Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini akiwasilisha mapendekezo ya mipango mkakati iliyojadiliwa katika kundi la chama chake jinsi ya kuwasaidia wazee wilayani kwake. |
Washiriki wa warsha wakifuatilia mafunzo kwa makini. |
VYAMA vya siasa vya CCM, NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA wilayani Shinyanga vimekubaliana kila kimoja kujiwekea mpango mkakati wa jinsi wa kutatua matatizo yanayowakabili wazee katika wilaya hiyo bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika warsha maalumu iliyoandaliwa na Shirika la TAWLAE mkoani Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la Help Age International – (HAIT) Tawi la Tanzania na kuwashirikisha viongozi wa vyama hivyo vya siasa wakiwemo viongozi wa mabaraza ya wazee wilayani humo.
Hatua hiyo inatokana na michango mbalimbali iliyowasilishwa katika warsha hiyo na kubainika kuwa matatizo mbalimbali yanayowakabili wazee wengi nchini yanafanana na hayawapati kwa kufuata itikadi ya vyama vyao vya siasa ambapo viongozi hao waliahidi kufikisha mipango mikakati hiyo katika vikao vya maamuzi ndani ya vyama vyao ili iweze kufanyiwa kazi.
Mmoja wa wawezeshaji katika warsha hiyo, Ramadhani Msoka ambaye ni makamu mwenyekiti kutoka Shirika la Tanzania Social Protection network (TSPN), alisema vyama vya siasa vina fursa nyingi ya kuweza kuwasaidia wazee nchini kwa vile vinaweza kuweka mipango mikakati mbalimbali ya jinsi ya kutatua kero kupitia ilani zao za uchaguzi na sera za chama husika.
Msoka alisema kwa mujibu wa taratibu zilizopo hivi sasa hapa nchini kila kinapofika kipindi cha uchaguzi mkuu, kila chama hupata fursa ya kunadi sera na ilani yake ya uchaguzi kwa wapiga kura ambamo ndani ya ilani ndimo hueleza mambo gani itakayowatekelezea wananchi wake iwapo watakipa ridhaa ya kuunda serikali.
“Mnayo fursa kubwa ya kuweza kuwasaidia wazee, sasa wakati tunaelekea kwenye chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu TAWLAE na Help Age International wameona kuna kila sababu ya kuwakutanisheni ninyi viongozi wa kisiasa na wazee wenyewe ili mjadili kwa pamoja kuona ni mambo gani ya msingi wanayohitaji kusaidiwa,”
“Tunataka kila chama sasa kijiwekee mpango mkakati wa jinsi wa kushughulikia matatizo ya wazee ili iwapo kitapata ridhaa ya kuunda serikali basi kiweze kuyafanyia kazi, lakini pia kwa wale walioko madarakani hivi sasa, tuache tabia ya kuwasemea wazee, tuwape nafasi wajisemee wenyewe matatizo yanayowakabili,” alieleza Msoka.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya mwaka 2012 inaonesha idadi ya wazee hapa nchini ni asilimia 5.6 ya watanzania wote ambao ni 2,507,568 huku wakilazimika kulea zaidi ya asilimia 50 ya watoto yatima waliopo nchini ambapo asilimia 80 ya wazee wote wanaishi maeneo ya vijijini.
“Tuwaombe vijana wa sasa waliokabidhiwa jukumu la utoaji huduma mbalimbali za kijamii waache tabia ya kuwabagua wazee au kupuuza masuala wanayoomba kuboreshewa, maana hicho kinachopiganiwa sasa na wazee hao ndicho watakachonufaika nacho zaidi wao watakapozeeka, mfano dai la wazee wote kulipwa pensheni bila kujali walikuwa waajiriwa,” alieleza Msoka.
Kwa upande wake mratibu wa TAWLAE mkoani Shinyanga, Elisanya Nnko aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa ili kuhakikisha wanafanikishia malengo wanayokusudia katika kushughulikia matatizo ya wazee ambapo aliwaomba makubaliano hayo yasiishie ukumbini bali wayafikishe katika ofisi zao ili yaweze kufanyiwa kazi.
Post a Comment