CCM YAJIVUNIA MTAJI WA WAPIGA KURA WALIOKO VIJIJINI.
HATIMAYE ile siku muhimu iliyokuwa ikisubiriwa sasa imewadia, ni siku ambayo vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi mkuu ndiyo itakayoamua mustakabali wa chama kipi kitapewa ridhaa ya kuwaongoza watanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo (2011 – 2015).
Kwa zaidi ya siku 70 wagombea mbalimbali wa vyama vya siasa vinavyoshikiri katika uchaguzi mkuu walikuwa wakinadi sera na Ilani za uchaguzi za vyama vyao ili kuwashawishi wapiga kura waweze kuwachagua wagombea wao katika nafasi za udiwani, ubunge na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Kutokana na hali macho na masikio ya vyama vyote hivi sasa yanaelekezwa katika kusikiliza matokeo ya kazi waliyoifanya katika kipindi hicho cha kampeni za kunadi sera zao.
Hata hivyo kwa kawaida kila mfanyabiashara anayefanya biashara yake ni lazima awe na mtaji, vipo vyama vya siasa hapa nchini hivi sasa pamoja na kuamini kuwa vimepanga vizuri karata zake za ‘turufu’ lakini bado havina mtaji wa kutosha wa wapiga kura.
Wanachama wa chama chochote kile ni mtaji, hawa ndiyo hutegemewa kukivusha chama chochote kile katika chaguzi mbalimbali, kwani siyo rahisi mtu ukafanya biashara bilaya ya kuwa na mtaji, biashara hiyo itakuwa ni ya kichekesho au ile ya ujanja ujanja kama au ya utapeli, utapeli hauhitaji mtaji wowote bali ujanja wako tu.
Wanachama ndiyo huhakikisha wanafanya chini juu katika kuhakikisha wagombea wao wanapata ushindi mkubwa na wa kishindo na hivyo hupita kila eneo wakiwanadi kwa wapiga kura ili waweze kuchaguliwa na wao ndiyo huwa wa kwanza katika kuwapigia kura.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu vyama 18 vimejitokeza kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuweka wagombea katika nafasi mbalimbali za udiwani, ubunge na urais.
Hata hivyo ni vyama saba tu kati ya vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu hapa nchini ndivyo ambavyo vimejitokeza katika kusimamisha wagombea wake katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Vyama hivyo ni CCM, CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi, TLP, UPDP na APPT-Maendeleo.
Mara baada ya uteuzi wa wagombea nafasi hiyo ya urais uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) wananchi walikuwa na shauku kubwa ya kuwasikia wagombea hao wakipita kuelezea sera na Ilani zao za uchaguzi na ni kipi kikubwa watakachowafanyia watanzania iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchini.
Lakini katika hali isiyo ya kawaida ni wagombea wachache kati ya hao saba ndiyo angalao waliweza kutembea katika mikoa yote nchini kunadi sera zao hali ambayo inatia wasiwasi kwa wagombea wengine wa nafasi hiyo nyeti kushindwa kuwafikia wapiga kura na kunadi sera zao.
Ni wazi kuwa hakuna mtanzania hata mmoja mwenye akili timamu ambaye atakubali kuipoteza kura yake kwa kumchagua mtu ambaye hakuwahi hata siku moja kuzisikia sera za chama chake na ilani yake ya uchaguzi imelenga mambo gani ya muhimu atakayowafanyia watanzania iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Itakuwa ni kichekesho kwa mgombea wa aina hiyo kupewa kura za watanzania wakati hawamuelewi wala sera za chama chake hazieleweki lakini pia tusishangae mgombea huyo mara baada ya matokeo ya kura za urais kutangazwa akajitokeza hadharani kupinga matokeo akilalamika kuibiwa kura zake au kudai hakutendewa haki.
Wagombea wanaogombea nafasi ya urais ni pamoja na mgombea anayetetea nafasi hiyo, kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mara nyingine tena anaomba aendelee kupewa ridhaa ya kuongoza nchi ili aweze kutekeleza na kukamilisha maendeleo mengi ambayo tayari chama chake kimeisha yaanzisha.
