BAADHI ya wazazi nchini
wametajwa kuwa chanzo cha kuporomoka kwa maadili kwa watoto wao kutokana na
kutowalea kimaadili tangu wakiwa watoto wadogo.
Hali hiyo imebainishwa na Sheikh wa mkoa wa Shinyanga, Ismail Habib Makusanya
alipokuwa akitoa nasaha zake katika mashindano ya kusoma na kuhifadhi Qur – an yaliyoshirikisha
wanafunzi zaidi ya 70 kutoka madrasa za mjini Shinyanga.
Sheikh Makusanya
alisema kuporomoka kwa maadili miongoni mwa vijana wengi hapa nchini
kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi ama walezi ambao hawana tabia ya
kuwalea watoto wao kimaadili tangu wakiwa na umri mdogo.
Alisema iwapo wazazi na
walezi wote watajenga utamaduni wa kuwalea watoto wao kimaadili na kuwafundisha
dini kwa ufasaha, hali ya kuporomoka kwa maadili kwa vijana wengi hapa nchini itapungua kwa
kiasi kikubwa tofauti ilivyo hivi sasa katika maeneo mengi.
Aliendelea kueleza
kuwa, kukosekana kwa maadili miongoni mwa vijana ndiyo chanzo cha matukio mengi ya
kiuhalifu ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, vitendo vya unyang’anyi, ukahaba
na ushoga vinavyofanywa na vijana wengi wakiamini ndiyo ujana na maisha ya
kisasa.
“Ndugu zangu lazima
turejee kwenye mafundisho ya mwenyezi mungu na mtume wetu Muhammad (S.A.W) juu
ya malezi ya watoto wetu, tuwajengee mazingira mazuri tangu wakiwa na umri
mdogo, tuwalee kimaadili ya dini, tukifanya hivyo ni wazi hawataweza kufanya
vitendo vichafu watakapokuwa watu wazima,”
“Hivi sasa serikali
inahangaika kupambana na watumiaji na wauzaji wa madawa ya kulevya, ukiangalia
wanaofanya mambo haya ni hawahawa watoto wetu wenyewe, tujiulize
walijifunzia wapi mambo haya? ni wazi hawakulelewa katika tabia na maadili
mema, hivyo hawaoni ubaya wowote kujihusisha na vitendo hivyo,” alieleza.
Sheikh
Makusanya alitoa
wito kwa wazazi na walezi wote wa kiislamu hapa nchini kumrejea mwenyezi
mungu kwa kufanya
vitendo vizuri kama mafundisho ya mwenyezi mungu yanavyoelekeza, ambavyo
vitawaepusha na mambo machafu pamoja na kuwafundishia watoto wao
tabia na maadili mema.
Alifafanua kuwa iwapo jamii nchini itajengwa katika misingi ya maadili mema hata serikali kwa upande wake haitokuwa na kazi
kubwa ya kupambana na wavutaji au wauzaji wa madawa ya kulevya, wahalifu au
makahaba kwa vile hapatakuwa na watu wanaofanya vitendo hivyo.
Kwa upande wake mgeni
rasmi katika mashindano hayo, Sheikh Hilal Soud ambaye ni mwenyekiti wa Kamati
ya Istiqama mkoani Shinyanga alitoa wito kwa wazazi wa kiislamu kuwapeleka
shule watoto wao ili waweze kupata elimu badala ya kuwaficha au kuwapa kazi
ndogondogo ambazo hazitowasaidia hapo baadae.
Sheikh Hilal alisema
suala la elimu ni muhimu katika ulimwengu wa hivi sasa na kwamba bila elimu
hakuna jambo lolote la muhimu ambalo mtu anaweza kulifanya iwe upande wa dini
au kidunia na hata mwenyezi mungu amesisitiza sana juu ya umuhimu wa watu kusoma.
“Elimu ndiyo urithi
usiofilisika, na kwa sisi waumini wa kiislamu suala la kutafuta elimu ni moja
ya mambo yaliyofalidhiwa juu yetu, hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu
kuhakikisha anawapatia watoto wake elimu zote mbili, ya dunia na ile ya akhera,”
“Tuache tabia ya
kuwaficha majumbani au kuwapa vishughuli visivyo kuwa na faida ya
baadae kwao, tuwapeleke shule wasome elimu ya dini na ya dunia kwa kadri ya
uwezo wao, tuache kuridhika na elimu ya msingi tu, tuwakazanie, vinginevyo
watakuwa na maisha magumu hapo baadae,” alieleza Sheikh Hilal.
Katika mashindano hayo
mwanafunzi, Abdulaziz Mussa kutoka Madrasatul Farouq ya majengo Shinyanga
aliibuka mshindi wa kwanza katika washindani waliohifadhi juzuu tatu ambapo
alipewa zawadi ya shilingi 300,000 taslimu, tafsiri ya Qur-an moja na kitabu
cha fiqhi.
Washindi waliohifadhi
juzuu tatu, ni Said Muhibu kutoka Madrasat Ibaadh aliyepewa shilingi 200,000, Mussa
Juma pia kutoka Ibaadh aliyekuwa mshindi wa tatu na kupewa shilingi 100,000 na
msahafu mmoja wa tafsiri. Mohamed Mdone, Aisha Aboubakar na Mohamed Omari washindi
kwa waliohifadhi juzuu mbili na kupewa shilingi 50,000 kila mmoja.
TUMEKUWEKEA HAPA PICHA ZAIDI ZA SHINDANO LA USOMAJI NA UHIFADHI WA QUR - AN KWA MADRASA ZA MJINI SHINYANGA.
Baadhi ya watoto walioshiriki shindano la Usomaji na Uhifadhi wa Qur - an. |
Viongozi na waumini wakifuatilia kwa makini mashindano ya usomani na uhifadhi wa Qur - an |
Majaji na waongozaji nao walikuwa katika kuhakikisha haki inatendeka. |
Majaji kazini |
Mau-staadhi wa Madrasa zilizofanya vizuri pia walitunukiwa zawadi. |
Sehemu ya washindi wakipokea zawadi zao kutoka kwa mgeni rasmi, Sheikh Hilal Soud. |
Post a Comment