rufaa wakidai uamuzi huo umechukuliwa kwa kukurupuka.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari mjini humo baadhi ya wakazi hao wamedai kitendo cha uongozi wa mkoa kukubali kupandishwa hadhi kwa hospitali hiyo kimeanza kuwasababishia matatizo kutokana na kutokuwepo maandalizi yoyote ya maana katika Zahanati za manispaa wanazoshauriwa kuanzia kwa ajili ya kupata matibabu.
Aprili mosi mwaka huu uongozi wa hospitali hiyo uliwatangazia wakazi wa mkoa huo mabadiliko ya utolewaji wa huduma sambamba na ongezeko la gharama za matibabu katika vitengo vyake vyote ikiwemo wajawazito kutozwa shilingi 70,000 wanapokwenda kujifungua, watakaohitaji upasuaji mkubwa shilingi 80,000 na shilingi 40,000 kwa kung’oa jino moja.
Wakazi hao wanasema serikali ilipaswa kufanya maandalizi ya kina katika zahanati zote kwa kuongeza miundombinu muhimu ili ziweze kumudu ongezeko la wagonjwa kabla ya kuipandisha hadhi hospitali hiyo kuwa ya rufaa hasa ikizingatiwa kuwa ni wilaya moja tu mpaka sasa katika mkoa (wilaya ya Kahama) ndiyo yenye hospitali kamili ya wilaya.
Mmoja wa wakazi hao aliyekutwa na waandishi wa habari nje ya Zahanati ya Kambarage, Bilali Mjanakheri alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha serikali kuiruhusu zahanati hiyo kuanza kutoa huduma kama kituo cha afya huku ikiwa na jengo moja tu la kutolea huduma kitu ambacho alidai ni kinyume cha sheria za afya.
“Hii hali kwa kweli viongozi wetu huenda walikurupuka aidha walichukulia uamuzi huo kisiasa zaidi badala ya kuangalia uhalisia wake na kujali afya za wananchi, hili jengo unaloliona ndilo linalotoa huduma zote, kliniki ya mama na mtoto, vyumba vya madaktari, maabara, chumba cha sindano, vidonda, akina mama wanaojifungua na huduma za meno,”
“Inasikitisha sana, nimelazimika kukaa hapa nje baada ya kushindwa kuvumilia sauti za mama anayejifungua ndani, hakuna ufaragha kwa akina mama hawa, kila mtu anasikia jinsi wanavyohangaika, jamani huku si kuwadhalilisha? Hawa wanahitaji watengewe jengo lao maalumu tofauti na hali ilivyo sasa, nasikia hawana hata sehemu ya kupumzikia baada ya kujifungua!!” anaeleza Mjanakheri.
Kwa upande wake mkazi wa kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga ambaye hata hivyo hakupenda kutajwa gazetini amesema zahanati hiyo haistahili kuitwa kituo cha afya kama inavyoshinikizwa na viongozi wa kiserikali kutokana na kuwa na mapungufu mengi ikiwemo kutokuwepo sehemu ya kujisaidia wajawazito wanapokwenda kujifungua.
“Hawa viongozi wetu hawawezi kuyafahamu matatizo haya, wao binafsi hawana muda wa kuzitembelea zahanati hizi kuangalia baada ya kuelekeza tuje huku, je zinamudu kutoa huduma kikamilifu?, baba yangu sisi wajawazito ni kama vile tunadhalilishwa, maana sehemu tunakojifungulia hata choo hakuna, tunalazimishwa kuja na mabeseni kwa ajili ya kujisaidia,” ameeleza.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Zahanati ya Kambarage, Dkt. Costantine Hubi amekiri zahanati yake kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa na kwamba hivi sasa inatoa huduma zake kama kituo cha afya japokuwa haijafanyiwa mabadiliko yoyote ya usajili kutoka hadhi ya zahanati na kuwa kituo cha afya.
“Ni kweli hiki si kituo cha afya, usajili wake unasomeka ni zahanati, na ukisema ni kituo itakuwa bado hakikidhi vigezo vya vinavyohitajika, mnaona huduma zote tunatolea ndani ya jengo moja, eneo la maabara tumelazimika kusitisha upimaji wa wagonjwa wa TB na kuwalazimisha waende hospitali ya mkoa,” anaeleza Dkt. Hubi.
Post a Comment