Shinyanga
MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Shinyanga mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Bw. Steven Masele jana alifunga kampeni zake katika kata za Kambarage na Lubaga kwa kukanusha uvumi uliodai kuwa yeye ni mtu wa kuja na si mzaliwa wa Shinyanga.
Bw. Masele alilazimika kukanusha uvumi uliokuwa ukisambazwa na mpinzani wake anayegombea pia ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya chama cha CHADEMA, Bw. Philipo Shelembi ambaye katika mikutano yake ya kampeni amekuwa akiwataka wakazi wa Shinyanga kutomchagua mgombea wa CCM kwa vile ni mtu wa kuja.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Masele hiyo jana alilazimika kuelezea wasifu wake tangu alipozaliwa ambapo alitoa ushahidi kuwa babu yake ndiye aliyekuwa msukuma wa kwanza kujenga nyumba ya ghorofa katika mji wa Shinyanga.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida, mgombea huyo wa CCM alijikuta akimvurumishia makombora mgombea wa CHADEMA baada ya kuwataka wakazi wa Shinyanga kutomchagua kutokana na kutokuwa mwaminifu na pia ana kesi mbili mahakamani.
Aidha alisema mgombea huyo wa CHADEMA hivi sasa anatafutwa na mmoja wa waliokuwa waajiri wake mkoani Kagera ambako alikimbia kutokana na tuhuma za upotevu wa maziwa hali ambayo inamfanya hivi sasa aishi kwa kufuga ndevu nyingi na kuvaa miwani myeusi akikwepa kufahamika.
Mbali ya hali hiyo pia alisema mgombea huyo wa CHADEMA hafai kuchaguliwa kuwa mbunge kwa vile hana elimu ya kutosha ambapo alitoa ofa iwapo atashinda na kuwa mbunge atajitolea kumshomesha kuanzia darasa la tano mpaka afikie kiwango cha kwenda kusomea chuo cha sanaa Bagamoyo.
Alisema mgombea huyo wa CHADEMA anaonekana na uwezo mkubwa wa kuwa msanii mzuri hivyo iwapo atatapatiwa elimu zaidi ataweza hapo baadae kumtumika katika kufundisha vikundi vya ngoma za akina mama na vijana.
“Ndugu zangu leo napenda niwathibitishie kuwa mimi ni mzaliwa wa Shinyanga, na babu yangu ndiye aliyekuwa msukuma wa kwanza kujenga ghorofa hapa Shinyanga, kutoonekana kwangu kunatokana na kuwa masomoni kwa miaka kumi,”
“Hivyo wengi wenu hamnifahamu, na nilipomaliza masomo niliwahi kufanya kazi na Rais Kikwete alipokuwa wizara ya mambo ya ndani, lakini napenda niwathibitishie kuwa mimi ni mzawa wa Shinyanga na siyo mluguru kama inavyodaiwa na wapinzani wangu, niwaulize mliishawahi kuona mluguru mrefu?” alihoji Bw. Masele.
Kwa upande mwingine mgombea huyo alisema iwapo atachaguliwa atahakikisha anapigania haki na maslahi ya wakazi wa Shinyanga bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa, dini, rangi au kabila na kuhakikisha akina mama na vijana wanawezeshwa katika shughuli zao kwa kupata mikopo kutoka Manispaa.
Alisema akiwa mbunge pia atakuwa diwani hivyo atahakikisha kila mwaka Manispaa inatenga fungu la fedha kwa ajili ya kuwawezesha akina mama na vijana kuweza kupata mikopo ya kuendeshea biashara zao ndogo ndogo.
Pia alisema akiwa mbunge atahakikisha barabara za mji wa Shinyanga zinajengwa kwa kiwango cha lami ambapo alizitaja barabara kadhaa kuwa tayari mipango imo mbioni kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Hata hivyo barabara zote zilizotajwa na mgombea huyo ni zile ambazo tayari mbunge aliyemaliza muda wake, Dkt. Charles Mlingwa alitangaza rasmi kuwa fedha yake iliishapatikana na ujenzi wake unatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa fedha.
Post a Comment