SHINYANGA YATISHIWA NA KASI YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA:
APRILI MOSI ya kila mwaka ni siku maalumu kwa ajili ya upandaji wa miti katika mikoa yote hapa nchini Tanzania, ni siku mbadala baada ya ile iliyozoeleka ya Januari Mosi iliyobadilishwa kutokana na tarehe hiyo kuangukia kipindi cha kiangazi kifupi.
Uamuzi wa serikali kutenga siku maalumu kwa ajili ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini unatokana na kasi ya uharibifu mkubwa wa mazingira na kutishia uwepo wa jangwa katika baadhi ya mikoa.
Uharibifu huo wa mazingira unasababishwa na mambo mengi lakini sababu kubwa ni ukataji holela wa miti kwa ajili ya uchomaji wa mkaa ikiwa ni nishati muhimu inayotumiwa na watanzania wengi katika shughuli za kila siku kwenye familia zao.
Mkaa ni nishati muhimu ambayo ili iweze kupatikana ni lazima idadi ya miti iteketee huku maeneo inakokatwa miti hiyo hubaki wazi na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira hali ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa mvua za uhakika katika maeneo mengi.
Matumizi ya nishati ya mkaa yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku wakati hakuna juhudi zozote zinazofanyika katika kuhakikisha urejeshwaji wa mamilioni ya miti inayokatwa kila siku kwa ajili ya uchomaji wa mkaa huo.
Ukitembelea katika barabara zote kuu hautokosa kuona magunia ya mkaa yaliyorundikwa kandokando ya barabara hizo yakiwa yanasubiri wateja wa kununua ili kwenda kutumia katika familia zao, lakini hata hivyo ni vigumu kukuta kando ya marundo hayo ya magunia ya mkaa kukiwa na miti iliyoandaliwa ili watu wanunue kwa ajili ya kupanda katika makazi yao.
Laiti kauli mbiu ya kata mti mmoja panda mitatu ingepewa uzito nafikiri maeneo mengi hapa nchini yangekuwa na mandhari za kuvutia kutokana na wingi wa miti iliyopandwa.
Mkaa ni moja tu ya eneo ambalo linachangia uteketeaji wa misitu hapa nchini, lakini pia zipo sababu nyingine zinazochangia uharibifu wa misitu yetu likiwemo suala la ujenzi, ufugaji na kilimo cha zao la tumbaku zao ambalo husababisha miti mingi kukatwa ili kuweza kukaushia zao hilo.
Pamoja na kwamba serikali imekuwa ikiweka mkazo juu ya suala zima la utunzaji wa mazingira, lakini bado juhudi hasa hazijafanyika wala hakuna mkakati wowote wa kuhakikisha watu wanapanda miti kama wehu katika maeneo yao.
Ukifanya uchunguzi ‘huru’ katika maeneo mengi nchini utabaini kitu cha ajabu kabisa, kitu hiki si kingine bali ni kuona kuwa wale watanzania wenzetu waliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha misitu haihujumiwi kwa shughuli zozote zile, wao ndiyo wamekuwa mstari wa mbele katika kuendesha hujuma hizo.
Katika maeneo mengi vijiwe vya kuuzia mkaa, mbao au magogo vinamilikiwa na watumishi wa idara ya maliasili, hawa kwa kawaida hawajioneshi wazi bali wanatumia ndugu zao kuendesha biashara hiyo, hali ambayo inasababisha kuendelea kwa shughuli za uvunaji haramu wa miti hata katika misitu isiyoruhusiwa kuvunwa.
Ukitaka kupata ukweli huu jaribu kutembelea hifadhi ya pori la Kigosi kule Muyowosi wilayani Bukombe mkoani Shinyanga, utaamini ukweli kuwa serikali haiku makini na suala zima la uhifadhi wa mazingira.
Katika hifadhi hii kubwa katika mkoa wa Shinyanga, kumekuwepo na kasi kubwa ya ukataji wa miti ovyo, ufugaji wa mifugo, uchimbaji wa madini na shughuli za kilimo ambazo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria.
