Waziri
wa kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini, Dkt. Charles Tizeba ametembelea kijiwe
maarufu cha kuuza kahawa kilichopo eneo la Soko kuu mjini Shinyanga ambapo alipata
nafasi ya kubadilishana mawazo na wananchi kuhusiana na masuala muhimu ya
kitaifa ikiwemo yanayogusa wizara yake.
Waziri
Tizeba katika kikao hicho kisicho rasmi ameweza kujibu hoja mbalimbali
zilizotolewa na wananchi ikiwemo suala la uhaba wa chakula katika maeneo mengi
nchini, ongezeko la bei ya sukari, kuzuka kwa wadudu waharibifu wa mazao na
kukwama kufanya kazi kwa kiwanda cha nyama kinachomilikiwa na kampuni ya Triple
“S.”
Akijibu
swali kuhusiana na na madai ya kuwepo kwa njaa katika baadhi ya maeneo hapa
nchini, Dkt. Tizeba hoja ya njaa inatafsiriwa vibaya na baadhi ya wanasiasa
wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wenye lengo la kutaka kutumia mwanya huo
kutengeneza fedha.
Akifafanua
alisema mpaka hivi sasa tafiti zinaonesha nchi bado ina akiba ya kutosha ya
chakula katika maeneo mengi na kwamba kinachodaiwa kuwa ni njaa ni uhaba wa
fedha kwa baadhi ya watu na serikali ina uhakika hakuna njaa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu wakiwemo wana siasa.
“Ndugu
zangu si kweli kwamba hapa nchini tuna njaa, la hasha, nasema hivi kwa
ushahidi, ninyi wenyewe tembeleeni maeneo mbalimbali katika masoko yetu
mtajionea hali halisi, vyakula ni vingi vipo, tatizo ni uhaba wa fedha kwa
baadhi ya watu, sasa hii huwezi kusema ni njaa,”
“Wapo
baadhi ya wanasiasa wanashinikiza kuitaka serikali itoe chakula cha akiba ili
kigawiwe bure kwa wananchi na kingine kiuzwe kwa bei rahisi, hawa hawatutakii
kheri, tukikurupuka na kukigawa ama kukiuzwa kwa bei rahisi, kitakapomalizika
basi wafanyabiashara watapata mwanya wa kuuza vyakula walivyonavyo kwa bei
kubwa sana,” alieleza Dkt. Tizeba.
Akitoa
mfano alisema, mtu anaweza kuwa mkoani Kagera na kudai kuna njaa kwa vile tu
migomba mingi imeharibiwa aidha na mvua au janga la tetemeko, hata hivyo akienda
katika masoko mengi ya mkoa huo atakuta kuna vyakula vingine tofauti na ndizi mfano
wa mahindi, mihogo na viazi vimejaa hali inayodhihirisha kutokuwepo kwa njaa.
Waziri Dkt. Tizeba akiagana na wananchi baada ya kumaliza maongezi yao, nyuma ya waziri ni mmoja wa wafanyabiashara maarufu katika Soko Kuu la Shinyanga mjini, Sancho Emily. |
Hata
hivyo alisema utaratibu uliokuwepo zamani wa serikali kugawa chakula bure hivi
sasa haupo tena na kwamba hakuna nchi ye yote duniani inayogawa chakula bure kwa
wananchi wake.
Aliendelea
kufafanua kuwa mpango wa serikali kwa hivi sasa ni kuwaelimisha wakulima waweze
kulima kisasa kilimo ambacho kitawawezesha kujipatia mavuno ya kutosha na
wafanye biashara badala ya kulima mazao ya chakula.
“Mpaka
sasa wakulima wetu bado hawajajikita vya kutosha katika suala zima la kilimo
cha kisasa na kinachozingatia utaalamu wa kilimo, wengi wanalima maeneo makubwa
lakini wanavuna mavuno machache ikilinganishwa na nguvu wanazotumia katika
kilimo,”
“Ndoto
yangu kwa hivi sasa ni kutaka kumsaidia mkulima wetu aweze kulima eneo dogo
lakini ambalo litamuwezesha kupata mazao mengi ya kutosha ikilinganishwa na
hivi sasa, ekari moja pekee ya mazao yoyote yale iwapo italimwa na kupandwa
kitaalamu inamuwezesha mtu kuondokana na umasikini,” alieleza.
Kwa upande mwingine waziri alifafanua kuwa ili nchi ionekane kukumbwa na njaa ni pale vyakula vya aina yote vitakapokuwa vimekosekana kwenye masoko na wakati huo wananchi wakiwa na fedha hawaoni chakula cha kununua tofauti na hali ilivyo hivi sasa ambapo panapotokea upungufu wa mahindi ama ndizi kwa watu wa Kagera watu wanasema nchi ina njaa wakati masoko yana vyakuna vingi vya aina nyingine.
Akizungumzia
suala la wafugaji wa ng’ombe, alisema mpaka hivi sasa bado wafugaji wengi
hawajanufaika na ufugaji wanaoufanya kutokana na kutokuwepo utaratibu maalumu
wa soko la mifugo yao pale wanapokwenda kuwauza minadani.
