IGUNGA
SERIKALI
imeshauriwa kuanza mikakati ya kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji
nchini ili kumaliza kabisa migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kati ya
wafugaji na wakulima ambayo tayari imeanza kusababisha mauaji katika maeneo
mengi.
Imeelezwa
kuwa migogoro hiyo inaweza kuendelea kujitokeza kila mara na kusababisha vifo
kwa wananchi wasio na hatia iwapo serikali haitaweka kipaumbele katika
kuainisha maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili makundi hayo mawili
yaache kuhasimiana kwa kugombea maeneo.
Ushauri
huo umetolewa hivi karibuni na meneja wa utawala bora na haki za binadamu
kutoka Shirika la Wafugaji nchini (PINGOs Forum), Emmanuel Saringe alipokuwa
akizungumza kwa nyakati tofauti na wafugaji na wakulima katika wilaya za Igunga
mkoani Tabora, Kishapu Shinyanga, Bariadi na Meatu mkoani Simiyu.
Saringe
alisema migogoro kati ya wakulima na wafugaji inayoendelea hivi sasa katika
maeneo mengi nchini huku ikiwa imesababisha kupotea kwa maisha ya watanzania
wasio na hatia inachangia kwa kiasi kikubwa na kutokuwepo maeneo yaliyotengwa
maalumu kwa ajili ya wafugaji.
Alisema
utatuzi wa migogoro hiyo ni serikali kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili
yaweze kufahamika rasmi kama ilivyofanyika kwa wanyamapori ambapo hifadhi kwa
ajili ya wanyama hao zimetengwa na kuwekea mipaka inayotambulika kisheria na
kwamba inaweza kufanyika pia kwa wafugaji.
“Pamoja
na serikali kila mara kutangaza dhamira yake ya kumsaidia mfugaji hapa nchini
ili aweze kufuga kisasa lakini hakuna utekelezaji wowote unaofanyika kuhusiana
na kauli hiyo, mara kwa mara wafugaji wanashauriwa kupunguza idadi ya mifugo
yao ni ushauri mzuri, swali linabaki palepale kwa hii michache wanayosalia nayo
waifugie wapi?”
Kwa
upande mwingine meneja huyo ameishauri pia serikali kuainisha vizuri mipaka
iliyopo kati ya hifadhi za wanyamapori na maeneo ya serikali za vijiji ili
kupunguza malalamiko ya wanavijiji ambavyo vimepakana na hifadhi hizo
kubughudhiwa kila mara na askari wanyamapori huku mifugo yao ikikamatwa kila mara
na kutozwa faini kubwa.
Nao
wanavijiji vya Mbushi, Bukundi na Jinamo wilayani Meatu, Ihushi na Nkindwabiye
wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu, Magalata wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga
wameiomba serikali kuangalia upya suala la mipaka katika maeneo yao ili
kumaliza migogoro iliyodumu kwa muda mrefu na kusabababisha kutokea mapigano.
Katika
kijiji cha Ihushi uongozi wa serikali ya kijiji ulilalamikia kitendo cha
serikali kuendelea kumega kinyemela eneo la ardhi katika chao na kuongeza upana
wa eneo la hifadhi ya Maswa Game reserve bila ya wao wenyewe kushirikishwa hali
ambayo imewashangaza na kuomba mipaka hiyo ipimwe upya.
Akizungumzia
hali hiyo mkuu wa wilaya ya Bariadi, Erasto Sima alisema ofisi yake haina
taarifa zozote za kusudio la kutaka kuongezwa kwa eneo la Maswa Game reserve
kwa vile idara ya wanyamapori Taifa imekuwa haiwashirikishi viongozi wa
kiserikali kila pale wanapotekeleza majukumu yao.
“Sina
taarifa kama kuna mpango wa kuongezwa kwa eneo la hifadhi ya pori la akiba la
Maswa, maana hawa wenzetu mambo mengi wanayafanya bila ya kutushirikisha, ni
mpaka pale wanapopata tatizo ndipo hukumbuka uwepo wa ofisi serikali katika
eneo husika,”
“Ni
vizuri tukakaa pamoja na kuangalia jinsi gani tunawasaidia wafugaji wetu,
sheria za hifadhi ya wanyamapori zinafahamika, lakini pia wapo wafugaji wenye
tabia ya kuingiza mifugo yao kwa nguvu ndani ya hifadhi, yote haya yanaweza
kupatia ufumbuzi kwa kukaa pamoja kati ya pande zote husika,” alisema Sima.
end.
Post a Comment