Shinyanga
CHAMA Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya nchini (TUGHE) kimeiomba serikali iangalie uwezekano wa kupunguza idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kupunguza migogoro ya kugombea wanachama inayoanza kujitokeza hivi sasa.
Ombi hilo limetolewa wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Ally Kiwenge alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa idara mbalimbali za serikali kwa nyakati tofauti mkoani Shinyanga na Simiyu akiwa katika ziara ya siku 12 ya uhimizaji wafanyakazi kuwajibika kwenye maeneo yao ya kazi.
Kiwenge alisema pamoja na nia nzuri ya kuwepo kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenye lengo la kuwasaidia wafanyakazi pale wanapostaafu, lakini uwepo wa mifuko mingi hivi sasa unawachanganya wafanyakazi huku baadhi ya watendaji wake wakianza kunyang’anyana wanachama.
“Ni vizuri sasa serikali ikaangalia uwezekano wa kuwa na mifuko michache ya hifadhi ya jamii ili kupunguza vurugu za kugombea wanachama zinazofanywa na mifuko hii, baadhi wamekuwa wakiwakata wafanyakazi michango yao bila hata ya kuwashauri na kuingia makubaliano nao kwanza, sasa huu siyo utaratibu,”
“TUGHE tunashauri iwapo serikali itakubali ni vizuri tuwe na mifuko miwili tu hapa nchini, mmoja uwe kwa ajili ya watumishi wa umma na mwingine uhudumie sekta binafsi, hii itasaidia kuwaondolea kero wafanyakazi, maana wengine wanarubuniwa na kujikuta wakijiunga na mifuko isiyowahusu,” alisema Kiwenge.
Kwa upande mwingine katibu mkuu huyo alielezea kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini ambao wamekuwa wakidiriki kuwaingiza wafanyakazi katika vyama vyao kwa nguvu bila ridhaa yao na pasipo kuzingatia wanastahili kujiunga na chama kipi kutokana na kazi wanazozifanya.
Kiwenge alisema utaratibu huo umesababisha migogoro mikubwa katika baadhi ya maeneo ambapo alitoa mfano wa wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) kulazimishwa bila ridhaa yao kujiunga na chama cha Wafanyakazi wa serikali za mitaa nchini (TALGWU) kwa madai kwamba wanafanya kazi katika serikali za mitaa.
“Vyama vya wafanyakazi tusiwe chanzo cha vurugu nchini, ni muhimu tukashikamana katika kuwahudumia wafanyakazi badala ya kukaa tukigombania na kunyang’anyana wanachama, tujiepushe tusiwe asusa ya waajiri, tuache kushawishi wafanyakazi kwa kuwarubuni kujiunga na vyama visivyo wahusu, tusiwafanye kuwa sawa na mizoga inayozolewa na ovyo na mwewe,” alisema Kiwenge.
Aidha Kiwenge alisisitiza suala la vikao vya mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi kwa kuwataka waajiri kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kwa wakati kwa vile yameundwa kwa mujibu wa sheria za nchi na lengo lake kubwa ni kushauriana na mwajiri ili kuboresha ufanisi wa utendaji kazi sehemu ya kazi.
Post a Comment