“JUNI 5, 2010 ni siku ambayo haitasahaulika kwangu, ni siku ambayo niliamini kuwa ule msemo wa mtu kulala masikini na asubuhi kuamka tajiri, ni usemi wenye ukweli, na unawatokea watu,”

“Ni siku ambayo kwa mara yangu ya kwanza niliandika historia katika nchi yetu baada ya kutangazwa kuwa ni mshindi katika shindano la utunzaji wa mazingira nchini, kwa kweli sikuamini masikio yangu pale nilipokuwa nimeketi,” ndivyo anavyoanza kueleza Bw. Mussa Nyamve Sambe mkazi wa kijiji cha Mwambengwa wilayani Meatu mkoani Shinyanga.

Bw. Sambe anasema alizaliwa katika kijiji cha Zebeya wilayani Maswa mkoani Shinyanga mwaka 1961 akiwa ni mtoto wa sita katika familia yao ya Mzee Nyamve Sambe ambapo mwaka 1974 alipelekwa shule na kuanza kusoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mwanyahina na kufanikiwa kumaliza darasa la saba mwaka 1980.

“Nilipomaliza darasa la saba sikufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uhaba wa shule za sekondari wakati huo ilikuwa ni vigumu sana kupata nafasi na hivyo nililazimika kubaki nyumbani nikisaidiana na wazazi wangu katika shughuli za kilimo,” anaeleza Bw. Sambe na kuongeza,

“Mwaka 1982 nilihamasika na suala la utunzaji wa mazingira ambapo pale nyumbani nilipanda miti miwili tu mmoja wa mpera na mwingine aina ya Mhi’gu, hii niliitunza mpaka ikakua vizuri na hapo nilihamasika zaidi na wazo la kuendelea kupanda miti mingi kadri nitakavyoweza ambapo mwaka uliofuata nilipanda miti 25, ikiwemo ya matunda na mingine ya asili,” anaeleza.

Anasema kutokana na kustawi kwa miti hiyo japo katika mwaka huo miti miwili ilikufa kutokana na kushambuliwa na wadudu, alipata hamasa zaidi na kuamua kutafuta eneo lake mwenyewe ambalo ataweza kupanda miti mingi kwa lengo la kutunza mazingira katika maeneo yao ya kijiji chao.

“Unafahamu eneo letu tulilokuwa tukiishi lilikuwa na ukame wa kutisha, lakini nilipochunguza nilibaini kuwa hali hiyo ilisababishwa na uharibifu wa mazingira uliofanywa na wazee wetu miaka ya nyuma wakidai kupambana na wadudu aina ya mbungo waliokuwa wakishambulia mifugo yao, hivyo walikata miti ovyo,” anaeleza Bw. Sambe.

Mkereketwa huyo wa mazingira anasema, alifanikiwa kupata eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 80 kijijini lililokuwa halina miti ambalo hata hivyo katikati yake kunapita mto mkubwa uitwao mto Mwanhuzi, hivyo alianza shughuli za kuliandaa eneo hilo kwa ajili ya kupanda miti mbalimbali kwa lengo la kuligeuza kuwa eneo la hifadhi na la mfano katika kijiji chao.

“Nilipoanza shughuli za kupanda miti sikuwa na wazo kuwa ipo siku moja nitatembelewa na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya, mkoa na kitaifa pia na watu wa aina mbalimbali kutoka taasisi zinazojishughulisha na utunzaji wa mazingira ili kuja kuangalia eneo hili, lakini leo hii nashangaa hata mawaziri wengi wa serikali wamenitembelea,” anaeleza.

Bw. Sambe anasema mwanzoni mwa mwaka 2010 aliweza kusikia tangazo redioni likiwataka wananchi ambao ni wakareketwa wa mazingira kushiriki katika shindano la Tuzo ya Rais juu ya utunzaji wa mazingira nchini, ambapo alihamasika na kuamua kushiriki shindano hilo ambapo alichukua fomu na baada ya kuzijaza alizirejesha katika ofisi za maliasili wilayani Meatu.

Anasema, wakati akiwa anasubiri matokeo ya fomu hizo, alitembelewa na kundi la viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya waliofika kukagua eneo lake hilo analoshughulika katika uhifadhi wa mazingira, ambapo walikagua eneo lote na kisha waliondoka wakimtaka asubiri matokeo baada ya kuwa ni mmoja kati ya watu waliojitokeza kushiriki shindano hilo.

“Mbali ya kutembelewa na viongozi hao wa ngazi ya wilaya, lakini pia lilifuata kundi la pili lililokuwa na timu ya viongozi wa ngazi ya mkoa na wao niliwatembeza katika eneo langu lote ambapo waliweza kujionea jinsi ambavyo nimeweza kubuni mbinu mbalimbali katika utunzaji wa mazingira,”

“Baada ya kuondoka kwa timu ya mkoa, muda mfupi likafuata kundi la ngazi ya kitaifa, hawa nao niliwatembeza katika eneo langu lote wakalikagua na wao wakajionea hali halisi ilivyo, na kwa kweli hata hawa nao walipoondoka hawakunieleza jambo lolote juu ya kile walichokiona,” anaeleza Bw. Sambe.

