Sehemu ya mafuvu ya vichwa vya wanyarwanda waliouawa mwaka 1994 nchini Rwanda. |
Hakimu mmoja wa mahakama maalumu ya kusimamia
kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ameulaumu uongozi wa kanisa
katoliki kwa kuwalinda washukiwa waliohusika ambao ni viongozi wa dini.
Katika mahojiano aliyoyafanya na gazeti la "Badisches Tagblatt"
la Ujerumani, jaji Wolfgang Schomburg amewanyooshea viongozi wengi kidole:
Schomburg aliyekuwa sehemu ya jopo la majaji lililosimamia kesi ya mauaji ya
kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 amewataka mapadri wa kikatoliki waliohusika
katika mauaji hayo ya kinyama wafikishe mahakamani. Schomburg ameukosoa uongozi
wa kanisa katoliki, Vatikan, kwa kuwalinda mapadri hao ambao wanapaswa
kufikishwa mbele ya sheria.
Ni kweli kwamba vipo visa ambapo uongozi wa kanisa katoliki
uliamua kuwapatia hifadhi viongozi wa kiroho ambao walihusika moja kwa moja
kwenye mauaji ya kikatili.
Mmoja wao ni padri Wenceslas Munyeshyaka. Yeye mwaka 1994
alibeba bunduki kama mwanajeshi na kupanga njama na waasi wa Kihutu. Waasi hao
waliwaua mamia ya watu waliokuwa wametafuta hifadhi ndani ya kanisa la padri
Munyeshyaka. Padri huyo baadaye alihamia Ufaransa. Mahakama moja ya nchini
Rwanda ilimhukumu adhabu ya kifungo cha maisha lakini kanisa katoliki nchini
Ufaransa lilimtetea na kusema kuhukumiwa kwa Munyeshyaka kwa mauaji ya kimbari
si sababu ya kumfanya asiendelee na kazi yake ya upadri.
Mapadri
wafichwa Ulaya
Padri Munyeshyaka hayupo pekee yake. Mapadri na masista
waliofahamika kuhusika katika mauaji ya Rwanda walipelekwa Ulaya na kupatiwa
hifadhi huko. Miongoni mwao alikuwa Padri Athanase Seromba aliyeruhusu kanisa
lake libomolewe likiwa na Watutsi 2,000 ndani. Wale walioponea walifyatuliwa
risasi na kuuliwa. Kanisa Katoliki lilimsaidia kukimbilia Italia na hata
kuhakikisha kwamba anapwea jina jipya na pasipoti mpya.
Mbali na viongozi hao wa dini, bado wapo wanasiasa na wanajeshi
waliohusika ambao kamwe hawakuwahi kufikishwa mahakamani au kufunguliwa
mashtaka. Jaji Schomburg amekumbusha kuwa bila kuwepo kwa mahakama maalumu ya
Umoja wa Mataifa, watu wengi waliosababisha maafa ya Wanyarwanda wapatao
800,000 wangeweza kuukwepa mkono wa sheria.
Rwanda
imepiga hatua
Pamoja na hayo, jaji huyo wa zamani amekosoa pia namna ambavyo
jumuiya ya kimataifa ilichelewa kuingila kati mgogoro wa Rwanda hadi pale
ambapo mamia kwa maelfu ya raia, wengi wao Watutsi, walipokuwa tayari
wameuliwa. "Hata mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia mauaji ya
kimbari ya Rwanda ilianzishwa kwa kuchelewa," anakosoa Schomburg.
"Mahakama hiyo ilipaswa iundwe mwishoni mwa mwaka 1993 au mwanzoni mwa
1994."
Lakini jaji huyo, ambaye alifanya kazi kwenye mahakama hiyo
kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, hakuishia hapo. Ameelezea kushangazwa kwake na
ukweli kwamba hakuna Mfaransa hata mmoja aliyefunguliwa mashtaka, licha ya
kwamba baadhi ya Wafaransa walituhumiwa kuuza silaha nchini Rwanda katika miaka
ya 1990 na kwamba wakati mwingine hata walizigawa silaha hizo kwa Wahutu.
Wakati fulani serikali ya Rwanda ilijaribu kuwafungulia mashtaka
wahusika, lakini bila mafanikio. Schomburg anasema Ufaransa haina nia ya kweli
kufanya uchunguzi wa kipindi hicho kilichogubikwa na giza.
Lakini Schomburg ameisifu mahakama ya Umoja wa Mataifa ya
kushughulikia mauaji ya kimbari ya Rwanda kwa kupiga hatua za haraka
kuwawajibisha wahusika na kuwapatia haki wale walioonewa na hii imekwenda
haraka hata kuliko vile ambavyo Ujerumani ilivyoendesha kesi za waliohusika
katika mauaji ya Wayahudi chini ya utawala wa Wanazi.
Chanzo: DW Idhaa ya Kiswahili.
Post a Comment