Wagombea wengine katika kinyang’anyiro hicho cha urais ni pamoja na Dkt. Wilbroad Slaa (CHADEMA), Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF), Bw. Muttamwega Mgahywa (TLP), Bw. Peter Mziray (APPT-Maendeleo), Bw. Hashim Rungwe (NCCR-Mageuzi) na Bw. Fahmi Nasoro Dovutwa (UPDP).
Katika kuhakikisha kila mgombea anatendewa haki sawa, Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini (NEC) ilitoa siku 70 kwa ajili ya kampeni za kunadi sera za vyama vya wagombea kwa wapiga kura, hatua ambayo inatoa fursa kwa wapiga kura kuwa na uamuzi ni mgombea yupi anayestahili kupewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Hata hivyo katika hali ambayo haikutarajiwa na watanzania wengi baadhi ya wagombea wameshindwa kuwafikia wapiga kura kwa ajili ya kutangaza sera na ilani za vyama vyao, wengi wameonekana kupiga kampeni zao katika jiji la Dar es salaam na mikoa jirani ya jiji hilo kitu ambacho kitasababisha watanzania washindwe kuwapigia kura.
Lakini baadhi ya wagombea walijitahidi katika kuhakikisha wanawafikia wapiga kura katika mikoa yote nchini ambapo ni vyama vitatu tu ndvyo vilivyomudu hatua hiyo, ambavyo ni CCM, CHADEMA na CUF.
Hivi ndivyo vyama vinavyotarajiwa kutoa ushindani mkubwa katika nafasi hiyo ya urais, kutokana na jinsi ambavyo viliweza kutembea katika maeneo mengi nchini kwa lengo la kuwafikia wananchi na kunadi sera zao.
Kila mgombea kati ya wagombea wa vyama hivi vitatu katika kipindi hiki cha kampeni alijitahidi kuzinadi sera za chama chake pamoja na ilani yake ya uchaguzi kwa kila hali kwa lengo la kuwashawishi wapiga kura waweze kuwachagua ifikapo Oktoba 31, mwaka huu.
Lakini pamoja na mikakati yote hiyo ya kampeni, kila chama kimekuwa kikijitahidi kuhakikisha hakipotezi mtaji wa wanachama wake kilionao na vingine vinadiriki kushawishi na kuwarubuni wanachama wa vyama vingine kuhamia katika vyama vyao, lengo ikiwa ni kuongeza idadi ya wanachama na pia kuongeza idadi ya kura zao.
Pamoja na utafiti wa Taasisi mbalimbali uliokuwa ukifanyika kwa kutafuta maoni ya wananchi kuwa ni mgombea yupi anayestahili kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kuonesha kuongoza kwa baadhi ya wagombea wa vyama lakini ukweli ni kwamba kila chama kinategemea zaidi mtaji wa wanachama wake kilionao.
Tafiti za taasisi mbili za REDET na SYNOVET zimeonesha kuwa mgombea wa CCM alikuwa ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na kura za maoni zilizoendeshwa na taasisi hizo huku taasisi ya Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB) ikimtaja mgombea wa CHADEMA Dkt. Wilbroad Slaa ndiye aliyekuwa akiongoza.
Matokeo ya kura hizi za maoni yanaweza kuwa na ukweli wa aina fulani kutokana na jinsi ambavyo CCM ilivyoweza kuweka mtandao wake hadi katika ngazi ya chini kabisa kijijini ambako kuna wajumbe wa mashina, hawa mara nyingi wamezoeleka kuitwa mabalozi wa nyumba kumi.
Mtandao wa uongozi wa Chama cha Mapinduzi ni mpana zaidi ikilinganishwa na vyama vingine vyote vya siasa hapa nchini hali ambayo inakipa nafasi kubwa chama hicho kuweza kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wowote utakaofanyika hapa nchini.
