Shinyanga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewashutumu vikali wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo mgombea ubunge katika jimbo la Maswa Magharibi mkoani Shinyanga, Bw. John Shibuda kutokana na vurugu walizozifanya na kusababisha kifo cha mmoja wa wanachama wa CCM.

Shutuma hizo zimetolewa na Katibu mkuu wa CCM wa Taifa, Bw. Yusuf Makamba alipokuwa akihutubia mkutano wa wanachama wa CCM uliofanyika juzi katika uwanja wa michezo wa Kambarage mjini Shinyanga.

Bw. Makamba alisema tukio la kifo cha mwanachama wa CCM, Bw. Steven Kwilasa (26) kimeonesha wazi kuwa wafuasi wa CHADEMA wameanza kutekeleza dhamira yao ya kumwaga damu waliyoitangaza hapo awali.

Hata hivyo Bw. Makamba aliwataka wana CCM wasijaribu kujibu kisasi kwa vile CCM ni chama cha amani na utulivu na hivyo iwapo wangejibu mapigo ni wazi wangeharibu historia ya Chama.

“Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi, na viongozi wake wote waandamizi, CCM inatoa pole sana kwa familia ya marehemu Steven, tumesikitishwa sana na tukio hilo, ni wazi hawa wenzetu wa CHADEMA wameanza kutekeleza dhamira yao waliyokwisha itangaza tangu hapo awali,”

“CHADEMA waliahidi kumwaga damu, na kweli tayari damu imemwagika, vijana wetu wa CCM ilikuwa wajibu mapigo, na shida yao kubwa ilikuwa ni mgombea wa CHADEMA, Bw. Shibuda, lakini tumewakataza, tumesema njia nzuri ya kumwadhibu yeye (Shibuda), Slaa, Mbowe na wagombea wote wa CHADEMA ni sanduku la kura,”

“Oktoba 31, mwaka huu ndiyo siku nzuri ya kulipa kisasi kwa hawa watu, ushahidi wa kimazingira unaonesha wazi wao ndiyo walioua, ni malimbukeni na wauaji, waadhibiwe kwa kunyimwa kura waondoke patupu,” alieleza Bw. Makamba.

Bw. Makamba aliwataka wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu kwa kuhakikisha hawawi chanzo cha vurugu na kwamba wahakikishe siku ya uchaguzi wanawachagua wagombea wote wa CCM ili chama kipate ushindi wa kishindo.

Juzi wanachama wa CCM na wale wa CHADEMA walifanya vurugu kubwa zilizosababisha kutokea mapigano kati yao ambapo mmoja wa wanachama wa CCM aliyekuwa dereva wa gari lililokuwa limewabeba wafuasi wa CCM, Bw. Steven Kwilasa mkazi wa Malampaka alipigwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali na kusababisha kifo chake.

Watu 12 akiwemo mgombea wa CHADEMA, Bw. John Shibuda walikamatwa na polisi na kuwekwa ndani wakihojiwa kuhusiana na tukio hilo ambapo inadaiwa CHADEMA ndiyo walikuwa chanzo cha vurugu hizo.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top