IGUNGA Tabora
MIGOGORO
mingi inayotokea mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji nchini imekuwa
ikichangiwa na baadhi ya watendaji waliomo ndani ya serikali kutokana na
kushindwa kutekekeleza majukumu yao kikamilifu katika maeneo yao.
Hali
hiyo imebainishwa wiki iliyopita na baadhi ya wakulima wa kijiji cha
Isakamaliwa wilayani Igunga mkoa wa Tabora waliokuwa wakizungumza na viongozi
kutoka Shirika la Jumuiya ya Mashirika ya Jamii asili za wafugaji na wakusanya
matunda nchini (PINGO’S).
Wakulima
hao walisema baadhi ya watendaji wa serikali hasa wale wa ngazi za vijiji na
kata wamekuwa chanzo cha migogoro mingi inayotokea na kusababisha mapigano kati
ya wakulima na wafugaji na wakati mwingine kutokea mauaji baada ya watendaji
hao kushindwa kusimamia haki kati ya wafugaji na wakulima.
Wakizungumzia
tukio la mauaji ya wakulima watano yaliyotokea Machi 28, mwaka huu walisema
chanzo chake ni ng’ombe wa wafugaji wa jamii ya kitaturu kutoka wilayani
Kishapu mkoa wa Shinyanga kuvamia mashamba ya wakulima yaliyopo katika eneo la
Magogo kandokando ya mto Manonga.
Walisema
hali hiyo imechangiwa na watendaji wa serikali kushindwa kuwatengea maeneo
rasmi wafugaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli za ufugaji na hivyo kujikuta
wakitangatanga na mifugo yao maeneo mbalimbali kwa ajili kutafuta malisho hali
inayosababisha kutokea migogoro kati yao na wakulima.
Kwa
upande wake Ofisa mtendaji kata ya Isakamaliwa, Nyamuhanga Msabi alikiri kuwa
tatizo la mgogoro uliotokea hivi karibuni kati ya wafugaji na wakulima katika
eneo la Magogo limechangiwa pia na mmoja wa watendaji katika kijiji hicho (jina
limehifadhiwa) aliyekuwa akiuza maeneo ya wakulima kwa wafugaji.
Msabi
alisema mtendaji huyo alikuwa na tabia ya kukusanya fedha kutoka kwa wafugaji
na kisha kuwaruhusu kuchungia mifugo yao katika maeneo ya mashamba ya wakulima
ambapo hivi karibuni wafugaji walipodhibitiwa na kudai kurejeshewa fedha zao
aliwaelekeza kuvamia kwa nguvu maeneo hayo hali inayohisiwa kusababisha kutokea
kwa mapigano hayo.
Mkuu
wa wilaya ya Igunga, Emmanuel Kingu alikiri kuwepo kwa watendaji wasio
waaminifu wanaochangia kutokea kwa migogoro ya wakulima na wafugaji na kwamba
tayari ofisi yake imemchukulia hatua mtendaji anayetuhumiwa kuchangia kutokea
kwa mapigano kati ya wakulima wa Isakamaliwa wilayani Igunga na Magalata
wilayani Kishapu.
“Migogoro
hii itamalizika tu iwapo watendaji wa serikali tutajitahidi kutenda haki bila
ya kuegemea upande mmoja, tunapaswa kutoa elimu kwa wafugaji wetu wafuge kisasa
na kuvuna mifugo yao, pia elimu ya kupanga matumizi bora ya ardhi kwa wakulima
na wafugaji itolewe, kwa kuweka maeneo ya wafugaji na wakulima,” alisema Kingu.
Meneja
wa utawala bora na haki za binadamu kutoka PINGO’s Forum, Emmanuel Saringe
alisema moja ya kazi inayofanywa na shirika lake ni kuhakikisha wafugaji na
wakulima nchini wanaishi kwa amani na kwamba ni muhimu pakawepo na kiungo kati
ya wafugaji na viongozi wao wa serikali ili kutatua haraka migogoro pale
inapojitokeza.
End.
Post a Comment