NZEGA, TABORA
HALMASHAURI ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuongeza viwango vya mikopo inayotolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana wilayani humo ili iweze kuendana na wakati.
Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na baadhi ya viongozi wa vikundi vya uzalishaji mali vya wanawake na vijana wilayani Nzega waliokuwa wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea wilaya hiyo kuangalia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Viongozi hao walisema pamoja na kupatiwa mikopo na halmashauri yao kutoka asilimia 10 inayotengwa kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri hiyo lakini bado viwango wanavyokopeshwa haviwawezeshi kufikia malengo waliyoyakusudia.
Walisema kutokana na ongezeko kubwa la bei za vifaa wanavyotumia katika shughuli zao wanapokopeshwa fedha kidogo vikundi vingi vinashindwa kufikia malengo vilivyojipangia hali inayochangia kwa kiasi kikubwa baadhi yao washindwe kurejesha kwa wakati mikopo wanayokopa.
“Kwa kiasi fulani tunashukuru utaratibu huu uliowekwa na halmashauri zetu wa kutupatia mikopo sisi wajasiriamali wadogo, imekuwa ikitusaidia, lakini tunachoomba ni kuongezwa kwa viwango vya mikopo,”
“Viwango vinavyotolewa ni vile vile tangu utaratibu huu ulipoanza, gharama za vifaa mbalimbali zinapanda kila siku, kwa mfano tuliomba tukopeshwe shilingi milioni tatu, lakini tukapewa milioni moja na nusu tu, sasa hizi hazitoshi kulingana na ongezeko la gharama za vifaa,” alieleza Zainabu Jumanne katibu wa kikundi cha Tuleane.
Kwa upande wao kikundi cha vijana cha ushonaji cha Pegaa mjini humo kilishauri kubadilishwa kwa utaratibu wa utoaji wa mikopo ambapo walisema badala ya kukopeshwa fedha taslimu hivi sasa wakopeshwe vitendea kazi kwa mfano vyerehani kwa wanaofanya shughuli za ushonaji.
“Kutokana na kupanda kwa bei za vifaa mbalimbali hapa nchini, tunafikiri ni wakati muafaka sasa halmashauri yetu iwe ikitoa mikopo ya vifaa kwa wale wanaohitaji, kwa mfano sisi hapa tunahitaji vyerehani vya kisasa, bei ni kubwa hatuwezi kumudu kununua kwa viwango vya mikopo hii tunayopewa,” alisema Pendo Joseph.
Halmashauri ya wilaya ya Nzega kwa kipindi cha mwaka 2007/2008 na 2012/2013 iliweza kutoa mikopo ya jumla ya shilingi 202,000,000 kwa vikundi 277 vya wanawake na shilingi 54,300,000 zilizokopeshwa kwa vikundi 91 vya vijana.
Mwisho.
Na Suleiman Abeid,
Nzega
BAADHI ya wakazi wa kata za Isanzu na Shigamba wilayani Nzega mkoa wa Tabora
wameupongeza uongozi wa halmashauri hiyo ya wilaya kwa juhudi inazozifanya katika ujenzi wa zahanati za vijiji.
Wakizungumza na waandishi wa habari mapema wiki iliyopita, wakazi hao walisema kitendo cha kukamilika kwa zahanati katika vijiji vyao kimewapunguzia tatizo la kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya makao makuu ya wilaya.
Wakazi wa kijiji cha Shila kata ya Isanzu walisema awali kabla ya kujengwa kwa zahanati katika kijiji chao walilazimika kutembea umbali wa kilometa 14 kwenda katika hospitali ya wilaya ili kupata matibabu hali ambayo ilikuwa ikiwapa shida zaidi wazee na akinamama wajawazito.
“Mpango wa kujenga zahanati kila kijiji umetusaidia sana sisi tunaoishi mbali na hospitali kubwa za serikali, awali hapa Shila tulikuwa na shida sana, hasa inapotokea mama mjamzito kupata tatizo la kujifungua ilibidi akimbizwe mjini Nzega, barabara zenyewe ni kama mnavyoziona,” alisema Daud Ngegeshi mkazi wa kitongoji cha Iyangulu.
