Mbunge wa Babati Mashariki, Pauline Gekul |
Kwa mujibu
wa kile kilichoelezwa kuhusiana na faru huyo ambaye pia yupo katika Hifadhi ya
Ngorongoro mkoani Arusha kama ilivyokuwa kwa faru John, ni kwamba gharama za
kumtunza kwa mwezi ni Sh. milioni 64 na hivyo kushtua baadhi ya wabunge kiasi
cha kuibua maswali.
Kwa mujibu
wa chanzo cha Nipashe, mshahara wa mbunge mmoja kwa mwezi kabla ya makato ni
takribani Sh. milioni 3.6, hivyo gharama hizo za kumtunza Faru Fausta ni sawa
na wastani wa mishahara ya wabunge 17 kabla ya makato.
Aliyeibua
suala hilo la Faru Fausta ni Mbunge wa Babati Mjini(Chadema),Pauline Gekul,
ambaye alidai kushtushwa na kitendo cha Hifadhi ya Ngorongoro kutumia kiasi cha
Sh. Milioni 64 kwa mwezi sawa na Sh.Milioni 768 kwa mwaka kumlisha na kumtunza
faru huyo.
Akiuliza
swali la nyongeza kwa Waziri wa Maliasili na Utalii bungeni jana, Gekul alisema
faru huyo amekuwa akigharimiwa fedha nyingi na kuhoji serikali ina mpango gani
kuhusiana naye.
Akijibu
swali hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, alikiri faru
huyo kutunzwa kwa gharama kubwa kwa ajili ya kumlisha kwa sababu ni mzee.
Alisema
mbali na hilo, mnyama huyo pia huandamwa na magonjwa mbalimbali na ndiyo maana
ana gharimiwa kwa fedha zinazoonekana kuwa ni gharama kubwa.
Aidha, Prof.
Maghembe alisema wanafanya hivyo pia kwa sababu wanyama wa aina hiyo ni
wachache katika hifadhi nchini.
“Hivi sasa
utafiti unafanyika kwa kumtumia faru Fausta juu ya namna ya kuishi na wanyama
wa aina hiyo ili waweze kuishi maisha marefu… ni kweli kufanya hivi ni gharama
kubwa lakini takwimu zinazopatikana zina thamani halisi,”alisema.
Pamoja na
majibu hayo, Waziri Maghembe aliendelea kubanwa kuhusiana na gharama za faru
huyo.
Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka, aliomba mwongozo baada ya
kipindi cha maswali na majibu kuhusu majibu ya waziri huyo juu ya faru Fausta
kutunzwa kwa fedha hizo huku ikielezwa kuwa ni mzee ilhali ikifahamika kuwa kwa
hali yake, kamwe mnyama huyo hawezi kuingiza faida yoyote.
Akijibu
muongozo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema katika hifadhi hiyo yupo pia
Faru Ndugai na kumwambia waziri kwa kutania kuwa siku faru huyo (Ndugai)
akitoweka patachimbika bungeni.
Hata hivyo,
kuhusiana na swali kuhusu faru Fausta, Ndugai alisema suala hilo analiachia
wizara ili wakalifanyie kazi.
TAARIFA
ZAIDI KUHUSU FARU FAUSTA
Kwa mujibu
wa Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk Freddy Manongi, ambaye alizungumza na
Nipashe hivi karibuni, ni kwamba faru Fausta ni mzee mwenye miaka 54 na kwamba,
alipokuwa porini alikuwa akishambuliwa na fisi na kupata vidonda vingi.
Alisema
baada ya kumwona fausta akiwa katika hali mbaya kiafya na pia kuwa katika
hatari kubwa ya kuuawa na fisi kutokana na uzee wake, askari wa uhifadhi
walimchukua na kumtengea eneo maalum huku wakilazimika kimnunulia chakula kama
miwa kutoka wilayani Babati na pia kumpatia huduma nyingine muhimu.
Alisema
kutokana na jitihada zinazofanyika katika kumtunza, hivi sasa vidonda aliyokuwa
navyo vimepona na anaendelea vizuri.
Hata hivyo,
taarifa nyingine kutoka kwenye hifadhi hiyo jana zilidai kuwa kutokana na umri
wake mkubwa, faru huyo hivi sasa ana tatizo la kutoona na jambo hilo linamuweka
katika wakati mgumu kimaisha ikiwa ataachiwa aishi porini bila ya uangalizi
maalumu.
Chanzo: Nipashe.
Post a Comment