MAHAKAMA ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemhukumu Mwenyekiti wa Baraza la ardhi na Nyumba katika wilaya hiyo, Mdimi Ilanga kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh Milioni 1.4 baada ya kupatikana na hatia na makosa mawili ya  kuomba na kupokea rushwa.
 
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Fredrick Lukuna alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka.
 
Alisema kuwa anamtia hatia mshitakiwa baada ya kujiridhisha kupitia mashahidi walioletwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuthibitisha kuwa alitenda makosa hayo ya kuomba na kupokea rushwa kiasi cha Sh 400,000 kutoka kwa Paul Shigela.
 
Kabla ya hukumu hiyo Mwendesha mashitaka wa Takukuru,Mzalendo Widege aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa serikali waliopewa dhamana ya kusimamia haki kujiingiza katika vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kwa lengo la kupindisha haki.
 
Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashitaka wa Takukuru,Widege kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo kutoka kwa Paul Shigela ambaye alikuwa na shauri  la madai  Namba 103 la Mwaka 2016 katika baraza hilo.
 
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa aliomba kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Shigela ili aweze kumpatia upendeleo wa maamuzi katika shauri lake hilo lililokuwa mbele yake.
 
Alizidi kuieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo mawili  januari 27 mwaka huu ndani ya ofisi ya baraza hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kwa kosa la kuomba rushwa  na Kifungu cha 15 (1) (a) Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kwa kosa la kupokea rushwa .
 
Katika kesi hiyo Na 14 ya Mwaka  2017 mara ya kwanza baada ya mshitakiwa kusomewa shitaka hilo  alikana kosa linalomkabili na kuiomba mahakama kufuta kesi inayomkabili kwa kile alichoeleza  kuwa kukiukwa kwa kanuni za kukamatwa na kuwekwa mahabusu jambo ambalo mahakama halikulikubali.


Kwa hisani ya bloger.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top