Ofisaelimu ya mpiga kura kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Salvatory Alute (aliyesimama) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) katikati ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Festo Kang'ombe.
Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga wakifuatilia hotuba ya mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva alipokuwa akifungua mkutano kati ya tume yake na waandishi wa habari.
TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewatoa hofu watanzania na kuwaomba
waendelee kuiamini pamoja na kwamba mwenyekiti na makamishina wake
wanateuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Hali hiyo ilibainishwa
na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alipofungua mkutano kati ya tume na waandishi wa habari mkoani Shinyanga
kwa ajili ya kupatiwa taarifa juu ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari
la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa teknolojia ya Biometrick Voter
Registration (BVR).
Jaji Lubuva amesema pamoja na kwamba Rais
ndiye aliyemteua yeye pamoja na makamishina wengine wa tume lakini haiwi
sababu ya kuwafanya watanzania waamini kuwa tume hiyo siyo huru na
kwamba tangu alipoteuliwa kuwa mwenyekiti wa tume haijatokea hata siku
moja kuelekezwa na Rais au chama chochote cha siasa kitu cha kufanya.
“Ndugu
zangu si kweli kwamba kitendo cha Rais kumteua mwenyekiti wa tume ya
uchaguzi pamoja na makamishina wake kinaondoa uhuru wa tume hiyo katika
kutimiza wajibu wake, binafsi tangu niteuliwe, Rais wala kiongozi ye
yote wa siasa hawajawahi kunielekeza nini cha kufanya, muda wote tume
ipo huru,”
“Tatizo hapa ni hisia zilizomo ndani ya vichwa vya
wananchi, kwamba kwa vile tunateuliwa na Rais basi hatuwezi kuwa huru,
lakini tupende tusipende mamlaka ya mwisho ya uteuzi bado yataendelea
kubaki mkononi mwa Rais wa nchi labda tusubiri iwapo mchakato wa katiba
mpya utapita kule Dodoma ndani ya bunge la katiba,” anaeleza.
Akizungumzia
uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia
ya Biometric Voter Registration (BVR) alisema lengo ni kuondoa
changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya teknolojia ya Optical Mark
Recognition (OMR) uliosababisha daftari la kudumu la wapiga kura kuwa na
kasoro nyingi.
“Matumizi ya BVR yatapunguza au kuondoa kabisa
matatizo yaliyomo kwenye daftari lililopo ikiwemo kuzuia mtu
kujiandikisha zaidi ya mara moja. Lakini pia tunaomba ieleweke na
kusisitiza kuwa kitambulisho hiki cha BVR – Kit ni kwa ajili ya
uandikishaji wapiga kura tu na hatutopiga kura kwa njia ya kielektroniki
au vinginevyo,” anaeleza Jaji Lubuva.
Akifafanua kuhusu
uboreshaji huo wa daftari, alisema baada ya kuanza kwa uandikishaji
wapiga kura wote waliojiandikisha awali na ambao hawajaandikishwa
walazimika kwenda vituoni kwa ajili ya kuandikishwa upya kwa maana ya
kuchukuliwa taarifa za kibaiolojia kwa wale waliomo ndani ya daftari na
kubadili taarifa kwa waliohama maeneo au kubadili majina.
Jaji
Lubuva aliwaomba waandishi wa habari kusaidia kuihamasisha jamii ili
ione umuhimu wa kwenda kujiandikisha pale kazi hiyo itakapoanza na
waache kuwasikiliza wapotoshaji wanaodai kwamba uboreshwaji wa daftari
la kudumu la wapiga kura umelenga kukisaidia au kukipendelea chama
chochote cha siasa.
“Waandishi ni sehemu muhimu katika jamii,
ninyi mkielewa itakuwa rahisi kuielimisha jamii, tuwaomba mtusaidie
kuwaondoa wasiwasi wananchi kwamba wasiwe na tabia ya kuogopa
mabadiliko, wapo wanaohofu yasije kutokea kama ilivyotokea katika nchi
jirani ya Kenya, kwetu hapa mfumo huu wa BVR utaishia katika
uandikishaji pekee, upigaji kura utakuwa kwa mfumo uleule tuliouzoea,”
“Kwa
utaratibu huu wa sasa, vituo vya kujiandikisha vimeongezeka kutoka
24,919 hadi 40,015 vilivyowekwa kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji,
mitaa ili kuwezesha kuwa karibu zaidi na wananchi ili kupunguza
malalamiko ya umbali wa vituo vya kujiandikisha na kuongeza mwamko wa
kujiandikisha na kupiga kura,” anasema Jaji Lubuva.
Post a Comment