Bw. Sambe anaendelea kueleza, “Alhamisi ya Juni 3, mwaka 2010 nilishangaa kupigiwa simu kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya ya Meatu ikinieleza kuwa natakiwa kwenda Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya sherehe ya Siku ya mazingira duniani,”

“Sikuamini masikio yangu nilipoelezwa kuwa mimi ni mshindi katika shindano la utunzaji wa mazingira kiwilaya, kimkoa na kitaifa kwa ngazi ya kaya katika utunzaji wa mazingira nchini, na kwamba natakiwa kwenda kukabidhiwa zawadi yangu na Rais Jakaya Kikwete,”

“Nilifurahi sana japo kidogo nilipatwa na wasiwasi, ilibidi nifunge safari ya ghafla kuelekea mkoani Dodoma, nilipofika huko nilikuwa naamini kuwa ni mshindi katika maeneo matatu niliyoelezwa hapo awali,”

“Nilipokea zawadi ya kitaifa ya shilingi milioni mbili na cheti, lakini ilipokuja zamu ya kutangazwa kwa mshindi wa jumla katika maeneo yote yaliyoshindaniwa, nilipatwa na mshituko mwingine baada ya kusikia jina langu likitajwa tena kwa mara ya pili,” anaeleza.

Bw. Sambe anasema alitangazwa kuwa mshindi wa jumla kitaifa wa shindano hilo baada ya kukidhi vigezo muhimu vilivyokuwa vikihitajika ili kumwezesha mtu kutangazwa kuwa mshindi wa jumla, na kwamba moja ya vigezo hivyo ilikuwa ni kuonesha ubunifu wa ziada ambapo katika ushindi huo alipata zawadi ya ngao na shilingi milioni 10.

Anasema kwa upande wake aliweza kuonesha ubunifu wa ziada kutokana na kugundua utengenezaji wa mbolea ya juice ambayo inatengenezwa kutokana na mchanganyiko wa kinyesi cha kuku na sungura, na kwamba mbolea hiyo ilibainika kuwa bora katika kukuzia mimea kuliko mbolea nyingine.

Pia vigezo vingine vilikuwa ni kuwa na choo bora ambapo pia aliweza kuonesha ubunifu wa kutengeneza eneo la kuhifadhia taka ngumu ambazo huwa haziozi na hivyo zikisambaa au kuchomwa huchangia uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa.

Anasema amekuwa na utaratibu wa kuwasiliana na watu Halmashauri ya wilaya pale taka hizo zinapojaa wazichukue na kwenda kuzitupa katika maghuba yao badala ya kuzichimbia chini au kuzichoma moto.

Kwa ujumla Bw. Sambe anasema utunzaji wake wa mazingira umeweza kuwasaidia wanakijiji wenzake kuiga mfano wake ambapo mpaka hivi sasa tayari kuna kaya zipatazo 360 ambazo zimeanza kutunza mazingira na kusababisha maeneo yao kupata mvua za uhakika kila mwaka.

Anasema kutokana na mafanikio hayo hivi sasa amekuwa akitoa mafunzo ya utunzaji wa mazingira katika shule saba za msingi wilayani Meatu anazozitaja kuwa ni pamoja na ile ya kijijini kwake Mwambengwa, shule ya msingi Ikigijo, Buhangija, Nkoma, Itaba, Mshikamano, Sapa na Mwanhuzi.

“Suala la uhifadhi wa mazingira ni kitu muhimu sana, pamoja na kwamba nilianza na miti miwili, lakini leo hii eneo langu lina zaidi ya miti 200,000 ya kupanda na mingine ya asili, naamini iwapo jamii ikihamasika katika suala hili!! mazingira yetu yataboreka, maeneo mengi mkoani Shinyanga huko nyuma yaliathirika sana na baadhi yapo katika hatari ya kugeuka jangwa, sasa lazima tubadilike,”

“Binafsi kupitia uhifadhi huu wa mazingira nimeweza kuisadia jamii inayonizunguka kwa kuwapatia matunda ninayovuna katika miti yangu, sina kawaida ya kuuza matunda, ninagawa bure ili kuihamasisha jamii ione umuhimu wa kupanda miti, na pia katika matatizo ya misiba nimekuwa ninasaidia kuni bure,”

“Wito wangu kwa jamii ninawataka wabadili tabia, badala ya kuharibu mazingira sasa wageukie utunzaji wa mazingira ili yawatunze, mimi kupitia kuni na nyasi ninazouza kwa wafugaji kwa mwaka napata zaidi ya shilingi milioni tatu, sasa kama ningeharibu mazingira faida hii nisingeipata,” anaeleza Bw. Sambe.

Mkereketwa huyo wa mazingira anamalizia simulizi yake kwa kuwaomba viongozi wa serikali wampatie ushirikiano zaidi ili aweze kuendeleza ndoto yake hiyo muhimu katika suala zima la utunzaji wa mazingira kwani ni kupitia utunzaji wa mazingira pekee ndipo jamii inapoweza kupata hewa safi ya Oxygen.

Mwisho.


Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top