Shughuli hizo zimekuwa zikifanyika huku kukiwepo na watanzania wenzetu waliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha ulinzi katika hifadhi hiyo, lakini cha kusikitisha shughuli haramu zimekuwa zikiendelea kufanyika katika hifadhi hiyo kama vile hakuna watu waliokabidhiwa jukumu la kuzuia shughuli hizo.
Uongozi wa mkoa wa Shinyanga umekuwa ukifanya kila juhudi ili kuhakikisha kasi ya uharibifu wa mazingira inadhibitiwa kwa kuweka malengo mbalimbali ya upandaji wa miti, ambapo moja ya mkakati wake wa miaka ya hivi karibuni ni kila mkazi wa mkoa huo kutakiwa kupanda miti 10 kwa mwaka.
Laiti mkakati huu ungewekewa mkazo, ni wazi kuwa hali ya uoto wa asili ingeenea katika maeneo mengi, lakini hata hivyo kasi ya mwitikio wa wananchi kutekeleza mkakati huo bado ni ndogo na hata viongozi wenyewe wa serikali wameshindwa kuonesha mfano katika maeneo wanayoishi.
Kutokana na kutokuwepo mkazo wowote juu ya suala zima la utunzaji wa mazingira, maeneo mengi katika mkoa wa Shinyanga yameendelea kuathirika kutokana na uvunaji holela wa miti ambapo mbali ya miti mingi kukatwa kwa ajili ya uchomaji wa mkaa lakini pia biashara ya mbao inachangia wingi wa miti inayokatwa kila siku.
Mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa nchini ambayo inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira hali ambayo isipodhibitiwa mapema maeneo mengi katika mkoa huo yatageuka kuwa jangwa.
Mwaka 1974 wakati wa uongozi wa Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuliwahi kuandaliwa warsha ya kitaifa ya upandaji miti ambapo uzinduzi wake ulifanyika katika eneo la Kishapu, hivi sasa ni wilaya kamili eneo ambalo ni moja ya maeneo katika mkoa lenye uharibifu mkubwa wa mazingira huku baadhi ya maeneo yake hivi sasa yakikumbwa na mmomonyoko mkubwa wa ardhi.
Wilaya nyingine inayokabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazingira ni wilaya ya Maswa na sehemu ya wilaya ya Meatu ambako baadhi ya watu wameanza kukata miti iliyopandwa katika miaka ya 90 wakati wa kampeni kubwa ya upandaji miti katika wilaya hiyo iliyoongozwa na aliyekuwa mkuu wake wa wilaya Bw. Miraji Pazi.
Hata hivyo katika hali inayoashiria kutokuwepo na juhudi za makusudi za kuunusuru mkoa huo na uharibifu wa mazingira, hakuna shughuli yoyote iliyofanyika katika siku ya upandaji miti kitaifa katika mkoa huu kwa kwa mwaka huu wa 2011.
Mwaka jana sherehe za upandaji miti kitaifa zilifanyika katika mkoa huo ikiwa ni lengo la makusudi lililopangwa na viongozi wa kitaifa kutokana na hali mbaya ya uharibifu wa mazingira iliyopo katika maeneo mengi hasa wilaya Maswa, Meatu na Kishapu.
Maadhimisho ya mwaka huu kama alivyoeleza waziri wa maliasili na utalii Bw. Ezekiel Maige katika hotuba yake ya siku ya upandaji miti nchini, ni ya kipekee kutokana na Umoja wa mataifa kuutangaza kuwa ni mwaka wa kimataifa wa Misitu. Ni mwaka wa kutafakari mchango wa watu wa mataifa yote katika kuilinda misitu na kuitumia kiuendelevu.
Bw. Maige anasema huu ni mwaka ambao umepangwa kuwa wa kuhamasishana na kuendeleza uhifadhi na upandaji miti ili misitu iwanufaishe watu wa kizazi hiki na vizazi vijavyo ambapo aliwataka watanzania kuitumia siku ya Aprili Mosi kama siku rasmi ya upandaji miti na mwaka wa kimataifa wa Misitu.