Katika kipindi hiki cha kampeni, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ameweza kutembelea mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani, na si katika makao makuu ya mikoa peke yake bali hadi katika maeneo ya vijijini ambako wagombea wa vyama vingine hawakuweza kufika.
Maeneo hayo ya vijijini kuna watanzania wengi sana , na hawa kwa kipindi chote cha kampeni wameweza kulishwa imani ya Chama cha Mapinduzi, wameelezwa nini chama hicho kimeweza kufanya ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita na nini kitafanya katika miaka mingine mitano ijayo iwapo kitachaguliwa tena.
Ni wazi kuwa mtanzania aliyeko katika maeneo hayo siyo rahisi kwake kuna wagombea wengine wa nafasi hiyo ya urais mbali ya Rais Kikwete wa CCM, nani kawashitua kama kuna wengine maana hawajawaona katika maeneo yao , ni wazi chaguo lao litakuwa ni CCM.
Hiyo ni moja ya faida mtaji wa wanachama hadi katika ngazi ya kijiji hawa piga ua garagaza wanachofahamu mtu anayestahili kuchaguliwa ni wagombea wa CCM iwe ni mgombea udiwani au ubunge maana ndiyo waliokuwa wakiwaona katika kipindi cha kampeni wakipita kuwaomba kura.
Faida ya pili wanayoipata wagombea wa CCM ya kuwa na mtaji wa wanachama katika ngazi ya kijijini, ni kuwa na mtandao wa uongozi hadi katika maeneo hayo, hawa ni wajumbe wa mashina, viongozi wa matawi na wale wa ngazi ya kata, wote hawa ni mtaji na kila mtu huwa anakabidhiwa jukumu la kuhakikisha anawavusha wagombea wa chama hicho iwe kwa nafasi ya udiwani, ubunge na urais.
Siku hiyo ya uchaguzi kila balozi anatakiwa kuhakikisha wanachama wake wote wasiopungua kumi wanakwenda katika kituo cha kupigia kura na wanapiga kura zao kuwachagua wagombea wao, hapa ndipo vyama vingine vya upinzani vinapopigwa bao la kisigino, unafikiri kama havina mtandao huo, nani atakayewahamasisha wananchi wawapigie kura wagombea wao?
Lakini pia pamoja na hali hiyo ni Chama cha Mapinduzi pekee ndicho angalao kinafahamu idadi ya wanachama wake kilionao nchini kote ambapo mara kwa mara kimekuwa kikitamba na kutamka kwamba kina zaidi ya wanachama milioni nne nchini na hii inatokana na orodha kinayoipata kutoka katika matawi yake mijini na vijijini.
Kwa vyovyote vile huo ni mtaji tosha, kati ya wanachama hao robo tatu yao tu kila mmoja siku ya kupiga kura iwapo atakwenda katika kituo cha kupigia kura na watu wawili ni wazi CCM mgombea urais wa CCM atakuwa na uwezekano wa kupata kura zaidi ya milioni tisa, achilia mbali kura nyingine za wapenzi na wakereketwa wengine ambao si wana CCM.
Kutokana na hali hiyo tambo za wana CCM kuwa wataibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu si za kupuuza, tayari wenzetu hawa waliishawekeza. Ni vizuri sasa kwa vyama vingine vya siasa hapa nchini na vyenyewe vikajifunza mfumo huu wa kuwa na wanachama hadi vijijini pamoja na kupanua mtandao wake wa uongozi hadi katika ngazi za chini.
Watanzania hawana tatizo la kukiunga mkono chama chochote cha siasa ili mradi tu wameelezwe sera za chama hicho na iwapo zitakuwa nzuri na zinazokubalika wanaweza kujiunga, mbona katika maeneo ya mijini inawezekana.
Tumeona katika mikutano mingi ya kampeni iliyofanyika maeneo ya mijini wagombea wa vyama vya upinzani hasa CHADEMA na CUF wamekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi sasa vipi washindwe kuwaendea na watanzania wengine walioko vijijini, ni wazi safari bado ndefu ili kuweza kuiondoa CCM madarakani.
Post a Comment