Hata hivyo wakazi hao walishauri serikali itoe kipaumbele cha kuhakikisha zahanati hizo zinapelekewa mgao wake wa dawa kwa wakati muafaka badala ya hali ilivyo hivi sasa ambapo dawa huchelewa kupelekwa vituoni na hivyo kuondoa maana ya uwepo wa huduma hiyo kwa wanakijiji.
“Lipo tatizo la dawa kutoletwa kwa wakati katika zahanati yetu, tatizo hili husababisha turejee kule tulikotoka, maana mtu anapougua na kwenda hapo kituoni anaelezwa dawa hakuna, unakuwa huna jinsi lazima uende Nzega mjini, tunarudi kule kule kwenye shida tunachoshauri ni vizuri dawa ziletwe kwa wakati,” alisema Susana Shija.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa dawa daktari ya wa zahanati hiyo, Dkt. James Kibona alisema linachangiwa kwa kiasi kikubwa na wakala wa bohari la usambazaji dawa nchini (MSD) kutosambaza dawa hizo kwa wakati.
Hata hivyo alisema pia tatizo linalojitokeza katika ugawaji wa dawa hizo kutozingatia idadi halisi ya wakazi wanaopata huduma katika zahanati husika ambapo alitoa mfano wa zahanati yake inayohudumia vijiji vitano kwa hivi sasa kupatiwa dozi 60 ya dawa za malaria zinazotakiwa kutumika kwa miezi mitatu.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nzega, Abdulrahman Mndeme alisema tatizo la upatikanaji wa dawa kwa wakati hivi sasa linafanyiwa kazi na halmashauri yake kwa kuhakikisha zinasambazwa kwa wakati baada ya kufikishwa wilayani hapo na watu wa MSD.
Nzega
SHULE ya Msingi Nyasa II wilayani Nzega mkoa wa Tabora inakabiliwa na tatizo kubwa la utoro wa watoto hali ambayo inachangia kushuka kwa taaluma kwa watoto hao.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni shuleni hapo mwalimu mkuu wa shule hiyo, Elipendo Methusela alisema tatizo la utoro limechangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wenyewe kutokana na kutokuona umuhimu wa elimu kwa watoto wao.
Shule hiyo yenye idadi ya watoto 1,572 wakiume wakiwa 832 na wakike 740 iliyoanzishwa mwaka 1985 mbali ya kukabiliwa na tatizo la utoro pia ina uhaba mkubwa wa nyumba za kuishi walimu ambapo wengi wanalazimika kupanga nyumba zilizoko mbali na eneo la shule.
“Kutokana na shule yetu kuwa katika eneo la mjini, imechangia watoto wengi kutoroka masomo yao kila siku huku wengi wakijiingiza katika kufanya shughuli ndogo ndogo za biashara katika vituo vya biashara ikiwemo kituo kikuu cha mabasi, hili ni tatizo, kwa siku panakuwa na watoro kati 70 hadi 100,”
“Hata hivyo tunachoshukuru shule yetu haina tatizo la mimba maana hapa tuna utaratibu wa kuwapima watoto wote wa kike kila baada ya miezi mitatu, na hatujawahi kupata mtoto ye yote mwenye tatizo, alisema Methusela.
Methusela alisema katika kukabiliana na tatizo la utoro hivi sasa wameanzisha utaratibu wa kupeleka majina ya watoto wote watoro katika ofisi ya Mtendaji wa kata ambako wazazi ama walezi watoto hao huitwa na kuelezwa tatizo la utoro wa watoto wao.
Kwa upande mwingine alisema tatizo la utoro pia linachangiwa na suala la njaa ambapo alisema hapo awali shule ilipanga kuanzisha utaratibu wa uchangiaji wa fedha zitakazotumika kwa ajili ya kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni hapo hata hivyo mwitikio wa baadhi ya wazazi haukuridhisha na hivyo mpango huo ulikwama.
Hata hivyo alisema shule hiyo kwa hivi sasa ina idadi ya kutosha ya walimu shuleni hapo na kwamba mpaka sasa shule inao walimu 46 wakiume wakiwa ni watatu na 43 wote ni wa kike pakiwepo na nyumba mbili za walimu, vyumba vya madarasa vilivyopo ni 12 mahitaji halisi ni vyumba 34.
Post a Comment