Pamoja na wilaya hizo kukabiliwa na uharibifu huo wa mazingira ambao pia unachangiwa na kiasi kikubwa cha mifugo iliyopo katika mkoa wa Shinyanga, lakini wilaya nyingine inayokabiliwa na kasi ya uharibifu wa mazingira kwa hivi sasa ni wilaya ya Bukombe.
Wilaya ya Bukombe ni wilaya pekee katika mkoa wa Shinyanga iliyokuwa na misitu mikubwa ya kutisha katika miaka ya nyuma lakini kwa hivi sasa misitu hiyo ipo katika hali ya hatari ya kutoweka kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu katika misitu hiyo.
Ofisa maliasili wa mkoa wa Shinyanga, Bw. Billie Edmott anasema tatizo la uharibifu wa mazingira katika misitu ya hifadhi wilayani Bukombe kwa hivi sasa linatokana na misitu hiyo kuvamiwa na makundi ya wafugaji kutoka nchi jirani za Rwanda na Burundi.
Bw. Edmott anasema hali siyo ya kuridhisha katika misitu hiyo kutokana na kasi ya uharibifu kuongezeka siku hadi siku ikiwemo suala la ukataji miti kwa ajili ya uchomaji wa mikaa.
“Tuna tatizo kubwa kule Bukombe, maeneo mengi ya hifadhi yanaonekana katika makaratasi tu, lakini ni kinyume kabisa na hali halisi katika misitu hiyo, ukipita kwa barabarani utaamini ni misitu mikubwa iliyohifadhiwa, lakini ukiingia ndani hali ni ya kusikitisha,”
“Sisi kama serikali tumekwishaiona hali hiyo, kuna opresheni ya kitaifa ya kuwafukuza wavamizi wote katika maeneo ya hifadhi ya misitu yetu, kule Bukombe lipo tatizo la wafugaji kutoka nchi jirani, wamevamia na kuendesha shughuli za ufugaji kinyume na sheria,”
“Tayari opresheni imeanza katika mkoa wa Pwani, na baadae itaendelea katika mkoa wetu wa Shinyanga, tunataka tudhibiti hali hii ili kuweza kuinusuru misitu yetu,” anaeleza Bw. Edmott.
Anasema katika kipindi cha mwaka 2009/2010 mkoa wa Shinyanga uliweka lengo la kupanda miti ipatayo 58,538,330 lakini hata hivyo miti iliyopandwa katika kipindi hicho ni 21,915,690.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali, Dkt. Yohana Balele ni mmoja kati ya wakereketwa wa mazingira mkoani humo, amekuwa mstari wa mbele kila mara kutoa maelekezo juu ya upandaji wa miti katika kila kaya, mashule na taasisi za umma.
Mbali ya hali hiyo Dkt. Balele binafsi amekuwa akihimiza suala la utunzaji wa uoto wa asili, maarufu kwa jina la ngitili ambapo katika baadhi ya maeneo ambako wakazi wake wameitikia wito wake hali imeanza kuwa ya kupendeza hali hiyo ikijionesha katika baadhi ya maeneo ya wilaya ya Meatu.
Hata hivyo agizo la kuwataka wakazi wa mkoa huo la kila kaya kupanda miti 10 kila mwaka na miti 10,000 katika maeneo ya shule za sekondari na zile za msingi bado halijatekelezwa kikamilifu, huku shughuli za ukataji miti zikiendelea kwa kasi ya kutisha.
Kutokana na hali hii upo umuhimu mkubwa kwa viongozi wa serikali kushituka hivi sasa na kuanza kuhimiza suala la utunzaji wa mazingira katika maeneo ambayo hali inaonekana kuwa mbaya na kuhatarisha kuwepo kwa jangwa.
Viongozi wanapaswa kuhakikisha maagizo wanayotoa kupitia nyaraka mbalimbali mara nyingi hubaki ndani ya majalada ya watendaji wa wilaya, kata na vijiji pasipo utekelezaji wa aina yoyote ile, kimefika kipindi sasa wazinduke na wafuatilie kuona maagizo hayo yanafanyiwa kazi kwa vitendo, vinginevyo jangwa litauvamia mkoa huo.
Post a Comment