Kwimba, Mwanza
MKUU wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Bw. Christian Kangoye anatuhumiwa kuendelea kukaidi hukumu iliyotolewa na Baraza la Ardhi katika mgogoro wa ardhi kati ya familia ya Bw. Salu Bucheyeki na serikali ya kijiji cha Buyogo wilayani Kwimba.
Hatua ya mkuu huyo wa wilaya inafuatia kitendo chake cha kuagiza kukamatwa na kuwekwa ndani siku nne bila kufunguliwa mashitaka yoyote kwa familia ya Bw. Bucheyeki wakidaiwa kuharibu hifadhi ya kijiji katika eneo ambalo tayari Baraza la ardhi liliishatoa hukumu yake kuwa ni mali ya familia hiyo.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida mkuu huyo wa wilaya aliwatimua ofisini kwake waandishi wa habari waliokuwa wamekwenda kupata ufafanuzi juu ya kitendo chake cha kukataa kutii na kuheshimu hukumu iliyotolewa na chombo halali cha kisheria katika migogoro yote ya ardhi hapa nchini.
Kufuatia kitendo cha kukamatwa kwa wanafamilia hao, tayari familia hiyo imeandika barua kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete na waziri mkuu Bw. Mizengo Pinda wakiomba msaada wao ili mkuu huyo wa wilaya aache kuwasumbua na kuzuia matumizi ya ardhi ambayo Baraza la Ardhi liliishawaruhusu waitumie baada ya kushinda kesi.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na msemaji wa familia hiyo, Bw. Bucheyeki, mkuu huyo wa wilaya mnamo Oktoba 16, mwaka huu aliagiza kukamatwa kwa Bw. Lucas Jihulya na mkewe Bi. Ester Bucheyeki ambao walikuwa wakiandaa mashamba katika eneo lao hilo la ardhi ya ukoo.
Bw. Bucheyeki alisema mkuu huyo alitoa agizo la kukamatwa kwa nduguze hao kwa madai kuwa walikuwa wamevamia eneo la hifadhi ya kijiji cha Buyogo na kukata miti huku wakiharibu mazingira kwa makusudi.
Akifafanua alisema, Oktoba 16, mwaka huu mkuu huyo wa wilaya alifika katika kijiji cha Buyogo mnamo saa sita mchana akiwa na magari mawili, moja likitumiwa na yeye mwenyewe na jingine lilikuwa limebeba askari polisi wengi kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na serikali ya kijiji.
“Wakati mkutano ukiendelea, Bw. Kangoye aliuliza iwapo katika mkutano huo walikuwepo Bw. Lucas na mkewe Bi. Ester, alijibiwa kuwa wapo, papo hapo aliagiza wawekwe chini ya ulinzi na polisi waliwakamata na kuwapakia ndani ya gari walilokuwa nalo, na mkutano ulipofungwa waliondoka nao hadi Ngudu, ambako waliwekwa mahabusu,” alieleza Bw. Bucheyeki.
Hata hivyo alisema madai ya mkuu huyo wa wilaya kuwa eneo hilo la ardhi ni mali ya serikali ya kijiji na kwamba kijiji kiliamua kulitenga kama eneo la hifadhi ya mazingira si ya kweli baada ya uongozi wa serikali ya kijiji kushindwa katika kesi ya madai namba 57 ya mwaka 2009 iliyofunguliwa katika Baraza la ardhi la wilaya ya Mwanza.
“Kwa kweli sisi wanafamilia tumesikitishwa sana na kitendo cha mkuu huyu wa wilaya, ameshindwa kabisa kuheshimu hukumu ya Baraza la Ardhi, baada ya hukumu hiyo iliyotolewa katika kesi yetu ya madai namba 57 ya mwaka 2009 mnamo Januari, 15 mwaka huu kutupa haki ya kumiliki kihalali eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 114,”
“Awali mkuu huyo mnamo Juni 25, mwaka huu alifika kijijini kwetu na kuitisha mkutano wa hadhara ambapo katika hali isiyokuwa ya kawaida alitangaza kutengua amri hiyo ya Baraza la Ardhi kitu ambacho sisi hatukuafiki na hivyo kuendelea kulitumia eneo hilo kwa vile tulikuwa tumeshinda kesi,” alieleza Bw. Bucheyeki.
Alisema baada ya kumbana zaidi mkuu huyo wa wilaya alidai alizuia matumizi ya eneo hilo kwa vile anatarajia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo maelezo ambayo yalitushangaza kutokana na madai yetu ya msingi kutokuwa kati yetu na yeye bali ni serikali ya kijiji cha Buyogo ambayo ndiyo iliyopaswa kukata rufaa.
“Kwa kweli tulishangazwa na madai ya mkuu wa wilaya kutaka kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, kwani kisheria waliopaswa kukata rufaa ni watu ambao tulikuwa tumewashitaki, kijiji mpaka hivi leo hakina mpango wowote na suala la kukata rufaa, hata muda wa rufaa uliishapita, lakini mkuu bado ametung’ang’ania,” alieleza Bw. Bucheyeki.
Alisema kutokana na manyanyaso hayo ya Bw. Kangoye hivi sasa wamemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete pamoja na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda katika hali ya kutafuta msaada wa kuokolewa na usumbufu wa mara kwa mara wanaoupata wanafamilia kwa kuwekwa ndani pasipo kufunguliwa mashitaka.
Post a Comment