Meneja wa utawala bora na haki za binadamu katika shirika la PINGOs
Forum, Emmanuel Saringe akizungumza na baadhi ya wafugaji wa jamii ya kitaturu
katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu, ambapo pamoja na mambo mengine
walilalamikia kutwaliwa kwa sehemu ya ardhi yao na wakulima wa kijiji cha
Isakamaliwa wilayani Igunga mkoa wa Tabora, na hivyo kujikukuta wakikosa maeneo ya kulishia mifugo
yao nyakati za masika.
KISHAPU:
SERIKALI
imeshauriwa kuingilia kati haraka tatizo la mgogoro wa mpaka kati ya wilaya ya
Kishapu mkoani Shinyanga na Igunga mkoani Tabora ili kumaliza migogoro ya muda
mrefu inayojitokeza kati ya wafugaji na wakulima wanaoishi jirani na mpaka huo
na kusababisha mapigano.
Ombi
hilo linatokana na mapigano yaliyotokea hivi karibuni huko katika kijiji cha
Isakamaliwa kati ya wafugaji wa jamii ya kitaturu na wakulima na kusababisha
vifo vya watu watano baada ya kutokea kutokuelewana juu ya eneo la mpaka huku
wafugaji wakilalamikia kuvamiwa kwa eneo ambalo hulitumia kwa ajili ya malisho
ya mifugo yao.
Baadhi
ya wafugaji wa jamii ya kitaturu katika eneo la Magalata wilayani Kishapu mkoa
wa Shinyanga waliozungumza na viongozi wa Shirika lisilo la kiserikali
linalojishughulisha na utetezi wa haki za wafugaji nchini, PINGOs Forum wiki
iliyopita walidai chanzo cha mapigano hayo ni kukamatwa ng’ombe waliodaiwa
kuingia mashambani na kuharibu mazao.
Wafugaji
hao walisema mapigano hayo yalitokea baada ya wakulima wanaoendesha
shughuli za kilimo kandokando ya mto Manonga eneo la Magogo katika kijiji cha
Isakamaliwa wilayani Igunga kukamata ng’ombe wapatao 246 na punda saba ambapo
walimjeruhi kijana aliyekuwa akiwachunga kwa kumpiga mshale mguuni na kumjeruhi
vibaya.
Walisema
kijana huyo aliyetajwa kwa jina la Giligisiti Galiwida alipigwa mshale pale
alipojaribu kuwakomboa ng’ombe waliokamatwa na baada ya wafugaji kupata taarifa
hizo ndipo yalipotokea mapigano kati yao na wakulima na kusababisha vifo vya
watu watano.
“Ukweli
ni kwamba sisi wafugaji tunachokiomba kwa serikali ni kututengea maeneo kwa
ajili ya malisho ya mifugo yetu, muda mrefu tunahangaika kutafuta malisho kwa
vile hatuna maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili yetu kama inavyofanyika kwa
wanyamapori ambao wametengewa maeneo yao ya hifadhi,”
“Inashangaza
kuona kwamba pamoja na ufugaji kutambulika kuwa moja ya shughuli halali za watu
kujipatia kipato, lakini serikali haijatoa kipaumbele katika kutusaidia, kila
siku tunasumbuliwa tukidaiwa tunaharibu mazingira, lakini kule Ngorongoro
wenzetu wanaruhusiwa kuchungia mifugo yao ndani ya hifadhi, tunaomba na sisi
tupewe maeneo,” alieleza Ute Gunju mkazi wa Magalata.
Gunju
alisema wafugaji hapa nchini wana mchango mkubwa tofauti na jinsi
wanavyonyanyaswa na kwamba pamoja na kudharauliwa kwao lakini watu wengi nchini
wanahitaji huduma mbalimbali kutoka kwao ikiwemo upatikanaji wa kitoweo na
maziwa ambapo alitoa mfano wa watu wanaoingia hotelini huomba kupatiwa supu ya
ng’ombe au mbuzi na chai ya maziwa.
Kwa
upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Wilson Nkhambaku mbali
ya kukiri kutokea kwa mapigano kati ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha
Isakamaliwa alisema tayari kamati za ulinzi na usalama katika mikoa ya
Shinyanga na Tabora zimeunda Tume maalumu itakayochunguza ili kubaini chanzo
chake.
“Ni
kweli kule katika kijiji cha Isakamaliwa kulitokea mapigano kati ya wafugaji na
wakulima, tumefuatilia na kubaini chanzo ni kugombea maeneo ya ardhi na mgogoro
wa mpaka, Naibu waziri wa mifugo na uvuvi alikuja na ameahidi kuleta tume ya
wataalamu ili kubaini mpaka halisi ili kumaliza utata uliopo,” alisema
Nkhambaku.
End.
Post a Comment