Alisema
wengi wa wafugaji bado wameendelea kuuza ng’ombe au mbuzi wao kienyeji bila
kujali uzito walionao kutokana na kutotumia mizani pale wanapowauza hali inayowakumba pia wafanyabiashara ya nyama ambao hununua kwa kukadiria tu ukubwa wa ng'ombe ama mbuzi anayenunuliwa.
“Mpango
wa wizara yangu na serikali kwa ujumla kwa hivi sasa ni kuhakikisha wafugaji
wananufaika na kile wanachokifuga kwa kuwawezesha pale wanapokwenda minadani kuuza
mifugo yao basi waiuze kwa kutumia mizani, siyo kwa kukisia kwa
macho tu,
“Pia
utaratibu huu utamwezesha mfanyabiashara wa nyama kumnunua ng’ombe mnadani
akiwa na uhakika wa faida atakayoipata baada ya mauzo, kwa vile atakuwa
anafahamu ng'ombe aliyemnunua ana uzito wa kilo ngapi na na kiasi atakachobaki nacho baada ya kuchinjwa na kuingizwa buchani,” alieleza Dkt. Tizeba.
Aliendelea
kueleza kuwa hata suala bei ya nyama kuwa kubwa katika jiji la Dar es Salaam na
miji mingine mikuu hapa nchini linachangiwa na wafanyabiashara kuendelea
kufanya biashara zao kizamani ambapo alitoa mfano ng'ombe kusafirishwa akiwa alivyo kwenye maroli kutoka mikoa ya kanda ya Ziwa na kwenda kuchinjiwa Dar es Salaam.
“Kwa
utaratibu huu wa sasa wa kumsafirisha ng’ombe kwenye Semi trailer kutoka mikoani hadi Dar es Salaam akiwa na kwato,
pembe, ngozi na matumbo yake, lazima nyama iuzwe kwa bei ya juu sana, na inachangiwa na watanzania kuendelea na kasumba ya kutaka kula nyama inayovuja damu,”
“Lakini iwapo ng’ombe huyo huyo angechinjiwa
hukohuko katika machinjio ya kisasa na kusafirisha nyama pekee kwa kutumia
vifaa maalum ni wazi nyama ingeuzwa kwa bei ya chini na kusafirishwa kwa wingi kwa wakati mmoja tofauti na kumsafirisha ng'ombe mzima na hivyo kumuwezesha
mfanyabiashara kupata faida kubwa,” aliendelea kufafanua.
Aidha
waziri alikiri kuwepo kwa ongezeko la bei ya sukari katika maeneo mengi nchini
ambapo alisema taarifa za wiki iliyopita zimeonesha baadhi ya maeneo kilo moja
ya sukari ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi 3,000 na kwamba hali hiyo imechangiwa na
viwanda kusimamisha uzalishaji kipindi hiki cha masika.
Akizungumzia
suala la uwepo wa wadudu waharibifu wa mazao katika maeneo mengi nchini, swali
aliloulizwa na mkazi wa kata ya Ndala, Erick Ngezabuke, Dkt. Tizeba alisema
tatizo hilo linachangiwa na ugumu wa kukabiliana na wadudu hao kutokana na
mashamba mengi kulimwa kwenye maeneo ya makazi ya watu.
“Ni kweli lipo tatizo la wadudu waharibifu katika maeneo mengi hapa nchini hasa viwavi jeshi, na si hapa nchini tu, hata katika nchi jirani tatizo hili lipo, na hii inachangiwa na mashamba mengi kuwa madogo madogo na yapo katika makazi ya watu,”
“Hata
hivyo tunawashauri wakulima wetu kwa hili hakuna sababu ya kusubiri serikali,
waungane watatu ama watano watano wanunue vifaa pamoja na dawa za kuulia wadudu
hawa, bei siyo kubwa sana, wanaweza kunyunyuzia kwa kupeana zamu, na sisi
serikali tutafanya kazi hii kwenye mashamba makubwa,” alieleza.
Waziri akitolea ufafanuzi swali aliloulizwa na Bw. Erick Ngezabuke mkazi wa kata ya Ndala kuhusiana na ongezeko la wadudu waharibifu wa mazao ikiwemo viwavijeshi. |
Kuhusu
uendelezwaji wa kiwanda cha nyama kilichoshindwa kuanza uzalishaji kwa zaidi ya
miaka 25 hivi sasa, Dkt. Tizeba alisema hawezi kukizungumzia kwa vile tayari
Rais Dkt. John Magufuli alitoa maelekezo kwa viongozi wa serikali mkoani Shinyanga
na tayari kuna hatua zinaendelea kuchukuliwa.
Alisema
pamoja na maelekezo yaliyotolewa na Rais Magufuli bado anaamini kiwanda hicho
kitabaki katika lengo lake la awali la uchinjaji na usindakaji wa nyama hata baada ya
kupatikana kwa mwekezaji mwingine, swali hilo lilikuwa limeulizwa na
mfanyabiashara wa Soko Kuu Sancho Emily.
Post a Comment